Ujerumani yaweka rekodi ya mabao Euro

Muktasari:

  • Uswis ilianza vizuri kwenye mchezo huo baada ya kuongoza kwa muda mrefu, lakini Ujerumani ikasawazisha mwishoni na kupata nafasi ya kumaliza kama kinara wa kundi hilo ikiwa na pointi saba na mabao nane.

Ujerumani imefanikiwa kumaliza kileleni kwenye Kundi A, la michuano ya Euro 2024, baada ya juzi kupata bao la jioni na kumaliza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Uswiss huku ikiweka rekodi ya mabao.

Uswis ilianza vizuri kwenye mchezo huo baada ya kuongoza kwa muda mrefu, lakini Ujerumani ikasawazisha mwishoni na kupata nafasi ya kumaliza kama kinara wa kundi hilo ikiwa na pointi saba na mabao nane.

Hii ni mara ya kwanza Ujerumani inafunga mabao mengi kiasi hicho kwenye hatua ya makundi tangu mwaka 2006.

Pamoja na Ujerumani, timu nyingine iliyofuzu kutoka kwenye Kundi A ni Uswiss ambao wamemaliza na pointi tano huku Hungary ikiwa na pointi tatu na ya mwisho kwenye kundi hilo ni Scotland ambayo imemaliza na pointi moja.

Sasa Ujerumani inasubiri kufahamu timu itakayomaliza nafasi ya pili kwenye Kundi C ili kuvaana nayo kwenye hatua ya 16 Bora, zinazopewa nafasi kubwa ni England yenye pointi nne au Denmark yenye pointi mbili, huku Uswiss yenyewe ikisubiri kukutana na mshindi wa pili Kundi B kwenye hatua hiyo.

Hungary ambayo imemaliza nafasi ya tatu kwenye kundi hilo inaweza pia kufuzu hatua ya 16 Bora baada ya makundi yote kumaliza mechi zake kama itamaliza kama mshindwa bora 'best loser' kwenye nafasi nne ambazo zinatakiwa ili timu zitimie 16.

Mechi za leo Albania inavaana na Hispania ambayo tayari imeshafuzu 16 bora huku Italia ikivaana na Croatia zikiwa ni mechi za mwisho kwenye kundi B.