VAR kuanza kutumika Ligi Kuu Bara

Iringa. Muda sio mrefu ujao, baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara zitaanza kuamriwa kwa usaidizi wa teknolojia ya video ya waamuzi (VAR).
Hiyo ni kufuatia uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuipa Tanzania vifaa vya VAR ambavyo vitafungwa katika baadhi ya viwanja.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unaofanyika Iringa, Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia amesema ufungwaji wa vifaa hivyo utafanywa katika viwanja vinavyokidhi vigezo vya CAF na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa).
"Niwape habari njema kuwa tumepata VAR kutoka CAF na hii ni mwendelezo wa uhusiano mzuri na CAF. Wataalamu wameingia jana kutoa mafunzo. Itafungwa katika viwanja vyenye standard (ubora)," amesema Karia.
"Kamati ya waamuzi kwa vile tumewapa jukumu la usimamizi mtasaidia katika mafunzo na uzuri tunaye mkufunzi wa waamuzi wa CAF, Leslie Liunda ambaye atakuwa mratibu wa hayo mafunzo."
Karia amesema kuwa wanaangalia pia uwezekano wa VAR kufungwa katika Uwanja wa Amaan Zanzibar ikiwa ni katika kuhakikisha kwamba mchezo wa soka unaendelea kupata mafanikio hapa nchini.
Mjadala wa ufungaji VAR katika viwanja vya soka nchini umewahi kuwaibua kwa nyakati tofauti mawaziri wa sasa, Mohammed Mchengerwa ambaye ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi) wakati huo akiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mwigulu Nchemba (Fedha).
Mchengerwa alisema kuwa serikali ilikuwa na mpango wa kushughulikia kuleta vifaa vya VAR nchini kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu Bara -kauli iliyokuja wakati kukiwa kumetawala mijadala juu ya waamuzi kufanya madudu katika mechi za Ligi Kuu.
Nchemba pia alisema serikali italeta VAR ili kuwezesa haki kupatikana katika michezo ya Ligi Kuu baada ya kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka.