Vijana wafichua kufufua michezo kutapunguza ulevi Rombo
Wachezaji wa timu mbalimbali wilayani Rombo wakiwa pamoja kabla ya uzinduzi wa mashindano ya msimu wa pili wa Rombo Samia football tournament katika viwanja vya mpira Rongai.
Muktasari:
- Vijana wampa heko Profesa Mkenda wasema ufufuaji wa michezo utawapunguzia ulevi Rombo
Rombo. Vijana Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wamemshukuru Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda kwa namna alivyoibua michezo katika wilaya hiyo na kusema itawapa fursa ya kufanya shughuli za michezo na kuacha kujiingiza kwenye mambo ya ulevi.
Wameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa msimu wa pili wa mashindano ya mpira wa miguu ya 'Rombo Samia Football Tournament' ambayo yamezinduliwa na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande katika Uwanja wa Rongai uliopo Tarafa ya Tarakea, wilayani humo.
Akizungumzia uzinduzi wa mashindano hayo, mmoja wa vijana hao, Julius Shayo amesema uzinduzi wa mashindano hayo utatoa fursa mpya kwa vijana wilayani humo kujishughulisha na mambo ya michezo na kuacha kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa ikiwemo kwenye ulevi.
"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wetu wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda kwa kufufua michezo katika wilaya hii lakini itatusaidia sisi vijana kutojiingiza kwenye makundi ya ulevi kwa kuwa michezo ni ajira na inaleta afya,"amesema
Mkazi wa Rongai, Erasmi Edward amesema kufufuliwa kwa michezo katika wilaya hiyo kutasaidia kuibua vipaji vingi kwa vijana na kuwahamasisha kujiingiza kwenye sekta hiyo ya michezo.
"Tunamshukuru mbunge wetu, Profesa Adolf Mkenda kwa kutuwezesha na kujali sera yake ya michezo, amejali kwa vitendo na siyo kwa maneno na kwa sasa katika wilaya hii kuna utofauti kubwa sana na vipindi vilivyopita, vijana walikuwa nyuma kimichezo lakini kadri siku zinavyozidi kwenda kupitia mashindano haya vijana wamebadilika," amesema.
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, amempongeza Profesa Mkenda kwa ubinifu huo wa kuibua vipaji kwa vijana kupitia mashindano hayo na kusema Rombo inaweza kuwa na wachezaji wakubwa wa soka la Tanzania.
"Nampongeza mbunge kwa kazi kubwa na adhimu anayoifanya katika wilaya hii ya Rombo, niwapongeze vijana wetu hawa kwa namna mlivyojitokeza kwa wingi na namna mnavyopiga soka," amesema.
Amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani amefanya mageuzi makubwa katika sekta ya michezo na kwamba Tanzania imefika mbali na imekuwa ikifanya vizuri katika ligi za Afrika.
Akizungumzia mashindano hayo, Profesa Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia amesema mashimdano hayo yamelenga kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa anayoyafanya katika wilaya hiyo ikiwemo Serikali kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
"Uzinduzi wa mashindano haya ya 'Rombo Samia Football Tournament' yamelenga kumshukuru Rais wetu, Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa mambo makubwa anayoyafanya hapa Rombo na nchi nzima kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali," amesema Profesa Mkenda.