Yanga kukutana na hawa robo fainali CAFCL

Muktasari:
- Yanga imemaliza ikiwa nafasi ya pili katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa imekusanya pointi nane.
Dar es Salaam. Yanga inaweza kukutana na ASEC Mimosas ya Ivory Coast au timu itakayoongoza kundi A au C kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo itafanyika mwishoni mwa mwezi huu na mwanzoni mwa mechi ijayo.
Kitendo cha kumaliza katika nafasi ya pili baada ya kufungwa bao 1-0 na Al Ahly huko Cairo, Misri jana kinaifanya Yanga imalize ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi D na pointi zake nane, nyuma ya Ahly ambayo ni kinara ikiwa na pointi 12.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu inayomaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi, inakutana na timu iliyoongoza kundi lingine katika hatua ya robo fainali.
Lakini pia katika hatua hiyo, timu haiwezi kukutana na timu ambayo ilipangwa nayo kundi moja jambo ambalo linaifanya Yanga iwe na uhakika wa kutokutana na Al Ahly.
Kwa maana hiyo, Yanga inaweza kukutana na ASEC ambayo tayari imejihakikishia uongozi wa kundi B la mashindano hayo.
Kama sio ASEC, Yanga inaweza kukutana na mshindi wa kundi A ambalo hadi sasa kinara wake hajajulikana na mechi ya leo baina ya Mamelodi Sundowns dhidi ya TP Mazembe itakayochezwa Afrika Kusini ndio itaamua timu ipi inamaliza ikiwa kileleni mwa kundi hilo.
Hadi timu hizo mbili zinaingia kwenye mechi ya leo, TP Mazembe inaongoza ikiwa na pointi 10 sawa na Mamelodi Sundowns lakini inabebwa na kigezo cha kuwa na matokeo mazuri katika mechi ambayo timu zilikutana mwanzoni.
Yanga pia inaweza kukutana na mshindi wa kwanza wa kundi C ambalo hadi sasa, kinara wake hajajulikana licha ya kwamba linaongozwa na Petro Luanda ya Angola yenye pointi tisa.
Kama Al Hilal ya Sudan itapata ushindi ugenini dhidi ya Esperance, Yanga itaumana na Petro Luanda katika robo fainali lakini kama Esperance itashinda na kisha Petro Luanda ikapoteza au kutoka sare na Etoile du Sahel, maana yake Yanga itakutana na Esperance katika robo fainali.