Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yaizamisha Polisi kwa Mkapa, Mayele huyoo..

Muktasari:

  • Bao la Fiston Mayele katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Polisi Tanzania linamfanya nyota huyo kuongoza kwenye mbio za ufungaji bora hadi sasa baada ya kufikisha 11 akimuacha Moses Phiri (Simba) mwenye 10.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga imeanza vyema mzunguko wa pili baada ya kuifunga Polisi Tanzania mabao 3-0, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. 

Mabao ya Yanga yalifungwa na Jesus Moloko dakika ya 47 akipokea pasi ya Bernard Morrison aliyeingia muda mchache huku la pili likiwekwa kimiani na Fiston Mayele dakika ya 77 wakati la tatu likifungwa na Clement Mzize dakika ya 86.


Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huo.

Ushindi huu kwa Yanga unaifanya kupata pointi zote sita dhidi ya wapinzani wao baada ya mchezo wa mzunguko kwanza uliopigwa Agosti 16 kushinda pia mabao 2-1, mechi iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. 

Tangu Polisi Tanzania ilipopanda rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020 haijawahi kuifunga Yanga kwani mchezo huu ni wa nane kwao kukutana ambapo kati ya hiyo imefungwa mara tano na kutoa sare tatu tu. 

Katika michezo hiyo Yanga imefunga jumla ya mabao 14 huku kwa upande wa Maafande wa Polisi Tanzania wakifunga sita. 

Huu ni mchezo wa pili kwa Kocha, Mwinyi Zahera kukiongoza kikosi cha Polisi Tanzania tangu alipokabidhiwa jukumu hilo Desemba 2 akichukua nafasi ya Mrundi, Joslin Bipfubusa aliyetimuliwa Oktoba 26 kutokana na matokeo mabovu. 

Mchezo wa kwanza kwa Zahera alianza kwa kichapo pia cha bao 1-0 na Azam FC, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi Desemba 5.
Kadi nyekundu aliyopata nyota wa Polisi Tanzania, Ambrose Awio ni ya 17 kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu huku kinara akiwa ni beki wa timu hiyo, Mohamed Mmanga aliyepata mbili.

Awio anakuwa mchezaji wa pili wa Polisi Tanzania kupata kadi nyekundu dhidi ya Yanga baada ya Mohamed Mmanga kufanya hivyo wakati timu hizo zilipokutana raundi ya kwanza Agosti 16.

Kichapo hiki kinaifanya Polisi Tanzania kupoteza michezo minne mfululizo baada ya kufungwa (2-1) Vs Mtibwa Sugar, Novemba 21, (3-1) Vs Simba Novemba 27 na 1-0 Vs Azam FC Desemba 5.

Hiki ni kipigo cha 11 kwa Polisi Tanzania msimu huu katika michezo 16 iliyocheza ambapo kati ya hiyo imeshinda miwili tu na kutoa sare mitatu ikiendelea kusalia mkiani na pointi zake tisa. 

Bao la Fiston Mayele linamfanya nyota huyo kuongoza kwenye mbio za ufungaji bora hadi sasa baada ya kufikisha 11 akimuacha nyuma nyota wa Simba, Moses Phiri mwenye 10.

Kwa upande wa Yanga huu ni ushindi wa 13 katika michezo yake 16 iliyocheza ikitoa sare miwili na kupoteza mmoja ikiendea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 41.