Yanga yawekewa Sh300 milioni kuiua Rivers

KUNA kila dalili Rivers United wakaangukiwa na kitu kizito leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa. Kocha wa viungo, Helmy Gueldich na bosi wake, Nasreddine Nabi wameshamaliza kazi yao kambini huku tajiri nae akiweka Sh300milioni mezani.

Helmy amesisitiza kwamba mastaa amewapika na wako fiti tayari kwa historia huku Nabi akisema watapambana kwa nguvu kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho na amewaonya wachezaji wasibweteke na unyonge wa Rivers na maneno yao ya mitandaoni.

Helmy ambaye ni raia wa Tunisia, ameliambia Mwanaspoti kuwa  amefanya tathmini ya kikosi chake na kubaini kwamba wana ratiba ngumu baada ya Jumapili ndio maana wamekaa chini na kocha Nasreddine Nabi na kuweka mkakati mzito.

"Tunahitaji matokeo ya ushindi ili kutinga hatua ya nusu fainali hivyo tutamia nguvu nyingi, baada ya hapo tutasafiri kuikabili Singida Big Stars nimezungumza na Nabi kuhakikisha anatafuta namna ya kuwatumia wachezaji wake ili waweze kumaliza ligi bila ya majeraha,"alisema.

Helym alisema ili timu hiyo iweze kumaliza vizuri msimu bila ya majeraha kwa mastaa wake ni kuhakikisha kocha anakuwa na mabadiliko ya kikosi chake kwenye mechi tatu zilizo mbele yao kuanzia Jumapili.

Alisema amefanya mazungumzo na Nabi anaamini kwenye michezo hiyo kutakuwa na mabadiliko makubwa huku akisisitiza kuwa kikosi chao kina wachezaji bora na wenye uchu wa ushindani huku akiweka mastaa wao wote wako fiti kwa asilimia 90.

"Ni suala la muda tu kuona mabadiliko kikosini hasa kwenye mechi mbili dhidi ya SBS kwasababu kocha amenihakikishia hilo kutokana na kuhitaji huduma ya wachezaji wake wote wakiwa fiti ili kumaliza msimu wakiwa kwenye hali nzuri;

"Wachezaji wote kuanzia kikosi cha kwanza ambacho kimekuwa kikitumika mara kwa mara wapo kwenye hali ya ushindani na wana morali nzuri ya ushindani lengo lao ni kuona wanafikia lengo la kutinga hatua ya nusu fainali," alisema.

Helmy alisema ushindani wa wachezaji wenyewe kwa wenyewe unaongeza nguvu kwa benchi la ufundi kukosa chaguo muhimu ambalo linaweza kuipa timu matokeo mazuri.
"Timu ikitoka kucheza mchezo inatakiwa kwenda Gym au kuingia kwenye mabarafu ili kurudisha miili yao kwenye ubora hilo limekuwa likifanyika na pia vyakula wanavyokula inaweza kuwa moja ya chachu ya utimamu wao," alisema.


Mechi yenyewe
Itaanza saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa. Yanga inahitaji ushindi wowote au hata sare kutinga nusu fainali baada ya kuwafunga Rivers kwao kwenye mchezo wa kwanza kwa mabao 2-0 wakilipa kisasi cha kwanza dhidi ya Wanaigeria hao.

Yanga wanasema bado kisasi hicho hakijakamilika wakitaka kuwafunga na hapa pia baada ya Rivers kuwafunga Yanga miaka miwili iliyopita hatua ya mtoano wa awali wa Ligi ya Mabingwa mechi zote mbili matokeo yakimalizika kwa Yanga kupoteza kwa bao 1-0.

Yanga imechukua tahadhari zote kuhakikisha wapinzani wao hawapindui meza hapa nyumbani ambapo kambini kwao wamekuwa wakijiandaa kusaka uimara wa safu yao ya ulinzi lakini pia kule mbele kunoa makali yao ya kusaka mabao yatayowapa ushindi.

Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba ukiondoa kipa wao Aboutwalib Mshery ambaye ni majeruhi wa muda mrefu wachezaji wao wengine wote wako salama ni uamuzi wa benchi la ufundi watachagua mastaa gani watakaoikamilisha historia yao.

Tayari tajiri wao namba moja Ghalib Said Mohamed 'GSM' hakutaka kuchelewa ameshatangaza kuwa kuna Sh300 milioni mezani wakimaliza kwa ushindi mchezo huo huku pia zile fedha za hapo kwa hapo kutoka wa Rais Samia Suluhu Hassan zikiendelea ni uamuzi wao Yanga kushinda ngapi.
Shirikisho la Soka Afrika CAF wao kupitia idara yao ya mashindano imeshaweka bayana kuwa mchezo huo utasimamiwa na waamuzi wote kutoka Morocco Redouane Jiyed wa kati,  akisaidia na msaidizi wake wa kwanza Lahsen Azgaouna wa pili ni Mostafa Akarkad huku mwamuzi wa akiba akiwa Jalal Jayed.

Takwimu zinaonyesha Jiyed ambaye amecheza jumla ya mechi 17 za kimashindano hana historia ya kutoa kadi nyekundu kwa timu mwenyeji akiwa amecheza mchezo mmoja wa shirikisho msimu huu wa hatua ya makundi kati ya Marumo Gallats ya Afrika Kusini dhidi ya FC Lupopo na wenyeji kushinda kwa mabao 3-2.

Kocha wa Yanga Nabi akizungumzia mchezo huo alisema wamekuwa katika msisitizo mkubwa wa kuondoa ushindi wao wa kwanza kwenye akili za wachezaji wao na kufanikiwa ambapo sasa wanakwenda kutafuta ushindi mwingine nyumbani.

"Kuna wakati mchezo wa soka unakuwa na maajabu yake, unapoamini sana umeshinda utakutana na mshtuko ambao utakuondoa kwenye malengo yako, unajua tulishinda kweli ugenini lakini sisi makocha tunajua kwamba Rivers bado ina kitu ambacho inaweza kufanya hapa kwetu na wakashinda,"alisema Nabi.

"Tunawaheshimu Rivers na tutaingia uwanjani kutaka kushinda kwa dhamira kubwa, nimefurahia mazoezi yetu tangu turejee nchini,kambini kumekuwa na morali kubwa, tutakuwa mbele ya mashabiki wetu bora tunakwenda kupambana kushinda hiki ndicho naweza kusema."

Staa wa Yanga mshambuliaji Fiston Mayele mwenye mabao manne msimu huu Afrika, akiwa katika kiwango chake bora anarudi uwanja wa nyumbani akiwatisha Rivers kufuatia kuwatungua mabao mawili katika kipigo chao cha kwanza Mkongomani huyo akisaka rekodi nyingine ya kuendelea kuibeba timu yake.

Rivers wao kuna akili wanaitumia kuwazuga Yanga kwamba wamekata tamaa wakidai safari yao ya kutua nchini imekubwa na mazingira ya ukata maneno ya kocha wao Stanley Eguma kauli ambayo Yanga hawataki kuamini wakidai 'anacheza na akili zetu'.

Yanga inajua kuwa Rivers haikuwatumia wachezaji wao watatu muhimu wakieleza walikuwa majeruhi na kama mshambuliaji wao Paul Acquah atakuwa tayari kwa mchezo huo anaweza kurudisha uhai wa safu yao ya ushambuliaji.

Acquah raia wa Ghana amefunga mabao manne katika mechi 6 za hatua ya makundi yakiwemo mabao matatu Hat trick aliyoipiga nyumbani  aliyowapiga Motema Pembe wakishinda kwa mabao 3-1 endapo atacheza leo safu ya ulinzi ya Yanga itatakiwa kuwa naye makini asije watibulia shughuli.