CCM Arusha yatangaza walioteuliwa kuwania udiwani kata 160, Dogo Janja ndani
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Arusha, Saipulan Ramsey akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu
Muktasari:
- Katika uteuzi huo wa wagombea wataopeperusha bendera ya CCM kuwania udiwani katika uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho itatoa uamuzi kwenye Kata ya Olasiti na Viti Maalumu Tarafa ya Elerai za jijini Arusha.
Arusha. Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Arusha kimetangaza majina ya walioteuliwa kuwania nafasi ya udiwani katika kata 160 zilizopo mkoani hapa na udiwani Viti Maalumu isipokuwa Kata ya Olasiti na Tarafa ya Elerai kwa Viti Maalumu.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoani Arusha, Saipulan Ramsey akitangaza uteuzi huo amesema umezingatia katiba,kanuni na miongozo ya chama hicho katika kuwapata wanachama wake wanaowania kushika nafasi kwenye vyombo vya dola.
Amesema CCM imezingatia haki za kila mwanachama kuwania nafasi za uongozi na kufuata taratibu zake katika mchujo wa awali hadi wa wanachama kuwapigia kura za maoni na uteuzi jambo linalokifanya chama hicho kuongoza katika michakato ya kuwapata wagombea wake.
“Tunashukuru Mungu tumefikia hatua ya kuwatangaza walioteuliwa na vikao halali vya Chama cha Mapinduzi kuwa wamekidhi sifa, hata wale walioleta malalamiko yao yamefanyiwa kazi kwa kusikiliza pande zote na kutoka na uamuzi wa vikao ambao umewateua wagombea niliowataja,” amesema Ramsey.
Kuhusu watia nia Kata ya Olasiti na Viti Maalumu tarafa ya Elerai za jijini Arusha, amesema kulikuwa na malalamiko yaliyowasilishwa na uchunguzi unaendelea juu ya tuhuma hizo kisha maamuzi yatatolewa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa.
Hata hivyo katika kata 160 ni wagombea wanawake wanne pekee ndio walioteuliwa kuwania nafasi ya udiwani.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Msanii wa muziki wa kizazi kipya Dogo Janja katika Kata ya Ngarenaro na wengine ni Melace Kinabo Kata ya Themi, Julius Sekeyani Kata ya Terrat na Elirehema Nnko Kata ya Osunyai waliowahi kuwa madiwani kwenye mabaraza yaliyopita kabla ya baraza lililovunjwa mwaka huu majina yao kuteuliwa tena.