Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yawarejesha watiania udiwani wote walioenguliwa

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla

Muktasari:

  • Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kuwarejesha wagombea wote wa nafasi ya udiwani waliokuwa kwenye orodha ya awali na waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa, ili wote washiriki kwenye kura za maoni. Hatua hiyo inafuatia malalamiko mengi kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu uhalali na usawa wa mchakato wa awali wa uteuzi.

Dar es Salaam. Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetoa uamuzi mzito wa kurejesha wagombea wote wa nafasi ya udiwani katika kata mbalimbali nchini kwenye mchakato wa kura za maoni itakayofanyika Jumatatu, Agosti 4, 2025.

Hatua hiyo ni ya kujibu malalamiko ya wanachama na wananchi yaliyowasilishwa kutoka maeneo mbalimbali nchini kupinga watiani wao kuenguliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, uamuzi huo umetolewa kutokana kikao cha sekretarieti kilichofanyika jana Alhamisi Julai 31, 2025.

Taarifa hiyo inaeleza wagombea wote waliokuwa kwenye orodha ya awali ya nafasi ya udiwani, pamoja na wale waliopitishwa na kamati za siasa za mikoa, wanapaswa kurejeshwa kwenye orodha rasmi ya kura za maoni bila kuondolewa.

Hii inamaanisha mchakato huo sasa utakuwa wa wazi zaidi, ukitoa nafasi kwa wanachama wa CCM kufanya uamuzi wao moja kwa moja kupitia kura.

“Wagombea wote waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa warejeshwe rasmi kwenye orodha ya kura za maoni. Vilevile, wagombea wote waliokuwemo kwenye orodha ya awali waliotumwa kwa makatibu wa mikoa waruhusiwe kushiriki kura hizo,” imeeleza taarifa hiyo.

Makalla amefafanua maelekezo hayo mapya yanabatilisha maagizo yote ya awali yaliyotolewa kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi ya udiwani na sasa maagizo haya ndiyo yanatakiwa kuzingatiwa na kutekelezwa kikamilifu.

Kulingana na taarifa hiyo, maagizo hayo yamelenga kuhakikisha haki, usawa na utulivu ndani ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jumatano, Oktoba 29, 2025.

 Sekretarieti imehimiza utekelezaji wa maagizo hayo ufanyike mara moja, bila kucheleweshwa na kuzingatia miongozo ya chama.

Uamuzi huo umekuja katika kipindi ambacho kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo baadhi ya wanachama wa CCM na wananchi walieleza kutoridhishwa na mchakato wa awali wa uchujaji wa majina ya wagombea wa nafasi ya udiwani.

 Baadhi ya malalamiko hayo yalihusu madai ya ukosefu wa uwazi na wagombea wenye ushawishi kuondolewa pasipo maelezo ya kutosha.

Wananchi na wanachama waliotilia shaka mchakato huo walidai baadhi ya waliokatwa walikuwa wagombea waliokubalika kijamii na kwamba hatua hizo zilitishia mshikamano ndani ya chama katika baadhi ya maeneo.

Ingawa taarifa ya CCM haikutaja maeneo maalumu yaliyosababisha malalamiko hayo, vyanzo mbalimbali vya habari vimekuwa vikiripoti kuwapo kwa malalamiko ya wana CCM kudai wagombea wanaowataka kuondolewa kwenye mchakato huo, hali iliyoashiria kuwepo kwa makundi na mpasuko ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu.

Kwa maelekezo hayo, chama kimechukua hatua kutatua changamoto hiyo kwa kurudisha mchakato kwa wanachama kupitia kura za maoni, hatua inayoashiria kuimarisha demokrasia ya ndani ya chama.