Finland na Tanzania waimarisha ushirikiano kupitia sekta ya misitu
Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting (kushoto) na Mkurugenzi wa Misitu na Ufugaji wa Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras wakizindua rasmi Mwongozo wa Uwekezaji katika Sekta ya Misitu Tanzania wakati wa hafla ya Siku ya Misitu ya Finland iliyofanyika Jijini Dar es Salaam huku wadau wengine wakishuhudia.
Muktasari:
- Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania kupitia Mpango wa Ubunifu wa Funguo, wameadhimisha Siku ya Misitu ya Finland 2026
Dar es Salaam. Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kibiashara wa nchi hizo mbili akisema ni muhimu katika kufungua fursa hasa za sekta ya misitu.
“Ushirikiano madhubuti wa kibiashara ni muhimu katika kufungua fursa zote za sekta ya misitu Tanzania. Siku ya Misitu ya Finland inatoa fursa ya kipekee kwa kampuni, wabunifu na wawekezaji kutoka nchi zote mbili kujenga uhusiano, kubadilishana ujuzi, na kubaini fursa za kivitendo za ushirikiano,” amesema Balozi Zitting katika maadhimisho ya Siku ya Misitu ya Finland 2026 yenye kaulimbiu:“Kufanya Biashara na Finland.”
Amesema tukio hilo linaashiria dhamira ya muda mrefu ya Finland katika maendeleo endelevu ya kiuchumi ya Tanzania kupitia uwekezaji, ubunifu na ushirikiano na sekta binafsi.
Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania kupitia Mpango wa Ubunifu wa Funguo, wameadhimisha Siku ya Misitu ya Finland jana Ijumaa Juni 5, 2026.
Tukio hilo limewakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, wajasiriamali na wataalamu wa misitu kutoka Finland na Tanzania ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na ukuaji endelevu katika sekta ya misitu.
Maadhimisho hayo yalihusisha mada kuu kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya misitu Tanzania, mawasilisho kutoka kampuni za Finland na jukwaa maalumu la maonyesho ya ufumbuzi endelevu wa misitu kutoka nchi zote mbili.
Akiwakilisha Serikali ya Tanzania, Mkurugenzi wa Misitu na Ufugaji wa Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras ameupongeza mpango huo wa ushirikiano na kusisitiza jinsi unavyoendana na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania.
“Sekta ya misitu ya Tanzania ina fursa nyingi kubwa ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu. Finland imekuwa miongoni mwa wabia wetu thabiti na wenye mchango mkubwa katika kufanikisha hili. Uhusiano wa namna hii wa kibiashara wa moja kwa moja ndio hasa unaohitajika ili kutafsiri malengo yetu ya pamoja kuwa ajira, kuongeza thamani na ukuaji endelevu,’ amesema
Pancras.
Akizungumza kwa niaba ya UNDP Tanzania, Meneja wa Mradi wa Funguo, Joseph Manirakiza ameangazia nafasi ya ushirikiano katika kukuza ubunifu.
“Ubunifu unastawi pale ambapo wajasiriamali wanapata sio tu ufadhili, bali pia mitandao, masoko na ushirikiano. Siku ya Misitu ya Finland ni jukwaa la aina yake ambalo wajasiriamali wetu wa #GreenCatalyst wanalihitaji ili kuunganishwa na kukua,” amesema Manirakiza.
Mwakililishi wa FORLAND ambao ni mradi unaojihusisha na misitu, matumizi sahihi ya ardhi na kuongeza thamani katika mazao ya misitu, Masasa Makwassa ameipongeza Finland kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu na kusisitiza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha malengo ya mradi huo yanayotekelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Finland yanafikiwa.