Kakama yafungua pazia mjadala matumizi ya akili unde kwenye Kiswahili
Muktasari:
- Kongamano la kimataifa la Kiswahili linafanyika kwa siku mbili nchini Burundi likifuatiwa na maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.
Burundi. Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili Jumuiya ya Afrika Mashariki (Kakama), Dk Caroline Asiimwe amesema kongamano la tatu la kimataifa limefungua rasmi hatua za kuanza kutumia akili unde kuleta maendeleo ya Kiswahili Afrika Mshariki na duniani.
Ameyasema hayo leo kwenye ufunguzi wa kongamano hilo lililoanza leo Jumapili Julai 5, 2026, Bujumbura nchini Burundi.
Aidha ametoa wito kwa vyombo vya habari vinavyotoa maudhui kwa Kiswahili kuanzisha sera ya kuwa na vipindi vinavyohimiza ukuzaji wa lugha ya Kiswahili katika nchi wanachama.
Amesema Kakama imekuwa mstari wa mbele kuonyesha fursa za Kiswahili ili kufikia, huku akihimiza juhudi za pamoja ili kuwekeza kwenye lugha ya Kiswahili kwani bila kufanya, hivyo hakuna mgeni kutoka nje ya nchi atakuja kuwekeza.
Dk Asiimwe amesema Kakama inaangalia uwezekano wa kushirikiana na wadau wa Kiswahili kuanzisha kozi kuwasaidia wanahabari ambao hawana ujuzi wa lugha ya Kiswahili.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano mgeni rasmi Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi, Lydia Nsekera
ametoa wito kwa wanajumuiya wa Afrika Mashariki kuipa hadhi lugha yao ya Kiswahili kutokana na kuwa chombo muhimu kinachowaunganisha.
Amesema awali jamii iliyokuwa ikitumia Kiswahili walionekana ni wahuni lakini hali imebadilika kwa sasa wale wanaokimbilia kujifunza wanaonekana ni wasomi.