Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makada wa CCM Mbeya, Moro waandamana kupinga uteuzi wa madiwani

Muktasari:

  • Leo Agosti 17, baadhi ya makada na wanachama wa CCM katika Kata ya Mbalizi Road jijini Mbeya wameandamana kupinga uteuzi wa mgombea, aliyepitishwa na chama hicho wakidai kutomkubali.

Mbeya/Moro. Wakati baadhi ya wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mbalizi Road jijini Mbeya wakiandamana kupinga uteuzi wa mgombea udiwani, wenzao wa Ulanga mkoani Morogoro wametishia kurejesha kadi wakipinga diwani aliyeongoza kwenye kura za maoni kukatwa.

Leo Agosti 17, baadhi ya makada na wanachama wa CCM katika Kata ya Mbalizi Road jijini Mbeya wameandamana kupinga uteuzi wa mgombea, aliyepitishwa na chama hicho wakidai kutomkubali.

Hata hivyo, CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, imefafanua kuwa, haiteui majina kutokana na utashi wa mtu, badala yake mgombea mwenye malalamiko, anapewa nafasi ya kuwasilisha kwa maandishi kisha vikao vitaamua.

Baadhi ya wanachama wa CCM Kata ya Minepa waliofika Ofisi ya CCM Mkoa wa Morogoro kuomba ufafanuzi wa jina la mgombea wao kukatwa. Picha na Jackson John

Stanley Mapunda amesema yapo baadhi ya mambo yamefanyika bila haki.

“Mimi ni mwenyekiti wa UVCCM katika kata hii, tunashangaa kwa nini chama kinamng’ang’ania huyu mtu, tunahitaji mtu mwenye kugusa maisha ya watu,” amesema.

Kwa upande wake, Noah Mwakafwila amesema maandamano ya amani waliyoyafanya ni kupinga uteuzi wa mgombea huyo.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya mjini, Mohamed Mavallah amesema chama hicho hakiteui kwa utashi wa mtu, bali kanuni inampa nafasi mgombea kuwasilisha malalamiko kwa maandishi kisha vikao vinaamua.

Amesema malalamiko aliyopokea ni kutoka kwa wananchi ambao kimsingi hawakuhusika na kura za maoni, ambazo ziliwashirikisha wajumbe wa chama na si wananchi, amefafanua kuwa hata hivyo anayelalamika alipata kura nane.

“Kwanza waliokuja ofisini kwangu walikuwa wananchi na si mgombea, nilipohoji miongoni mwao wakasema si wajumbe, nikauliza wamejuaje kwa kuwa kura zilihusu wajumbe, wakadai kura hazikuwa huru na haki.

“Mwisho, nikawaambia waende mkoani, ikaonekana haina uzito kwa kuwa aliyekuwa analalamika alipata kura nane, si wa pili wala wa tatu, kwa hiyo nafasi ya wananchi haijafikiwa, suala ni kushauri,” amesema Mavallah.

Kwingineko katika Kata ya Minepa iliyopo Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, wanachama zaidi ya 50 wametishia kurudisha kadi za uanachama kwa madai kuwa mtia nia aliyeongoza kura za maoni, Malugu Manosu kutopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Morogoro.

Wanachama hao wamefunga safari kutoka Minepa hadi Ofisi za CCM mkoani humo kwa lengo kupata ufafanuzi kutoka ngazi ya mkoa baada ya kutoridhishwa na uamuzi huo uliompa nafasi mshindi wa pili kwenye kura za maoni.

Hussein Ndalama amesema licha ya mchakato wa kura za maoni kufanyika kwa amani, wameshtushwa na taarifa za mtiania aliyeongoza kinyang’anyiro hicho, jina lake halijarudi badala yake limekuja la aliyeshika nafasi ya pili.

“Mgombea wetu aliyeshinda kura za maoni jina lake limekatwa baada ya kupata taarifa hizo, tumefuatilia ngazi ya wilaya, hatujapata majibu, tukaamua kuja mkoani kupata majibu sahihi,” amesema Ndalama.

Naye Hamisi Mustafa amesema maombi yao ni kurejeshwa jina la aliyeongoza kura za maoni ili kupeperusha bendera ya chama kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.

“Tunaomba jina la Malugu lirudishwe tumpambanie kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, ndiyo maana wanachama wengine wametukabidhi kadi endapo jina halitatangazwa tuzirudishe sisi tuondoke zetu,” amesema.

Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Nuru Ngereja amekiri kupokea malalamiko ya wanachama hao akisema tayari yamefikishwa ngazi ya Taifa kwa ajili ya uamuzi wa mwisho ili haki itendeke.

“Jambo lao linashughulikiwa na makao makuu kama rufaa yao ili tumpate atakayepeperusha bendera ya CCM Kata ya Minepa, kinachotakiwa kwao kwa sasa ni kuwa watulivu kwasababu chama kinaongozwa kwa utaratibu na si mihemko wala si kwa mashinikizo kama wanavyotaka wao,” amesema Ngereja.

Ameongeza kuwa kuongoza kura za maoni si kigezo pekee cha kumfanya mgombea kupitishwa na kuteuliwa na chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu, bali vikao vinakaa na kujiridhisha na ushindi wake.