Tanzania yafungua milango mipya ya biashara Russia
Muktasari:
- Tanzania imepata fursa mpya za kupanua soko la bidhaa zake nchini Urusi kupitia ushiriki wa St. Petersburg International Economic Forum (SPIEF) 2026, ambapo tayari mahitaji ya bidhaa kama kahawa mbichi, matunda na mazao mengine yameanza kuwasilishwa na wadau wa soko hilo.
Dar es Salaam. Tanzania imefungua ukurasa mpya wa fursa za biashara katika soko la Urusi baada ya kuanza kupokea mahitaji ya bidhaa mbalimbali za chakula, hatua inayotajwa kuongeza kasi ya mauzo ya nje na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dk Latifa Khamis amesema Tanzania inaendelea kutumia majukwaa ya kimataifa, ikiwemo St. Petersburg International Economic Forum (SPIEF) 2026, kutangaza bidhaa na huduma zake chini ya kampeni ya Made in Tanzania.
Amesema ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo umefungua milango mipya ya biashara, ambapo tayari wadau wa Urusi wameanza kuonesha uhitaji wa bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania zikiwemo kahawa mbichi (green coffee), parachichi, embe, papai na matunda ya passion.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dk Latifa Khamis, akizungumza kuhusu fursa za soko la Urusi kwa bidhaa za Tanzania.
Dk Latifa amesema fursa hizo ni matokeo ya diplomasia ya uchumi inayoendelea kuimarishwa, huku Tanzania ikitazamia kuongeza ushindani wa bidhaa zake katika masoko ya kimataifa kupitia mazao ya kilimo na bidhaa nyingine zenye ubora.
Ameongeza kuwa kuimarika kwa usafiri wa anga kati ya Tanzania na Urusi, pamoja na mipango ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuanza safari za moja kwa moja Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow mwezi Julai 2026, kutarahisisha zaidi biashara, utalii na uwekezaji kati ya pande hizo mbili.
Katika hatua nyingine, TanTrade imesema Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) mwaka huu yatakuwa ya kipekee kutokana na maadhimisho ya miaka 50, huku zaidi ya makampuni 3,000 ya ndani na nje yakitarajiwa kushiriki.
Dk Latifa amesema kampeni ya Made in Tanzania inaendelea kupata nguvu kimataifa, akisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara wa ndani kutumia fursa za masoko mapya yanayojitokeza, ikiwemo Urusi na mataifa mengine.
Maonesho hayo yatakwenda sambamba na matukio mbalimbali ya burudani na kijamii, yakiwemo Fashion Night na usiku wa Golden Jubilee utakaotoa tuzo kwa wadau waliotoa mchango mkubwa katika miaka 50 ya Sabasaba.