Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umeme wa kilovoti 400 Chalinze–Dodoma kukamilika Agosti

Muktasari:

  • Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema mradi huo utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa matumizi ya nyumbani, biashara na viwanda, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi.

Morogoro. Watanzania kote nchini wanatarajiwa kunufaika na umeme wa uhakika zaidi kufuatia maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambayo imefikia asilimia 89 ya utekelezaji.

Mradi huo wenye urefu wa kilometa 345 unatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026 na unalenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa umeme kutoka vyanzo vikubwa vya uzalishaji kwenda maeneo yenye mahitaji makubwa nchini, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akikagua maendeleo ya mradi huo Julai 1, 2026, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema mradi huo ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika kwa matumizi ya majumbani, biashara na viwanda.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha Gridi ya Taifa na kuwezesha umeme unaozalishwa katika Julius Nyerere Hydropower Station chenye uwezo wa megawati 2,115 kufika kwa ufanisi zaidi kwenye maeneo mbalimbali ya matumizi.

“Umeme wa uhakika una maana ya maisha bora kwa wananchi, biashara kukua, viwanda kufanya kazi bila kukatika kwa huduma na huduma za kijamii kama hospitali na shule kuimarika,” amesema Ndejembi.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya nishati ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata umeme unaowawezesha kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Razalo Twange, amesema ongezeko la uwekezaji katika miundombinu ya umeme limeongeza kasi ya uunganishaji wa wateja wapya nchini.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Tanesco imefanikiwa kuunganisha zaidi ya wateja laki nane, hatua anayoisema ni rekodi mpya ambayo haijawahi kufikiwa tangu uhuru.

“Kila mteja mpya anayepata umeme ni fursa mpya ya biashara, elimu bora kwa watoto na huduma bora za afya. Huu ndio msingi wa maendeleo tunayoyalenga,” amesema Twange.

Awali, Meneja wa Mradi, Mhandisi Newton Mwakifamba, amesema kazi zinaendelea kwa kasi na zinatarajiwa kukamilika kwa mujibu wa ratiba, hatua itakayofungua ukurasa mpya wa upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.