Watafiti wataka taasisi ya wakimbizi EAC
Profesa Opportuna Kweka wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kutoka Idara ya Jiografia, Ndaki ya Sayansi za Jamii na Mwenyekiti wa Kigoda cha Utafiti kuhusu Watu Wanaolazimika Kuhama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (UDSM Research Chair on Forced Displacement - UDSM-RCFD), akizungumza nje ya Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Arusha, jana Jumatatu Juni 22, 2026.
Muktasari:
- Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamependekeza kuundwa kwa taasisi maalumu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) itakayoratibu masuala ya wakimbizi na watu wanaolazimika kuhama makazi yao pamoja na nchi wanachama kuharakisha kupitisha sera ya pamoja ili kuondoa tofauti za usimamizi wa wakimbizi na kuimarisha ujumuishaji, elimu, ajira na upatikanaji wa huduma muhimu katika ukanda huo.
Arusha. Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamependekeza kuanzishwa kwa taasisi maalumu ya kikanda itakayoshughulikia kwa karibu masuala ya wakimbizi na watu wanaolazimika kuhama makazi yao katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wamesema nchi hizo pia zinapaswa kuharakisha utekelezaji wa sera za pamoja za wakimbizi na watu wanaolazimika kuhama makazi yao,wakisema tofauti za sera zilizopo zinachangia changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa huduma muhimu kwa wakimbizi katika ukanda huo.
Hayo yamesemwa jana Jumatatu Juni 22, 2026 na Profesa Opportuna Kweka,kutoka Idara ya Jiografia Ndaki ya Sayansi za Jamii UDSM na Mwenyekiti wa Kigoda cha masuala yanayohusika na watu wanaolazimika kuhama katika Kanda ya EAC (UDSM Research Chair on Forced Displacement (UDSM-RCFD).
Profesa huyo ameyasema hayo baada ya kukutana na Kamati ya masuala ya kikanda na usuluhishi wa migogoro ya EAC na kuwasilisha matokeo ya tafiti wanazoendelea nazo.
Amesema taasisi hiyo maalum itasaidia kusimamia kwa pamoja masuala ya elimu, vijana, watoto, mazingira, upatikanaji wa chakula, ajira na ujumuishaji wa wakimbizi katika jamii.
Amesema mapendekezo hayo yametokana na tafiti zilizofanyika kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka jana na unaendelea kufanyika katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kuhusu hali ya wakimbizi wanaoishi kambini, vijijini na mijini pamoja na watu wanaolazimika kuhama kutokana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na sababu za maendeleo.
Amesema tafiti hiyo imeaangazia wakimbizi wa kisiasa,wakimbizi walioshindwa kukimbia wakabaki ndani ya nchi zao na wanaolazimika kuhama kutokana na mabadiliko ya tabia nchi,umaskini, uliofanyika katika kambi za wakimbizi,vijiji,mijini,misaada wanayopewa na shughuli za kiuchumi.
“Kuna haja ya kuwa na mfumo wa pamoja wa kikanda unaoshughulikia masuala haya kwa sababu changamoto zinazowakabili wakimbizi zinafanana katika nchi nyingi za Afrika Mashariki,” amesema
“Tunaamini taasisi hiyo maalum itaangalia masuala ya elimu,vijana,watoto,kuchangamana,upatikanaji wa chakula,mazingira na tulipojadili sana tuliona tunaweza kuongea bila neno ukimbizi kwamba haikupaswa kuwa na mkimbizi ndani ya EAC,”ameongeza
Amesema tafiti hizo zimeonyesha kuwa licha ya EAC kuwa na sera zinazohamasisha ujumuishaji wa wakimbizi, bado kuna tofauti kubwa katika utekelezaji wake kati ya nchi wanachama.
Kwa mujibu wake baadhi ya nchi bado zinawazuia wakimbizi kuishi nje ya makambi au kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, hali inayokinzana na azma ya ujumuishaji inayosisitizwa na sera za kikanda.
“Tumebaini kuwa kuna tofauti kubwa za utekelezaji wa sera kati ya nchi za EAC,ambzo inazo sera ambazo zinazokazia masuala ya kuchangamana na pamoja na nchi kuwa na sera ambazo zinafanana.
“Ila tumeona bado kuna nchi ambazo zina changamoto hizo sera zake bado zinapingana kwa mfano sera ya EAC ambayo inasema kuwe na integration tunaona kwamba kuna nchi ambazo bado zina wakimbizi ambao wanatoka ndani ya nchi hizo, na wanakaa kwenye kambi hawaruhusiwi kujitafutia,”
Amesema wamebaini kuwa kupungua kwa misaada ya kimataifa kwa wakimbizi huku idadi yao ikiongezeka kunahitaji nchi za hizo za EAC kuanza kutafuta suluhisho za ndani zitakazowasaidia wakimbizi kujitegemea badala ya kutegemea misaada kwa muda mrefu.
“Tunahitaji kuangalia namna ambavyo tunaweza kutatua changamoto hizi kwa kutumia rasilimali na sera zetu wenyewe bila kusubiri misaada kutoka nje,” amesema.
Katika utafiti huo, watafiti walichunguza pia upatikanaji wa elimu kwa wakimbizi na kubaini kuwa ubora wa elimu katika baadhi ya makambi bado ni changamoto, jambo linalowafanya vijana wengi kushindwa kupata fursa za kuendelea na masomo ya juu au kupata ajira bora.
Amesema elimu bora kwa wakimbizi ni muhimu kwa maendeleo ya ukanda huo, kwa kuwa wengi wao ni sehemu ya jamii za eneo hilo na wanaweza kuchangia maendeleo ya nchi zao wanaporejea au wanapojumuishwa katika jamii wanazoishi.
Mratibu wa masuala ya utafiti katika Kigoda hicho, Benezet Rwelengera, amesema tafiti hizo zilifanyika katika kambi ya Nyarugusu na Nduta nchini Tanzania, Kakuma nchini Kenya pamoja na maeneo mbalimbali nchini Uganda.
Amesema utafiti umeonyesha kuwa wakimbizi wanaoishi mijini hukabiliwa na changamoto tofauti na wale waliopo kambini, ikiwemo kulazimika kuficha utambulisho wao kwa hofu ya kukumbana na vikwazo vya kisheria au kijamii.
Rwelengera aesema wakimbizi wengi wana mchango mkubwa katika shughuli za kijamii na kiuchumi lakini mchango huo haujatambuliwa kikamilifu katika mifumo rasmi.
“Tunapendekeza mifumo ya usimamizi wa wakimbizi isijikite tu katika ulinzi, bali pia iangalie namna ya kuwawezesha kuwa sehemu ya uchumi na maendeleo ya jamii wanazoishi,” amesema