Dk Mwinyi aonya wateule wake kugombana

Rais Mwinyi akizungumza baada ya kuwaapisha wakuu wa Mikoa na Wilaya Ikulu Zanzibar leo Novemba 20, 2023.

Muktasari:

  • Rais Mwinyi amesema licha ya ubinadamu, kutokuwepo kwa uhusiano mzuri kwa viongozi hao kunasababisha kazi zikwame.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussen Mwinyi ameeleza kuchukizwa na viongozi anaowateua kugombana wenyewe kwa wenyewe na kusababisha kazi zikwame akisema pale ambapo itabidi atachukua hatua.

“Kila siku ya Mungu Waziri kagombana na Katibu mkuu wake, Waziri kagombana na wakurugenzi wake, katibu mkuu kagombana na wakurugenzi, mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya hawaelewani, mkuu wa wilaya na katibu tawala hawaelewani, hii kazi itafanyikaje,” amehoji Dk Mwinyi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Novemba 20, 2023 wakati akiwaapisha wakuu wa Mikoa na Wilaya aliowateua hivi karibuni Ikulu Zanzibar na na kuzungumzia mambo matano huku akionya ugonvi unaoendelea baiana ya watu hao.

Waliopaishwa leo ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Rashid Hadid Rashid ambao wamebadilishana na wa kusini Unguja.

Wengine ni mkuu wa wilaya ya Kati Sadifa Juma Khamis, Mkuu wa wilaya ya Kaskazini Unguja, Othman Maulid na Mkuu wa wilaya ya Kusini Unguja, Galos Nyimbo.

Rais Mwinyi amesema iwapo wakiendelea hivyo wanaharibu kazi.

“Mko pale kufanya kazi lazima mfanye kazi kwa pamoja, wale ni wateule wangu mimi, sio wenu nyie, ninapomteua mtu wala siulizi kwa sababu sio uteuzi wako,” ameeleza.

Rais Mwinyi pia amezungumzia migogoro ya wabunge na wawakilishi kutoelewana na wakurugenzi, wakuu wa wilaya na watendaji wengi

“Kwa hiyo ningependa hili niliseme kwa Serikali nzima kuanzia sasa watu ambao hawawezi kufanya kazi kwa pamoja maanayake hawafai.”

Kuhusu wakuu wa mikoa na wilaya, amesema kazi ya kwanza ya viongozi hao ni kuhakikisha ulinzi na usalama vinaimarishwa na kwamba kumeibuka uhalifu katika Mikoa ya Kusini Unguja na Kaskazini Unguja.

“Hivi karibuni kumeibuka hali ya uvunjifu wa usalama husuani maeneo ambayo utalii unakua kwa kasi.

“Nungwi na Paje kunatokea taarifa za kiusalama ikionyesha taarifa za kiuhalifu ili hali kuna wakuu wa mikoa na wilaya, matukio yake yanaongezeka hakikisheni hali ya ulinzi inongezeka,” amesema.

Amesema aliamini yanapotokea matukio kama hayo kuna operesheni maalumu zinazofanywa lakini anashangaa hakuna jambo lolote linaloendelea.

Amewasisitiza kushughulikia sula hilo kwa nguvu zao zote akisema inasikitisha kuona matukio hayo yanatokea bila hatua zinazochukuliwa.

Pia Dk Mwinyi amesema kuna kero nyingi zinazowakabili wananchi lakini baadhi ya viongozi hawashughuliki nazo badala yake kero hizo zinawafuata hadi Ikulu.

“Sio kusiki kila siku mwananchi anatoka wilayani, mkoani anakwenda Ikulu kupeleka kero zake ilhali kuna wahusika katika ameeno hayo.

Amesema kero nyingi zinatokana na ardhi ambazo zimekuwa tatizo kubwa huku baadhi ya viongozi wakihusika na kuchangia migogoro hiyo.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya watende haki maana ndio wajibu wao wa kwanza na wasiwe sehemu ya kuvunja haki hizo.

Jambo lingine alilotaja Kuhusu kero wanazokutana nazo watalii, Dk Mwinyi amewataka viongozi hao kuzishughulikia haraka kwa kuwa theluthi moja ya pato la Zanzibar linatokana na sekta hiyo.

“Hakikisheni mnashughulikia kero za wawekezaji kuna watu wanaondoa haki za wawekezaji, hakikisheni mnazimaliza, nyie muwe seehemu ya utatui wa changamoto zao,

Amewataka pia viongozi hao kusimamia halmashauri zao kwani sehemu kubwa kazi hazifanyiki kikamilifu kwenye halmashauri akitaja masuala ya ujasiriamali na mazingira kero zake hazitatuliwi.

“Pale unaposikia mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa hashughuliki na halmashauri ndio haya unasikia yanatokea, sisi huku juu tumekuwa wa kushughulikia kero hizo.

Wakizungumza baada ya kuapishwa, baadhi ya viongozi wamesema watahakikisha wanatekeleza maagizo ya Rais kuleta mabadiliko anayoyataka

“Tunaenda kutekeleza maagizo hayo kuondoa kero alizosema mheshimiwa Rais,” amesema Ayoub.