Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madereva Kusini Unguja waipa kongole ZRA

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Yusuph Juma Mwenda.

Muktasari:

  • Baada ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kuzindua huduma za kutoa leseni za udereva na stika za magari ya biashara Mkoa wa Kusini Unguja, wadau wa sekta hiyo wamepongeza hatua hiyo, wakieleza jinsi walivyokuwa wakipata usumbufu kufuata huduma hiyo makao makuu ya mamlaka hiyo.

, Mwananchi [email protected]

Unguja. Baada ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kuzindua huduma za kutoa leseni za udereva na stika za magari ya biashara Mkoa wa Kusini Unguja, wadau wa sekta hiyo wamepongeza hatua hiyo, wakieleza jinsi walivyokuwa wakipata usumbufu kufuata huduma hiyo makao makuu ya mamlaka hiyo.

Said Abdalla Juma, dereva wa magari ya biashara, amesema walikuwa wakipata changamoto kubwa wakilazimika kusafiri zaidi ya kilomita 60 kufuata huduma hizo.

“Wakati mwingine unatoka hapa kwenda mjini, ukifika unaambiwa muda wa kazi umeshamalizika, inabidi urudi ili upange safari nyingine ya kufuata huduma hiyo, kwa hiyo ilikuwa inaumiza sana,” amesema.

Dereva mwingine, Ibrahim Abdalah alisema hatua hiyo itawasaidia kupunguza masafa ya kufuata huduma hiyo mjini, huku akiiomba mamlaka hiyo kuendelea kuwasogezea huduma nyingine.

Kauli ya ZRA
Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Yusuph Juma Mwenda amesema hatua hiyo inalenga kuwasogezea huduma wateja wao karibu na kuwapunguzia gharama kufuata huduma hiyo mjini.

Amesema hivi sasa madereva wanapotaka leseni za vyombo vyao na wale wanaotaka kuongeza muda, sasa wanapata huduma hiyo kwa urahisi.

Pia, amesema kazi ya ZRA sio kukusanya kodi pekee, bali pia kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo alipongeza kiongozi wa mkoa huo kuja na ubunifu ambao umewasaidia wateja wao.

“Hatua hii ni nzuri, kwani jambo hili mbali na kuwapunguzia gharama za kufuata huduma ya leseni mjini, pia linathibitisha kwamba Serikali ipo karibu na wananchi wake,” amesema Mwenda.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa kodi za ndani, Ali Adnan alisema katika vipindi vyote vya fedha mkoa huo umekuwa ukifanya vizuri ukilinganisha na mikoa mengine, hivyo aliwasisitiza kuendeleza hilo.

Nao wafanyakazi wa ofisi hiyo walisema zipo baadhi ya changamoto ambazo zinaisababisha Serikali kukosa mapato, ikiwemo uwepo wa watu wanaowakodisha nyumba wageni kiholela.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Salum Mahita ameomba suala hilo lifanyiwe kazi ili kuisaidia Serikali kuingiza mapato sahihi.