Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwinyi awaapisha RC, maDC wakiahidi kushughulikia kero za wananchi

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (kushoto) akimwapisha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Khamis Mussa Ikulu Zanzibar

Muktasari:

  • Julai Mosi Rais Mwinyi aliwaweka pembeni, Mkuu wa Mkoa na wakuu wa Wilaya ambao walichukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge na uwakilishi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewaapisha wakuu wa wilaya watano na Mkuu wa Mkoa aliowateua hivi karibuni huku wakiahidi kushughulikia changamoto zinazowakumba wananchi na kuhakikisha amani inadumishwa wakati wa uchaguzi mkuu.

Walioapishwa ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis na wakuu wa wilaya watano ambao aliwateua hivi karibuni na kuwaweka pembeni waliokuwa wameshikilia nafasi hizo baada ya kuchukua fomu za kuwania kugombea nafasi za ubunge na uwakilishi kisiwani hapa.

Akizungumza baada ya kuapishwa leo Julai 3, 2025 Ikulu Zanzibar,  Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Hamida Mussa Khamis amesema licha ya uzoefu alio nao katika Serikali, lakini anaona anadhima kubwa kuhakikisha anaondoa changamoto za wananchi na kusimamia amani.

"Kikubwa naomba kwanza ushirikiano, najua kazi hii ni kubwa na ni nzito, lakini nitahakikisha natumia uzoefu nilionao na kushirikiana na wenzagu kutekeleza kazi hii ili kufikia malengo ya mheshimiwa Rais," amesema.

Amesema pamoja na mambo mengine ana wajibu mkubwa kuimarisha amani hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Wengine walioapishwa ni Cassian Gallos Nyimbo mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Rajab Ali Rajab Mkuu wa Wilaya ya Kati, Miza Hassan Faki Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Pemba, Mohammed Ali Abdallah Mkuu wa wilaya ya Mjini na Amour Yussuf Mmanga Mkuu wa wilaya ya Magharibi B.

Mkuu wa Wilaya ya Kati, Rajab Ali Rajab ameahidi kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na weledi ili kufikia malengo ya kuleta maendeleo.

Amewaomba wananchi wa wilaya hiyo kumpa ushirikiano kwani ndio silaha ya mafanikio ambayo yatakayosababisha wilaya na mkoa kwa ujumla kuendelea kupiga hatua za kimaendeleo.

Miza Hassan Faki ni Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Pemba, amesema mikakati ambayo anakwenda kuitekeleza katika wilaya yake ni kuhakikisha wilaya hiyo inaendelea kudumu katika amani na utulivu aliourithi na kuhakikisha wanashirikiana na Baraza la Mji Mkoani kuona mji unakuwa msafi na kusimamia shughuli za maendeleo ndani ya mkoa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Mohammed Ali Abdallah amesema ataendelea kusimamia suala la amani, utulivu na mshikamano kwa wananchi wa wilaya hiyo na kulisimamia Baraza la Manispaa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

“Tutahakikisha Manispaa wanafanya majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ili kuleta haiba nzuri za mji wetu na kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanapangwa kwa utaratibu mzuri ili kufikia maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kuweka mji safi na hakuna wafanyabiashara wanaozagaa,” amesema

Jambo lingine, amesema anatamani kuona wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi wanaondokana na vitendo vya wizi, unyang'anyi na matumizi ya dawa za kulevya kwani hiyo ni changamoto kubwa iliyopo katika maeneo yao.

Hafla ya kuwaapisha viongozi hao imefanyika Ikulu Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Talib Mwinyi Talib, wakuu wa vikosi vya ulinzi na Usalama na viongozi wengine wa chama na serikali.