Bulaya mikononi mwa majaji leo

Muktasari:

Wapigakura hao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic Malagila wanawakilishwa na Wakili Constantine Mutalemwa.

Mwanza. Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Salim Mbarouk, Augustine Mwarija na Shaaban Lila leo linaanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na wapigakura wanne wa Bunda Mjini kupinga matokeo ya uchaguzi dhidi ya mbunge wa jimbo hilo, Ester Bulaya.

Wapigakura hao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic Malagila wanawakilishwa na Wakili Constantine Mutalemwa.

Katika maombi ya msingi waliyofungua Mahakama Kuu, wapigakura hao wanaiomba mahakama itengue ushindi wa Bulaya dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen Wasira kwa madai kuwa uchaguzi huo wa Oktoba 25, 2015 haukuwa huru na haki.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe alisema juzi kuwa jopo hilo la majaji litasikiliza rufaa hiyo mfululizo kuanzia leo.

 Novemba 17 mwaka jana, Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu alimtangaza Bulaya kuwa mshindi halali wa uchaguzi huo baada ya kutupilia mbali maombi ya wapigakura hao.