28 wakiwamo wafanyabiashara mbaroni kwa tuhuma za mauaji Njombe

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Renata Mzinga

Muktasari:

  • Polisi mkoani Njombe nchini Tanzania wanawashikilia watu 28 wakituhumiwa kwa mauaji ya watoto mkoani humo wakiwamo wafanyabiashara, waganga wa jadi na wananchi wa kawaida

Njombe. Baadhi ya  wafanyabiashara wa miji ya Njombe na Makambako mkoani Njombe ni miongoni mwa watu 28 wanaoshikiliwa na polisi wakituhusishwa na na mwendelezo wa matukio ya utekaji na mauaji ya watoto yanayoendelea wilayani Njombe.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Renata Mzinga amesema leo Jumatatu Februari 04, 2019 ofisini kwake wakati akitoa taarifa ya msako wa kubaini mtandao wa watu wanaojihusisha na matukio hayo.

Amesema pia waganga sita wanaodaiwa kujihusisha na matukio hayo wametiwa mbaroni na wanaendelea na mahojiano dhidi yao.

HABARI ZAIDI:

"Tunaendelea na msako mkali kwa kushirikiana na kikosi maalumu kutoka makao na hadi leo hii tunawashikilia watu 28 wakiwamo waganga wa jadi sita, wafanyabiashara na watu wengine wa kawaida," amesema.

Amesema matukio yote yaliyojitokeza ya mauaji, wamekamatwa watu kuhusiana na uhusika wao na vyombo vya dola vinaendelea na upelelezi wa kuwabaini wahalifu.

Kamanda huyo amesema wana taarifa za watuhumiwa waliokimbia wakiwamo waganga wa jadi lakini wameshajua walikokimbilia na vyombo vya dola vitawasaka popote hadi watiwe nguvuni.

“Tunaendelea kuwasihi wananchi wa Njombe waendelee kutoa ushirikiano wa kuwabaini wahusika wa mauaji ya watoto wadogo wasio na hatia,” amesema.