Magufuli amtuma Lowassa afikishe salamu kwa wenzake la sivyo wataishia gerezani

Muktasari:

Waziri huyo mkuu wa zamani alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa wakati Rais akizindua maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo.

 


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemwambia waziri mkuu wa zamani, Edward Lowasa awaambie viongozi wengine wa upinzani watulie “la sivyo wataishia gerezani”.

Rais alisema hayo baada ya kumsifu Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, kuwa ni mwanasiasa mstaarabu ambaye alionyesha utulivu hata baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

Alisema hayo katika uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo Jumanne (Novemba 27) uliohudhuriwa na Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

"Ninakupongeza sana (Lowassa). Hii ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka. Vyama vyetu visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo," amesema Magufuli.

"Nimezungumza hili kwa heshima kubwa ili ukawashauri wale unaowaongoza watulie vinginevyo wataishia kwenye magereza."

Hadi sasa, viongozi kadhaa wa upinzani, hasa Chadema wana kesi za aina tofauti katika mahakama mbalimbali nchini; baadhi wakishtakiwa kwa uchochezi, wengine kwa kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais na wengine kwa kufanya mikusanyiko bila ya kibali.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifutiwa dhamana pamoja na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria.

Lakini Lowassa, ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu kujivua uanachama wa CCM na kujiunga na upinzani, hajawahi kukumbwa na matatizo dhidi ya mamlaka, zaidi ya kuitwa kituo cha polisi kutoa maelezo.

Lowassa alihamia upinzani mwaka 2015 akipinga kitendo cha Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake na la wagombea wengine wa urais na kujiunga na Chadema, ambayo ilimpa fursa ya kutimiza ndoto yake ya kugombea urais.

Katika harakati zake, Lowassa aliungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioundwa na Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi na kushika nafasi ya pili, akiwa ameweka rekodi ya upinzani kupata kura nyingi. Alipata kura milioni 6.7, akiwa nyuma kidogo ya Rais Magufuli, aliyepata kura milioni 8.8.

Akizindua maktaba hiyo ya kisasa yenye uwezo wakuchukua wanafunzi 2,100 na kutunza vitabu 800,000, Rais Magufuli amesema heshima iliyojengwa na UDSM inatakiwa iendelee kuwepo na wanafunzi wapate yanayostahili kwa wakati.

Amesema maktaba hiyo ni nyumba ya maarifa na ni kitu muhimu kwa maendeleo ya kielimu kwa sababu inatoa utulivu wa mtu kujisomea na kupata maarifa.

Rais Magufuli amesema kuanzia mwakani Watanzania watakuwa wakinufaika na mafunzo ya uhudumu wa maktaba kupitia ufadhili uliotolewa na serikali ya China

"Jukumu letu kama nchi ni kuitumia misaada hii vizuri ili iweze kuleta faida kwa manufaa ya Watanzania. Maktaba hii inatakiwa iwe ukumbusho wa W atanzania na watu wengine kutoka nchi jirani wanaokuja kututembelea," amesema.

"Nitasikitika sana kama siku moja nikija nikakuta maktaba hii imechorwachorwa na makaratasi yaliyopo katika shelf (kabatini) yamechanwachanwa. Badala yake tuitunze na iwe kumbukumbu ya ushirikiano wetu na serikali ya watu wa China."

Mbali na hilo pia Magufuli amesema kama nchi itaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali katika kuleta maendeleo baina ya nchi hizo.

Kuhusu mikopo ya wanafunzi, Rais alisifu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kuitoa kwa wakati na kutaka iendelee.

"Nimeambiwa suala la mikopo ni asilimia 60 tu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza ndiyo wamepata, endeleeni kushughulikia ili wapate mikopo itakayowasaidia kupata elimu," amesema Mgufuli.

Soma zaidi: