Kesi ya Bilionea Msuya ilivyoacha vilio, vicheko

Sunday December 30 2018

Washitakiwa saba wa kesi ya mauwaji ya mfanya

Washitakiwa saba wa kesi ya mauwaji ya mfanya biashara wa Madini ya Tanzanite, Erasto Msuya, wakingia katika Chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi jana kusikiliza uamuzi wa Jaji Salma Maghimbi kama wana kesi ya kujibu au la katika shitaka linalowakabili. Picha na Dionis Nyato. 

By Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Moshi. Adhabu ya kifo waliyopewa washtakiwa watano kwa kosa la kumuua bilionea Erasto Msuya, ndiyo iliyotikisa mwaka 2018 na kuacha kumbukumbu kwa ndugu na jamaa ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Adhabu hiyo iliyotokana na kesi hiyo ya mauaji iliyokuwa ikivuta hisia za watu wengi wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, ilitolewa Julai 23 na Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitegauchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa risasi za bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG), Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Katika eneo la tukio, kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22 huku gari ya marehemu aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola na simu zake mbili zikikutwa eneo hilo la tukio.

Katika hukumu iliyosomwa kuanzia saa 3:40 hadi saa 4:40 asubuhi Jaji Maghimbi aliwahukumu adhabu ya kifo washtakiwa watano na kumuachia huru mmoja.

Waliohukumiwa kunyongwa ni mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa, wa sita Sadik Jabir na wa saba, Ally Majeshi.

Advertisement

Hata hivyo, Jaji Maghimbi alimuachia huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne maarufu kwa jina la Mredii, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani kwa kosa la mauaji.

Akichambua ushahidi dhidi ya washtakiwa hao, Jaji Maghimbi alisema Mahakama imezingatia maelezo ya kukiri kosa na ya ungamo ya washtakiwa wanne na pia ushahidi huru kuunga mkono.

Maelezo ya kukiri kosa ambayo yalipokewa mahakamani na kusomwa, yakieleza mpango mzima wa mauaji hayo na ushiriki wa kila mmoja ni ya Sharifu, Mangu, Karim, Sadick na Majeshi.

Kwa mujibu wa Jaji Maghimbi, maelezo ya Sharifu ambayo yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri, yanaeleza mpango mzima wa mauaji ulivyosukwa na bunduki ya SMG ilivyonunuliwa.

Pia, katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo alieleza namna laini mpya za simu zilivyosajiliwa kwa majina ya Kimasai na namna pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo zilivyonunuliwa.

Kuhusu mshtakiwa wa tatu, Jaji Maghimbi alisema ingawa katika maelezo yake ya kukiri kosa alianza kwa kujitoa na kuwabebesha mzigo washtakiwa wenzake, alishiriki katika nia hiyo ovu.

“Ingawa alianza maelezo hayo ya kukiri kosa kwa kujitoa lakini alijua mpango huo wa mauaji na akaendelea kushiriki katika mipango hiyo ya mauaji hadi mwisho bila kujitoa,” alisema Jaji.

“Kitendo cha kutojitoa katika mpango mzima wa mauaji kinaonyesha nia yake ovu ya kutenda kosa hilo. Hakufanya juhudi zozote za kujitoa katika mipango hiyo miovu ya mauaji,” alisisitiza Jaji.

Jaji Maghimbi alisema maelezo ya mshtakiwa Karim kuwa ndiye aliyemfyatulia risasi nyingi marehemu, hadithi yake inaunganika na yale waliyoeleza Sharifu, Mussa na Mjeshi. Aidha, Jaji alisema maelezo hayo ya kukiri kosa na maungamo ya washtakiwa, yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri na hivyo kuthibitisha shtaka la mauaji pasipo kuacha shaka yoyote.

Akizungumza mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, dada wa marehemu, Antuja Msuya, alimshukuru Jaji Maghimbi kwa kutoa hukumu ya haki na pia wapelelezi wa kesi hiyo.

“Kwa kweli katika jambo hili nimemuona Mungu akitenda haki. Nawashukuru wapelelezi (wa polisi) makini waliopeleleza kesi hii. Zaidi ya yote namshukuru Jaji aliyetoa hukumu hii,” alisema.

“Kama familia nasema ahsante na tumeridhishwa na uamuzi huu,” alisema na baada ya hapo kuanza kububujikwa na machozi huku akibembelezwa na ndugu wengine.

Baba mzazi wa marehemu, Simon Msuya pia aliishukuru Mahakama akisema imetenda haki lakini akasema hakuridhishwa na hatua ya Jaji kumuachia huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne.

Hata hivyo, tayari washtakiwa hao watano waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, wamekata rufani katika Mahakama ya Rufaa Tanzania na sasa wanasubiri kupangwa kwa vikao vya mahakama hiyo.

Kesi hiyo ilichukua takribani miaka mitatu sawa na siku 1,285 kuanzia Februari 10, 2015, siku ambayo usikilizwaji wa awali ulifanyika mbele ya Jaji Amaisario Munisi.

Wakati hukumu hiyo ikitolewa, mke wa marehemu, Miriam Msuya hakuweza kushuhudia kwa kuwa alikuwa mahabusu kwa tuhuma za kumuua kwa makusudi wifi yake, Aneth Msuya.

Advertisement