Albamu ya sita ilivyo mtihani kwa Wizkid

Muktasari:
- Wizkid ambaye ni mshindi wa Grammy 2021 kupitia wimbo wa Beyonce, Brown Skin Girl (2019), anakuja na mradi huo kufuatia albamu yake ya tano, More Love, Less Ego (2022) kushindwa kufanya vizuri kama ambavyo ilitarajiwa.
Nigeria, Mwimbaji wa Afrobeat kutoka Nigeria, Wizkid, 34, amesema kwa kipindi kisichozidi mwezi mmoja albamu yake ya sita aliyoipa jina la ‘Morayo’ itatoka baada ya kuipiga kalenda mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali.
Wizkid ambaye ni mshindi wa Grammy 2021 kupitia wimbo wa Beyonce, Brown Skin Girl (2019), anakuja na mradi huo kufuatia albamu yake ya tano, More Love, Less Ego (2022) kushindwa kufanya vizuri kama ambavyo ilitarajiwa.
Staa huyo alipata umaarufu baada ya kuachia wimbo wake ‘Holla at Your Boy’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Superstar (2011) iliyotoka miaka miwili baada ya kusainiwa na Banky W’s Empire Mates Entertainment (E.M.E).
Tangu ametangaza ujio wa albamu hiyo, Wizkid amekuwa akisongeza mbele tarehe ya kuachiwa kwake kwa sababu mbalimbali ikiwemo kifo cha mama yake mzazi, Jane Dolapo ambaye alifariki Agosti 2023 akiwa na umri wa miaka 66.
Mwanzilishi huyo wa Starboy Entertainment mapema wiki hii amesema kabla ya albamu hiyo kutoka, mashabiki watapata wimbo mmoja kutoka kwake na kudokeza kuwa ifikapo Oktoba 1, 2024 ambayo pia ni siku ya uhuru wa Nigeria kila kitu kitakuwa wazi
Hata hivyo, Wizkid amekuwa katika mtihani kufuatia mafanikio makubwa aliyopata kupitia albamu yake ya nne, Made In Lagos (2020) ambayo yalishindwa kufikiwa na albamu yake iliyofuatia, More Love, Less Ego (2022).
Albamu ya Made In Lagos ilimuwezesha kuwania tuzo za Grammy 2022 katika vipengele viwili ambavyo ni Best Global Music Perfomance kupitia wimbo ‘Essence’ aliomshirikisha Tems, pia kipengele cha Best Global Music Album.
Wimbo ‘Essence’ ulimpa tuzo na rekodi lukuki, ulishinda tuzo mbili za AFRIMA 2021 kama Wimbo Bora wa Mwaka na Wimbo Bora wa Kushirikiana. Ulishinda tuzo tatu za AEAUSA 2021 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana, Video Bora na Wimbo Bora wa Mwaka.
Ulishinda tuzo mbili za NAACP Image Awards 2022 kama Video Bora na Wimbo Bora wa Kimataifa, ulishinda The 3Music Awards 2022 kama Wimbo Bora Afrika, kubwa zaidi ulishinda BET 2022 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.
Vilevile ulishida tuzo mbili za American Music Awards 2022 kama Wimbo Bora wa R&B, huku Wizkid akishinda kama Msanii Bora wa Afrobeats na kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kufikia mafanikio hayo.
Ulifanya vizuri chati kubwa duniani, ulishika namba moja Billboard US Afrobeats Songs, namba tisa Billboard Hot 100, namba 11 US Rolling Stone Top 100, namba 28 Billboard Global 200 na namba moja Billboard US World Digital Song Sales n.k.
Kwa matokeo hayo, Essence uliandika rekodi kama wimbo wa kwanza nchini Nigeria kuingia chati za Billboard Hot 100 na Billboard Global 200 kwa wakati mmoja.
Huu ndiyo mtihani unaomkabili Wizkid, kila albamu atakayotoa mashabiki wanailinganisha na Made In Lagos (2020) wakitazamia kupata wimbo mkali kama Essence kitu ambacho albamu yake, More Love, Less Ego (2022) ilishindwa. Je, hii mpya itaweza?.