Harmonize kufanya tamasha la wamachinga Dar

Muktasari:
- Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Rajab Abdul maarufu kama Hamornize amesema atafanya tamasha la muziki ambalo litakuwa maalum kwa ajili ya wamachinga wote wa jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Rajab Abdul maarufu kama Hamornize amesema atafanya tamasha la muziki ambalo litakuwa maalum kwa ajili ya wamachinga wote wa jijini Dar es Salaam.
Harmonize ameyasema hayo leo Jumamosi Februari 26, 2022 wakati wa ufanyaji usafi katika soko la Kariakoo lililoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.
Amesema tamasha hilo litafanyika katika jiji humo na pindi taratibu mbalimbali zitakapokamilika ataweka wazi litafanyika tarehe ngapi na katika eneo gani.
"Mimi na msanii mwenzangu Alikiba tumejipanga na tumefikiria kufanya tamasha kwa ajili ya wamachinga, tutaanza kufanya usafi kisha tukimaliza tutafanya tamasha kubwa ambalo litaweka historia kwa wamachinga wenzangu," amesema Harmonize
Harmonize amesema kabla ya kufanikiwa katika muziki alishawahi kuwa mmachinga katika soko la Kariakoo hivyo anatambua shida mbalimbali zinazozikabili kundi hilo