Jay Mondy aweka rekodi 'kupostiwa' na YouTube

Muktasari:

  • Hii ni baada ya kupostiwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa YouTube kwa kuwa miongoni mwa madansa waliofanya vizuri kwenye 'chalenji' ya wimbo wa Tyla uitwao Art.

Baada ya kusota akijitafuta kwa miaka mingi katika uchekeshaji, sasa tunaweza kusema mchekeshaji na dansa maarufu nchini Jay Mondy amejipata. 

Hii ni baada ya kupostiwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa YouTube kwa kuwa miongoni mwa madansa waliofanya vizuri kwenye 'chalenji' ya wimbo wa Tyla uitwao Art.

Jay anakuwa dansa pekee kutoka Afrika Mashariki kuwahi kupostiwa katika ukurasa huo, ambao YouTube imeamua kuutumia kwa watengeneza maudhui mbalimbali wanaoupiga mwingi, mmojawapo akiwa Jay.

YouTube imetoa orodha hiyo ikiwapongeza watengeneza maudhui kutoka mataifa mbalimbali kufuatia juhudi wanazozifanya pamoja na maudhui yao kufanya vizuri.

Kwa sasa Jay anazunguka mataifa mbalimbali akiwa na mpenzi wake Isabella Afro, ambaye pia ni dansa aliyejulikana zaidi kupitia baadhi ya video za mwanamuziki Diamond Platnumz.

Kwenye mataifa hayo Jay amekuwa akitumia fursa ya kufanya chalenji za kucheza nyimbo ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mtandao wa YouTube.

Kupitia heshima hiyo iliyotolewa na YouTube, baadhi ya mashabiki wameonekana kuvutiwa na kitendo hicho, wengi wao wamempongeza mchekeshaji huyo kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Ikumbukwe kuwa Jay Mondy alianza sanaa akiwa kama mchekeshaji wa kuposti video kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii pamoja na kusimama katika majukwaa ya uchekeshaji, rasmi alianza kujikita katika dansi mwaka 2020.