Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kili Paul mbioni kuupoteza ufalme wa Diamond

Muktasari:

  • Ipo hivi, kufuatia kushika kasi kwa matumizi ya mitandao ya kijamii na kupanuka kwa ugunduzi wa kidijitali duniani, wasanii hasa wa muziki wamenufaika na maendeleo hayo yaliyowarahisishia kusambaza na kuuza kazi zao.

Dar es Salaam, Je, wajua muda siyo mrefu Kili Paul maarufu kama Masai wa TikTok anaenda kuwa Mtanzania mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mitandao ya kijamii akimpiku Diamond Platnumz ambaye ni namba moja kwa sasa?.

Ipo hivi, kufuatia kushika kasi kwa matumizi ya mitandao ya kijamii na kupanuka kwa ugunduzi wa kidijitali duniani, wasanii hasa wa muziki wamenufaika na maendeleo hayo yaliyowarahisishia kusambaza na kuuza kazi zao.


                        

Hata hivyo, hapa katikati kumeibuka kundi la wazalishaji maudhui (content creator) ambalo kwa kutumia majukwaa yale yale, limeweza kupata uungwaji mkono mkubwa na sasa wanaenda kuwapiku wanamuziki.

Kundi hilo ambalo kwa sehemu kubwa hutengeneza maudhui yenye lengo la kuburudisha limeanza kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi katika mitandao ya kijamii kama TikTok, Instagram, Facebook na YouTube.

Mathalani mtu mwenye wafuasi wengi TikTok duniani siyo mwanamuziki, bali mzalisha maudhui kutoka Senegal, Khabane Lame mwenye wafuasi zaidi ya milioni 160, na hata namba mbili na tatu nao wanafanya kazi hiyo.

Ukija Tanzania, mtengeneza maudhui ya michezo, Zero Brainer ndiye anaongoza TikTok akiwa na wafuasi milioni 9.2, anafuatiwa na staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz mwenye milioni 6.7 katika mtandao huo unaomilikiwa na kampuni ya China, ByteDance.

Kili Paul anashika nafasi ya tatu TikTok akiwa na wafuasi milioni 6.3 ambao amewapata kwa umaarufu wake na kunakilisha nyimbo za kihindi na hata kupata mialiko mingi nchini India.
Hata hivyo, huyu ndiye Mtanzania wa pili anayetazamwa zaidi YouTube kwa sasa akiwa na ‘views’ zaidi ya bilioni 2.4 na wafuasi (subscribers) milioni 6.1, huyu ametanguliwa na Diamond pekee mwenye ‘views’ zaidi ya bilioni 2.6 na wafuasi milioni 9.2.

                       

Anayemfuatia Kili Paul kwa watazamaji wengi YouTube ni mzalishaji maudhui pia ambaye ni Jay Mondy akiwa na ‘views’ bilion 1.88, ndipo wanafuatia wanamuziki wawili, Harmonize mwenye bilioni 1.12 na Rayvanny bilioni 1.15.

Hata hivyo, wazalishaji maudhui wana wastani wa kupata namba kubwa kila mwezi kitu ambacho kinaonesha muda siyo mrefu watakuwa juu ya wanamuziki hao na ndicho ameanza kukifanya Kili Paul.

Mfano kwa Agosti 2024, Jay Mondy huko YouTube alipata ‘views’ milioni 149, Kili Paul milioni 62, wakati upande wa wanamuziki, Diamond alipata milioni 53, Zuchu milioni 13, Rayvanny milioni 11 na Harmonize milioni 11.

Na YouTube ndiyo mtandao kinara kwa kuwalipa vizuri watu wake kupitia matangazo yao ambayo yanawafikia watumiaji bilioni 2.50 kila mwezi ikiwa ni zaidi ya asilimia 10 ya idadi ya bilioni 2.24 ambayo Meta iliripoti kwa Facebook.

Ikumbukwe Meta ndiyo wamiliki wa Facebook na Instagram ambao hivi karibuni wametangaza kuanza kuwalipa watu wake, yaani watengenezaji maudhui katika mitandao hiyo.

Kili Paul mwenye wafuasi milioni 10.1 Instagram tangu ajiunge na mtandaoni Aprili 2016 anaweza kuwa mnufaika wa mradi huku akifukuzia rekodi ya Diamond mwenye wafuasi milioni 17. 8 aliowakusanya tangu Julai 2012 na kumfanya kuwa kinara kwa Tanzania.

                     

Hayo yanajiri wakati uchunguzi wa Kepios unaonesha kulikuwa na watumiaji  wa mitandao ya kijamii bilioni 5.17 duniani kote hadi mwanzoni mwa Julai 2024, ikiwa ni sawa na asilimia 63.7 ya idadi ya watu wote duniani.

Idadi ya watumiaji imeongezeka kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita ambapo watu milioni 282 walijiunga katika mitandao hiyo ikiwa ni sawa na ukuaji wa kila mwaka wa asilimia 5.8.

Akizungumza na Mwananchi, Kili Paul amesema mafanikio anayopata kwa sasa ni ishara kuwa juhudi zake zimezaa matunda kitu ambacho kinampa nguvu ya kuendelea kuumiza kichwa ili kusonga mbele zaidi.

“Nafurahi kwa sababu kutoka kuwa na mfuasi mmoja hadi milioni moja na sasa milioni 10, ni hatua kubwa ambayo inanihamasisha kuendelea na hiki ninachokifanya maana wengi wanakipenda na kinawavutia kila siku zinavyozidi kwenda,” anasema.  

“Hiyo inaonesha kile ambacho nakifanya kinalipa, ninafurahi maana nilikuwa mtu ambaye sitambuliki popote na walikuwepo watu wengi hapo kwenye chati na sasa nimewapiku wote,” anasema Kili Paul.

Kuhusu kuja kuwa Mtanzania mwenye wafuasi wengi TikTok, Instagram na YouTube, hivyo kumpita Diamond, Kili Paul amesema anajiona huko muda siyo mrefu sababu ana mashabiki wengi kutoka nje hasa nchini India.

“Najiona huko kwa sababu kama YouTube imekua kwa haraka sana hadi kufikia hapo ilipo, pia ukiangalia mashabiki wangu wengi ni Wahindi na anajua India ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi duniani ikiwa na watu karibia bilioni 1.4, imewapita hadi China,” anasema.  

“Kwa hiyo wamenisaidia, wananipenda na wananiheshimu, hivyo muda siyo mrefu nitakuwa kweli namba Tanzania kwa sababu watu wengi wa nje wananifahamu na kazi zangu, hivyo hilo linawezekana hivi karibuni,” anasema Kili Paul.  

Anasema hatua aliyofika hakuna ubishi kwamba kazi yake imekubalika vilivyo, ukiachana na masuala ya kifedha, amefanikiwa kukuza chapa na kuongeza mashabiki wapya, mathalani Diamond mwenyewe ni shabiki yake na wamekuwa wakiwasiliana.

                         

Je, kwanini watengezaji maudhui mtandaoni wanafanikiwa zaidi kuliko wanamuziki?, Kili Paul anasema ni kwa sababu wamekuja na kitu cha tofauti.  

“Wasanii wanaweka video ndefu hadi dakika tatu ila sisi tunaweka video fupi, kama mimi nimekua kwa haraka kwa sababu naweka video fupi sana za kama sekundi 30 au 15, na short video kwenye YouTube ndizo zinavutia watu wengi.” 

Utakumbuka Oktoba 2020, Kili Paul alienda India na kushiriki katika TV Show maarufu nchini humo Big Boss 16 ambayo ilisimamiwa na msanii mkongwe wa filamu, Salman Khan.