Rostam ayaishi maono ya Rais Samia, Hichelema

Mfanyabiashara Rostam Aziz akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ikulu ya Zambia kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, Hakainde Hichelema, kuhusiana na uwekeaaji.
Picha na Peter Nyanje
Muktasari:
Wakati watu wakisifu hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Zambia, Hakainde Hichelema, kuimarisha uhusiano wa kibishara baina ya nchi hizo mbili, mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz tayari alishaanza kuyafanyia kazi maono hayo.
Wakati watu wakisifu hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Zambia, Hakainde Hichelema, kuimarisha uhusiano wa kibishara baina ya nchi hizo mbili, mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz tayari alishaanza kuyafanyia kazi maono hayo.
Wakati Rais Samia akitua Lusaka Zambia mwanzoni mwa wiki hii kwa ziara ya siku tatu iliyozaa makubaliano ya kuimarisha biashara baina ya Tanzania na Zambia, mfanyabiashara huyo alishaanzisha mwendo kwani siku chache zilizotangulia ziara hiyo alikuwa jijini Lusaka kuendeleza fursa za uwekezaji.
Katika safari yake Rostam, si tu alikamilisha mpango huo wa uwekezaji, bali pia alikutana na Rais wa nchini hiyo, Hichelema, na kumhakikishia kuwa ameamua kuingia nchini humo na kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo mengi.
Kupitia kampuni anayoimiliki ya Taifa Gas, Rostam amefanikiwa kupata mbia nchini Zambia na kuingia makubaliano ya awali kuwekeza katika eneo la uzalishaji umeme.
Taifa Gas ya Rostam imeingia ubia na kampuni ya Delta Marimba ya Zambia na kuunda kampuni ya Taifa Marimba, ambayo tayari imeshatenga kiasi cha dola milioni 100 za Marekani za awali zitakawekezwa kwenye uzalishaji wa umeme nchini humo.
Katika uwekezaji huo, Taifa Marimba inatumia kiasi hicho cha fedha kwa kuanzia, kuzalisha megawati 100 za umeme kwa njia ya gesi kwa kugeuza mitambo ambayo awali ilikuwa ikitumia dizeli. Mtambo huo utajengwa katika eneo la Kasama.
Rais Hichilema, ameonyesha kufurahishwa kwake na hatua hiyo na kumhakikishia Rostam Aziz kuwa serikali yake itatoa kila ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha uwekezaji huo.
“Tunaunga mkono uwekezaji huu si tu kwa sababu utatusaidia kupunguza tatizo ya upungufu wa umeme lakini mimi ninaamini kuwa muungano kama huu kwa kampuni za Afrika ni moja ya njia bora za kuleta maendeleo kwa haraka barani mwetu,” alisema Hichelema wakati akizungumza na Aziz aliyemtembelea Ikulu na ujumbe wake Ijumaa ya wiki iliyopita.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili walisitiza kuwa ni wakati sasa kwa Afrika kuwa na mkakati mahsusi utakaowezesha kampuni zake kuungana na kuzitumia rasilimali zilizopo kwenye bara hilo kwa ajili ya manufaa ya watu wake.
Hilo ni moja ya mambo ambayo yalisistizwa wakati wa ziara ya Dk Samia nchini humo iliyomalizika jana.
“Taifa Marimba imeamua kufanya uwekezaji huu ili kuonyesha dhamira yetu kuimarisha uhusiano wa kidugu na wa kihistoria baina ya nchi zetu mbili. Pia tunaamini kuwa hii ni moja ya njia bora kabisa ya kuhakikisha Afrika inajikwamua kiuchumi,” alisisitiza Aziz.
Kutokana na hilo, Rais Hichelema alizihimiza kampuni za Zambia kutafuta wabia ndani na nje ya nchi ili kuweza kukusanya nguvu za kuwekeza katika miradi mikubwa ya kiuchumi na kijamii, hasa miradi ya uchimbaji madini an myororow ake wa thamani.
“Kuongeza thamani ya bidhaa katika sekta yetu ya madini kutaharakisha ukuaji wa uchumi, kuzalisha ajira na fursa za biashara katika mnyororo huo wa thamani. Nina hamu ya kuona kampuni nyingi za Zambia zikiungana na kampuni nyingine kutoka nje ya nchi ili kufanikisha hili,” alisema Rais Hichelema.
Aidha, Rais Hichelema alibainisha kuwa serikali yake inalenga kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kwani uzalishaji kwa njia ya maji, ambao umezoeleka kwa miaka mingi, umeanza kupata matatizo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Ndio maana inapotokea fursa kama hii ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vingine kama ambavyo inavyoelekea kufanya Taifa Marimba tunaiunga mkono kwa sababu itatuhakikishia uzalishaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya wananchi wetu na shughuli za kiuchumi na kijamii,” alisisitiza.
Kwa mujibuwa Rostam Aziz, uwekezaji wa awali utalenga uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi kwa kubadilisha mitambo ambayo awali ilikuwa inatumia dizeli. Lakini uwekezaji huo utapanuliwa siku za usoni katika maeneo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za jua na upepo.
“Pia tutawekeza katika maeneo mengine nje ya yuzalishaji umeme. Sisi Taifa Marimba tutakuwa mabalozi wazuri wa kushawishi kampuni nyingine kuja kuwekeza hapa ambako kuna fursa nyingi sana,” alisema Aziz.
Mwenyekiti wa Delta Marimba, Padmore Muleya, alisema kuwa mtambo wa kwanza utakaozalisha megawati 100 za umeme kutokana na gesi unatarajiwa kuanza uzalishaji katika kipindi cha miezi 24 ijayo.