Vodacom kutotoa gawio baada ya kupata hasara

Vodacom kutotoa gawio baada ya kupata hasara

Muktasari:

Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni ya simu ya Vodacom imesema hakutakuwa na gawio kwa wanahisa katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Machi, 2021.

Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni ya simu ya Vodacom imesema hakutakuwa na gawio kwa wanahisa katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Machi, 2021.

Sababu za kutotolewa kwa gawio hilo ni hasara ya Sh30 bilioni iliyopatikana katika kipindi hicho na hii inakuwa mara ya kwanza kutotolewa kwa gawio tangu kampuni hiyo iorodheshwe katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) Agosti 2017.

“Kutokana na hasara iliyopatikana baada ya kulipa kodi, bodi ya wakurugenzi imeamua kutopendekeza gawio katika kipindi hicho cha mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2021,” ilieleza taarifa ya kampuni hiyo ya hesabu za awali.

Katika taarifa hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom, Hisham Hendi alisema hasara hiyo inatokana na namna kodi ilivyokokotolewa na kusababisha kutozwa kiwango kikubwa tofauti na mwaka uliopita.

Pia alibainishwa suala la kufungwa kwa laini milioni 2.9 za wateja wao ambao hawakukamilisha usajili liliathiri mapato na faida ya kampuni hiyo.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita (ulioishia Machi, 2020) Vodacom ilipata faida halisi ya Sh45.76 bilioni ikipungua kutoka Sh90.76 bilioni iliyopatikana kwa mwaka ulioishia Machi, 2019.

Faida ya mwaka 2020 ilipungua kutokana na kuongezeka kwa gharama za kuhakikisha wateja wote wanasajiliwa kwa alama za vidole na gharama za kupambana na ugonjwa wa Covid-19 pamoja na kuendelea kupanua mtandao wa huduma.

Kwa siku zilizopita, Vodacom imekuwa na mwenendo mzuri wa ufanisi mwaka jana ilitoa jumla ya Sh54.5 bilioni kama gawio na Sh400 bilioni zilitolewa kama gawio maalumu ambalo ni sawa na Sh178.57 kwa hisa moja.

Kwa mujibu wa taarifa za fedha za kampuni hiyo za hivi karibuni, mapato na faida yake vitaendelea kuzorota endapo hawatamaliza mizozo ya kikodi baina yao na TRA au Mahakama ya kodi.