‘Chiveleve’ siri ya shule kushika mkia Mtwara

Muktasari:
- Gazeti la Mwananchi limefanya uchunguzi na kugundua sababu mbalimbali zinazogusa maeneo tofauti tofauti.
- Sababu ya kwanza ni wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza wengi wao huwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mtwara. Baada ya Baraza la Mitihani (NECTA) kutangaza matokeo ya kidato cha pili na darasa la nne, mwaka jana, Mkoa wa Mtwara ulishika mkia kutokana na shule tisa kati ya 10 kufanya vibaya.
Gazeti la Mwananchi limefanya uchunguzi na kugundua sababu mbalimbali zinazogusa maeneo tofauti tofauti.
Sababu ya kwanza ni wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza wengi wao huwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Katika walimu wote wa shule waliofanya mahojiano na gazeti hili wameeleza hii ni sababu namba moja ya wanafunzi kufanya vibaya kutokana na kukosa stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika hali inayomlazimu mwalimu kuanza kumfundisha kusoma badala ya kumwanzishia masomo ya kidato cha kwanza.
Mkuu wa Shule ya Naputa, Rajab Nampoto anasema wamekuwa wakipokea wanafunzi wa aina hiyo, hivyo walimu hulazimika kuanza kuwafundisha kusoma badala ya kutekeleza mitalaa.
“Ni kweli tumefanya vibaya lakini sababu zipo nyingi, sisi tunapokea wanafunzi waliofaulu elimu ya msingi lakini tunakuta baadhi yao hawana stadi za 3K kwa hiyo tunalazimika tuanze nao kuwafundisha kusoma, kuandika na kuhesabu,” anasema Nampoto na kuongeza:
“Wakati wa mitihani ya kidato cha pili waliosajiliwa ni 110, waliofanya mitihani ni 108 lakini waliofaulu ni 42 na waliofeli ni 66 lakini yupo mwanafunzi aliyefanya mitihani nusu kutokana na utoro na baadhi ya wazazi hawachukui utambuzi wa watoto wao,”anasema.
Naye mwalimu Fatuma Hussein kutoka shule ya sekondari Chingungwe anasema baadhi ya wanafunzi inabidi uanze kuwafundisha a e i o u kutokana na kutokujua kabisa kusoma, hivyo inakuwa kama unamuanzisha darasa la kwanza badala ya hivyo kushindwa kuwafundisha masomo ya kidato cha kwanza.
“Baadhi hawajui kusoma kabisa
wala kuandika mimi binafsi wapo nilioanza nao kwa kuwafundisha kusoma a, e, i, o, u, mmoja yuko kidato cha pili sasa na hajui kusoma wengine wameamua kuwa watoro,” anasema Mwalimu Fatuma.
Chiveleve ndiyo habari ya mjini
Inaelezwa kuwa moja ya sababu inayochangia wanafunzi kufanya vibaya katika mkoa huo ni tabia ya wazazi kuwapa mafunzo ya unyago (cheveleve) na jinsi ya kumuhudumia mume watoto wadogo wa shule za msingi na wakati mwengine hata wale ambao hawajaanza kusoma.
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Sebastian Waryuba anasema tabia hiyo imeota mizizi wilayani kwake na kuwataka wazazi na walezi kubadilika ili kupunguza kuwafundisha watoto wadogo wa kike masuala ya ngono.
“Katika wilaya yangu ni jambo la kawaida kabisa kukuta baadhi ya wazazi na walezi wanawapeleka watoto katika shughuli za unyago ambapo huko hufundishwa mambo mbalimbali ya ukubwa. Cha kusikitisha zaidi wanawafundisha mambo makubwa hasa ya kuwahudumia wanaume ilhali bado watoto wadogo jambo linalochangia kuzorotesha juhusi za kumkomboa mtoto.”
Anasema mtoto mdogo hapaswi kufundishwa masuala ya ngono na badala yake anapaswa kuandaliwa katika misingi bora ikiwamo kupatiwa elimu bora ili iweze kumsaidia katika maisha yake.
Kutoroka kufanya mitihani
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walimu kutoka shule tofauti zilizopo wilayani Tandahimba wamelalamikia suala la utoro kwa wanafunzi hali iliyopelekea hata baadhi ya watahiniwa kushindwa kufanya mitihani yote hivyo kupelekea shule za mkoa huo kuwa miongoni mwa zilizofanya vibaya.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Lukokoda, Azizi Ndimbe anasema shule yake ilisajili wanafunzi 44 kwa ajili ya mitihani ya kidato cha pili lakini walioweza kufanya mitihani ni 38, kwani sita hawakutokea kufanya mitihani.
“Utoro umekuwa kikwazo kikubwa, wanafunzi sita hawakufanya mitihani kutokana na utoro na mmoja alikuwa mjamzito, tumekuwa tukijaribu kuwaita wazazi kukaa nao na kuzungumza nao lakini baadhi hawatuelewi licha ya kuwa afisa mtendaji huwa anatia msukumo wa elimu,” anasema Ndimbe.
Naye mwalimu Betina Pascal anasema kutokana na wanafunzi wengine kutoka vijiji vya mbali pindi wanapoharibikiwa na baiskeli zao hulazimika kukosa masomo huku baadhi ya wazazi wakienda shuleni hapo kuwaombea watoto wao ruhusa kwa kisingizio ni wagonjwa na kwenda kujishughulisha na shughuli nyingine kama biashara ya supu na kuzurura mitaani.
“Mzazi anaweza akaja hapa akamwambia mwalimu mwanangu anaumwa hivyo hawezi kufika shule lakini cha kushangaza mtoto yule aliyeombewa ruhusa unamwona anapita eneo la shule na biashara au mwingine akishaona mazingira ya shule na nyumbani yalivyo anaamua aolewe. Wengi wanaoacha shule wanakuwa ni wajawazito,” anasema mwalimu Betina.
Uhaba wa walimu wa Sayansi na Hisabati
Uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati nao umeelezwa kuwa kikwazo kikubwa katika shule zote za mkoa wa Mtwara huku baadhi ya shule zikikosa mwalimu wa somo la Hisabati toka kuanzishwa kwa shule.
Mkuu msaidizi wa Shule ya Salama, Omari Mnomba anasema shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa walimu wa masomo ya Fizikia, Bailogia, Kemia na Hisabati na kueleza toka kuanzishwa kwake mwaka 2007 haijawahi kupata mwalimu wa somo la Hisabati na hata waliokuwa wakifundisha masomo ya Fizikia na Bailojia waliondoka.
Anasema katika shule hiyo walisajiliwa wanafunzi 57 lakini mmoja hakufanya mitihani kutokana na mimba na kusema uelewa mdogo wa wanafunzi ndio unaosababisha ufaulu mdogo kwani hata hao wanaojua kusoma na kuandika siyo kwa kiwango cha mtoto wa kidato cha kwanza na wengine huacha shule kwa utoro na wengine kutokana na mimba.
Mapenzi na shule
Sababu nyingine inatajwa ni baadhi ya wanafunzi kujihusisha kimapenzi wanafunzi kwa wanafunzi na wengine wakijihusisha kimapenzi na wanajamii hali ambayo inamfanya mwanafunzi asiwe makini na masomo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Chingungwe, Hawa Ismail anasema wanafunzi kwa wanafunzi wamekuwa wakijihusisha kimapenzi na wengine wamekuwa wakijihusisha na wanakijiji na kwamba alipokamata simu za wanafunzi ndipo aligundua tatizo hilo pamoja na wazazi/walezi kutowajibika kutokana na aina ya ujumbe wa simu anazokuta kwenye simu.
“Baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijihusisha kimapenzi wenyewe kwa wenyewe na wengine wamekuwa wakijihusisha na wanakijiji, shuleni kwangu zilikamatwa simu mbili nilipozikagua nilichokutana nacho mpaka mhu! Mpaka unajiuliza hivi kweli huyu ni mwanafunzi?
“Lakini wazazi hawawajibiki hata unapomwita na ukimhoji kuhusu simu anakataa hajanunua yeye na mzazi mwingine unaweza kumwita shuleni kutokana na mwenendo wa mwanaye akija anakuwa upande wa mtoto,” anasema mkuu wa shule.
Mila na desturi
Imedaiwa kuwa baadhi ya wanafunzi kuna wakati hukosa masomo kutokana na kuwa kwenye unyago hali inayomlazimu mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba kupiga marufuku shughuli za unyago kipindi shule zinapofunguliwa na kuwatahadharisha wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi.
“Marufuku unyago siku za shule, utekelezaji wa mila usiathiri watoto kukosa elimu... sisi hatuzuii mila tunaziratibu zisimwathiri mtoto, kikubwa tusaidie watoto wa Tandahimba wapate elimu kwani ni haki yao na itawasaidia na wale wazazi wote wanaokwamisha watoto kwenda shule wachukuliwe hatua mara moja na wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi waache, tutawazika mzima mzima,” anasema Waryuba.
Mwamko mdogo wa elimu
Baadhi ya wanafunzi waliofaulu katika mitihani wanasema matokeo mabaya yamechangiwa na uzembe wa wanafunzi wenyewe pamoja na wazazi/walezi kutokufahamu umuhimu wa elimu kwa karne ya sasa.
Mwanafunzi Mfaume Hashim wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Chinguwe anasema Serikali na wadau wanapaswa kuwapa kwanza elimu wazazi wafahamu umuhimu wa elimu kwani baadhi wamekuwa wakiwapangia watoto wao majukumu hata wakati wanapohitaji kusoma kutokana na wao wenyewe kutojua umuhimu wa elimu.
“Wanafunzi tunafeli kwa sababu muda wa kusoma hatuna, tunapofika nyumbani kazi zinakuwa nyingi kama kukata kuni, halafu baadaye tunashindwa kusoma, mfano kama mimi sina ndugu wa kike naambiwa nipike na kufanya shughuli nyingine nnapomaliza usingizi unakuwa ushanibana inabidi nilale badala ya kusoma, naiomba Serikali iwape ushauri wazazi, kuwepo na mikutano ya kijiji waelezwe umuhimu wa elimu,” anasema Hashim.
Mzazi Ismail Bure kutoka kijiji cha Lukokoda anasema uzembe wa baadhi ya wazazi nao unachangia watoto kutopenda kusoma.
“Mwanangu mwenyewe alikuwa anapenda kusoma sikumlazimisha, hata alipomaliza darasa la saba alifaulu, mimi nikawa namtega niangalie akili yake ikoje lakini akanambia baba mimi nataka nisome nifike wanakoita chuo kikuu, sitaki kukaa hapa unilishe tu ugali wako kwa hiyo nikaanza kumgharamia lakini angenambia hataki kusoma ningempeleka polisi kumshtaki kwa sababu umri alionao kwanza hawezi kufuatana na mimi shamba kulima,” anasema Bure.
Mzazi Tabia Joram mkazi wa kijiji cha Chingunge anasema sio lazima kwa mtoto kusoma kama hapendi kwani kuna sababu mbalimbali zinazomfanya ashindwe kusoma.
“Kusoma siyo lazima kama mtoto hapendi shule asilazimishwe unaweza ukamlazimisha mtoto wewe mzazi ukapoteza pesa zako na muda wa mtoto, mimi ninachokitaka mtoto wangu ajue kusoma, kuandika na kuhesaba pesa, ili akifanya mambo yake yakae sawa,” anasema Joram.
Tatizo nyumba za walimu
Walimu kuishi mbali na vituo vya kazi na kuwachotesha wanafunzi maji. Mmoja wa wazazi, mzee Shaban Mfaume anasema kitendo cha walimu kukaa mbali na mazingira ya shule kinachangia wanafunzi kufeli jambo ambalo walimu wanasema wanalazimika kukaa mbali kutokana na vijiji kukosa nyumba za kupanga na huduma nyinginezo kama umeme na maji na hata nyumba wanazozipata zilizo za kawaida hupangishwa kwa bei kubwa.
Mwalimu Betina Pascal anasema: “Tunakuwa kazini lakini pia nyumba za kupanga zinakuwa hazipo unakuta mtu amejenga nyumba ya kujitosheleza yeye na familia yake, ilifikia kipindi walimu tukawa tunaishi kama tupo ‘big brother’ kitu ambacho siyo kizuri hata sisi hatufurahii kukaa mbali,” anasema mwalimu Betina.
Watoto kutumwa na walimu
Baadhi ya wazazi wanalalamikia watoto wao kuchoteshwa maji kipindi wawapo shuleni, hivyo kusababisha kutopata elimu wanayostahili kuipata.
Mwalimu mkuu msaidizi shule ya sekondari ya Chingungwe, Ludovick Somi anasema wanalazimika kuwatuma wanafunzi wakachote maji kwa ajili ya kupikia chakula cha wanafunzi shuleni, sasa kutokana na kijiji chao kukosa maji hasa wakati wa kipindi cha kiangazi, hubidi wanafunzi waende mbali kutafuta maji.
Ushirikina
Baadhi ya walimu wanaeleza kuwa wanapoishi katika nyumba za shule wamekuwa wakitendewa mambo ya miujiza na kuibiwa hali iliyowalazimu kuhamisha makazi yao katika kijiji husika na kuhamia maeneo ya mbali na shule.
Akizungumzia madai hayo, mmoja wa mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari Lukokoda, Abbas Membe (Jogologo)anasema walimu waliwahi kuwasimulia kuhusu madai hayo na wao kama bodi walilishughulikia tatizo hilo.
“Wale walimu wa mwanzo walikuwa wanalala kwenye chumba kimoja wengi na suala la kuibiwa walikuwa wakiibiwa kwa sababu wakati mwingine walikuwa wakiacha vitu vyao kwenye nyumba ya shule wanakwenda kuishi Tandahimba, hawakuwa wanaibiwa wakati wakiwapo, lakini pia ilitokezea wakilala pale wanajikuta wakifanyiwa mambo ya miujiza (uchawi).
“Waliwahi kutusimulia na walimu wakawa wanaogopa kuishi katika nyumba ya shule, sisi tukachukua jitihada kama bodi tukasema hilo jambo tunaweza tukalimaliza. Tukazungumza na wanakijiji wakatuelewa. Mimi naweza kusema hilo lilishakwisha,” anasema Membe.
Wanafunzi kufyatua tofali
Walimu wanadai kuna kipindi wanafunzi wamekuwa wakiacha masomo na kwenda kujishughulisha na kazi ya kufyatua matofali kwa ajili ya kupata pesa za haraka haraka na hivyo kuathiri mahudhurio yao darasani jambo ambalo mwenyekiti wa bodi ya shule ya Lukokoda anakiri kulitambua.
“Kuna maeneo wanafyatua tofali za kuchoma, inapofika mwezi wa pili, wa tatu na wa nne wanafunzi wanakwenda kufyatua tofali moja kwa Sh10 kwa hiyo watoto hadi wa shule za msingi wanakwenda kufyatua tofali na hata wengine kuendesha familia kwa sababu anaweza akapata Sh15,000 au Sh 20,000 akachukua sehemu ya pesa akanunua chakula,” anasema Membe na kuongeza:
“Na hapa ilipo shule watoto wengi wanaongoza kwa kuacha kusoma achilia mbali kufeli, hata kuacha kusoma hapa wanaongoza, tumehamasisha sana lakini bado, nimejaribu kuweka vitisho kuwapeleka polisi lakini hilo tatizo bado lipo, tunafanya mikutano na wazazi tunawahamasisha namna gani elimu itawasaidia lakini watu wengi wanakosa hamasa, wengine walifika mahali hata wakatamka kuwa si lazima watoto wao kusoma hivyo wasiende shule wafanya mambo mengine ya kuwapatia kipato,” anaeleza Membe.
Wasemavyo watendaji
Ofisa elimu wilaya ya Tandahimba, Sosthenes Luhende anasema sababu za shule kufanya vibaya zipo nyingi ikiwamo utoro kwa wanafunzi na ushirikiano mdogo kwa wazazi. Kadhalika lipo tatizo la kutokuwa na uwiano mzuri wa walimu.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Tandahimba, Said Msomoka anasema katika bajeti ya mwaka 2017/18 wametenga kiasi cha Sh48 milioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu kupitia mfuko wao wa elimu pamoja.
Kadhalika zimetengwa kiasi cha Sh10 milioni kukipa nguvu kitengo cha ukaguzi wa elimu wanaoangalia ubora wa elimu kutokana na kutotekeleza majukumu yake kutokana na ufinyu wa bajeti. Fedha nyingine ni zilizotengwa Sh78 milioni kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kupata uji mashuleni.
Mkuu wa mkoa
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego anasema matokeo yamekuwa mabaya kutokana na udanganyifu uliokuwa ukifanyika shule za msingi.
Anasema katika kipindi chake cha uongozi amewahi kurudishiwa wanafunzi wapatao 16 kutoka shule za vipaji maalumu walizokuwa wamepangwa baada ya kuonekana uwezo wao ni mdogo.
“Hili ni tatizo na kama viongozi tumelipokea kwa masikitiko makubwa lakini kubwa ni kuhakikisha tunazifanyia kazi zile changamoto ambazo tumeona ndizo zinarudisha masuala ya elimu nyuma.
“Sisi bahati nzuri tulishaweka tathmini kama mkoa tukaona mafanikio na pia changamoto hivyo tumeanza kuzifanyia kazi,” anasema Dendego na kuongeza:
“Kama mkoa tumekuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa, mabweni, nyumba za walimu na madawati. Tatizo la ukosefu wa madawati tumeshalifanyia kazi tukamaliza.
“Kuhusu suala la madarasa hata kabla ya kuelekezwa tulishaanza mchakato wa kuanzisha benki ya matofali kila kijiji kiwe na angalau tofali milioni moja za kuchoma kama ni za saruji ni tofali laki tatu.
“Lengo ni kuondokana na uhaba wa madarasa kwa sababu tulishaona tuna uhaba wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu, hivyo tumepanga mikakati ya kuwashirikisha wananchi ili tuweze kuvinyanyua vyote kwa kasi na kumaliza tatizo hilo,” anasema Dendego.
Kuhusu suala la walimu wa Sayansi na Hisabati, mkuu huyo wa mkoa anasema kuna upungufu wa walimu zaidi ya 600, kama mkoa wamefanya mpango wa muda mfupi wa kutumia walimu walio wanachuo wakati wa likizo kuliko wanafunzi kukaa bila kufundishwa kabisa.