Chinua Achebe, Baba wa Fasihi Afrika tunakulilia

Muktasari:
Achebe alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 83 nchini Marekani baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Hakuna shaka kwamba katika fasihi, si Watanzania au hata Waafrika ambao wamepoteza nguzo muhimu ambayo daima ilikuwa chachu ya uhuru na ulinzi wa mila.
Nigeria inalia. Afrika inaomboleza, ulimwengu wa fasihi umeweka tanga.
Machi 21, 2013 ni siku ambayo Baba wa Fasihi Afrika- mwasisi wa riwaya za kimapinduzi Afrika - shujaa wa taifa la Nigeria, Chinualumogu Okafo Achebe … aliaga dunia.
Achebe alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 83 nchini Marekani baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Hakuna shaka kwamba katika fasihi, si Watanzania au hata Waafrika ambao wamepoteza nguzo muhimu ambayo daima ilikuwa chachu ya uhuru na ulinzi wa mila.
Riwaya zake Achebe , zilimfanya kiongozi na mwalimu mzuri wa fasihi kwa shule za sekondari, ingawa wengi hawakuwahi kuuona uso wake.
Kwa jumla, Achebe alikuwa mburudishaji kwa karne nyingi kutokana na uandishi wake wa kipekee na riwaya tamu zenye ujumbe.
Wino wa kalamu yake ulioanza kujulikana mwaka 1958 kwa riwaya ya kwanza ya Things Fall Apart ulisambaa dunia nzima na alijulikana kwa umahiri wa kazi zake zenye kuchimbua ukweli, kuelimisha na hata kuburudisha.
Wapenzi wa siasa watamkumbuka kwa kuchambua na kuelezea harakati za kimapinduzi katika nchi za kufikirika za Afrika, lakini zenye uhalisia katika maisha ya kawaida.
Watoto watamkumbuka kwa kazi zake lukuki zilizosimulia hadithi fupi fupi.
Ameiaga dunia, lakini bado anafananishwa na jabali la fasihi kwa uwezo wake wa kutumia lugha ya picha kueleza dhima ya riwaya, aliweza kuwachora wahusika wake kwa kuwapa majina yanayoendana na nafasi zao.
Anakumbukwa kupitia, ‘Things Fall Apart’ ambayo ilitafsirwa kwa lugha ya Kiswahili na kuitwa‘Amkani si Shwari Tena’.
Wakati wakoloni walipoanza kuwakosoa Waafrika kuwa hawana Fasihi ya Kiswahili ndipo Achebe alipoandika riwaya ile, ‘Things Fall Apart’ mwaka 1958, akiwa kijana wa miaka 28.
‘Things Fall Apart,’ ni riwaya iliyosawiri harakati za kupigana dhidi ya ukoloni wa Kiingereza kwatu wa kabila la Waigbo nchini Nigeria.
Riwaya hiyo, daima imebaki kuwa miongoni mwa kazi bora Afrika, iliyouza nakala zaidi ya milioni kumi na kutafsiriwa kwa lugha tofauti 50 duniani.
Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliposoma riwaya hiyo alipata kuisifu na kusema, “Ni mwandishi ambaye kwa maandishi yake anaweza kuvunja kuta za gereza”
Ni Mwafrika wa kwanza kuandika riwaya za kimapinduzi bila hofu na pia kuonyesha kazi za wakoloni Afrika.
Baada ya kupata ajali ya gari mwaka 1990, Achebe alipooza kuanzia kiunoni hadi miguuni na alitumia gari la magurudumu kutembea hadi mauti yalipomfika.
Hata hivyo, hakuacha kazi yake… aliendelea kuandika na kuhamasisha. Mwaka jana, alitoa riwaya yake ya mwisho, ‘There Was a Country, ambayo inaelezea namna alivyojionea vita katika mji wa Biafra nchini Nigeria, mwaka 1967 -1970.
Ametumia sehemu kubwa ya maisha yake nchini Marekani ambapo alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Brown.
Maisha yake
Alizaliwa Novemba 16,1930 katika mji wa Igbo, Ogidi kusini mwa Nigeria.
Wazazi wake Isaiah, Okafo Achebe na Janet Anaechi walimlea katika misingi ya dini na kutokana na werevu katika masomo , alipata udhamini wa elimu ya juu.
Awali, Achebe alipewa jina la Albert Chinualumogu Achebe, lakini baadaye alilikataa jina la Albert kwa kuwa ni la kimagharibi na kubaki na Chinua Achebe.
Akiwa shule za sekondari na msingi, mara kadhaa aliwahi kurushwa madarasa kutokana na uwezo na werevu wake mkubwa, jambo lililomfanya amalize shule akiwa na umri mdogo.
Baada ya kuingia Chuo Kikuu, Achebe na maktaba walikuwa marafiki wa kudumu. Huko alitumia muda wake mwingi akisoma kazi mbalimbali za fasihi.
Hakuishia alipendelea kuandika hadithi mbalimbali na alipomaliza masomo chuo kikuu aliajiriwa katika kituo cha utangazaji Nigeria, NBS.
Mwaka 1967 wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe huko, Biafra alikuwa mtetezi wa watu hao na alizungumza na nchi za magharibi ili kupata msaada.
Alijaribu kuingia katika vyama vya siasa mwaka 1970, lakini aliacha baada ya kushuhudia rushwa na uvunjaji wa sheria uliokithiri.
Aliwahi pia kuwa mwalimu wa somo la Kiingereza katika mji wa Oba.
Septemba 1961, Achebe alifunga ndoa na Christie Okeli, mfanyakazi mwenzake katika televisheni ya NBS.
Achebe aliwahi kuzuru Afrika Mashariki, ambapo alitembelea Kenya na Tanzania na alikutana na mwanariwaya wa Tanzania, Shabaan Robert.
Wasemavyo wengine
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Method Samwel anasema, Achebe amefariki wakati ambapo fasihi inahitajika zaidi kimaendeleo.
“Kama mwanataaluma ameacha pengo kubwa, alikuwa kama nabii katika kazi zake,” anasema Dk Samwel.
Dk Samwel anasema Achebe alikuwa ni mtu mwenye uono wa mbali.
“Tumepoteza mtu muhimu sana na mwanafasihi aliyetukuta,” anasema
Mhadhiri wa Lugha, katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa David Massamba anasema kifo cha Achebe ni pigo kwa wasomi na wapenzi wa fasihi nchini.
“Tumesikitika sana, ni mtu aliyetegemewa Afrika, alikuwa mstari wa kwanza katika kulinda mila za afrika, alistahili kuigwa,” anasema Profesa Massamba
Anasema Chinua Achebe amefariki wakati ambapo alikuwa akihitajika mno kuelimisha kuhusu fasihi na umuhimu wake katika nchi za Afrika.
Naye Richard Mabala anasema,” Mwandishi aliyekonga nyoyo za kizazi changu na hata vizazi vilivyofuata ameaga dunia. Alikuwa mwandishi mashuhuri, mchambuzi asiye na uoga, aliyetuletea furaha na akili.”
Baadhi ya kazi za fasihi ambazo zimembeba na kumtmbulisha ni ; No Longer at Ease (1960), Arrow of God(1964), Girls at War(1973) Anthills of the Savannah (1984), En Bild Von Africa(2000),na riwaya yake ya mwisho, There Was A Country, aliyoipakua mwaka jana.
Nukuu ambayo ameiacha ikiwa hai duniani ni ile ya mwaka jana, 2012 isemayo, “Wasikilize kwa makini wazee wanapozungumza, si kwa sababu ya utamu wa maneno yao, bali kwa sababu tunaona mambo ambayo wewe huyaoni.”