Mkuu wa intelijensia wa jeshi la Israel ajiuzulu

Meja Jenerali Aharon Haliva

Muktasari:

 Aharon Haliva  anatajwa kuwa ofisa wa ngazi ya juu kuachia ngazi tangu kutokea kwa uvamizi wa Hamas Oktoba 7, 2023 na kusababisha vita ukanda wa Gaza

Israel. Jeshi la Israel limetangaza kujiuzulu kwa mkuu wake wa idara ya intelijensia baada ya kushindwa kuzuia shambulio la Oktoba 7, 2023 lililofanywa na Kundi la Hamas kutoka Palestina.

Meja Jenerali Aharon Haliva ambaye ni Mkuu wa Kurugenzi ya Ujasusi wa Kijeshi anatajwa kuwa ndiye ofisa wa kwanza wa ngazi ya juu kujiuzulu kwa kushindwa kuzuia shambulio hilo lililoishangaza Israel na jumuiya ya kimataifa.

"Meja Jenerali Aharon Haliva, ameomba kujiuzulu nafasi yake, kufuatia jukumu lake la uongozi kama mkuu wa kurugenzi ya upelelezi," limesema jeshi hilo katika taarifa na kunukuliwa na AFP.

Pia, AFP imesema katika barua yake ya kujiuzulu, Haliva ambaye amehudumu katika kikosi hicho kwa miaka 38, amefikia hatua hiyo baada ya kushindwa kuzuia Hamas kutekeleza shambulizi lililoua watu 1170 siku hiyo na wengine zaidi ya 200 kutekwa nyara.

"Jumamosi, Oktoba 7, 2023, Hamas ilifanya shambulio baya la kushtukiza dhidi ya Taifa la Israeli, Kitengo cha kijasusi chini ya amri yangu hakikutimiza jukumu tulilokabidhiwa," ameandika katika barua hiyo, ambayo nakala yake ilitolewa kwa waandishi wa habari na jeshi hilo.

Katika taarifa nyingine, Tovuti ya Times of Israel imesema Jeshi la Ulinzi wa Israel (IDF) litahitaji kutafuta mbadala wa Haliva.

Pamoja na kujiuzulu kwake duru za ndani zinaeleza kuwa, Haliva  anachunguzwa na jeshi la nchi hiyo kwa kushindwa kwake katika mauaji ya Hamas ya Oktoba 7.

Uchunguzi huo unatarajiwa kuwasilishwa kwa Mnadhimu Mkuu IDF Luteni Jenerali Herzi Halevi mwanzoni mwa Juni.

Tangu wakati huo, Israel imeapa kuiondoa Hamas na inahusika na mashambulizi makali dhidi ya kundi hilo linalotawala ukanda wa Gaza.

(Imeandaliwa na Sute Kamwelwe)