Biden, Trump wanavyopambana majukwaani

Muktasari:

  • Rais Joe Biden na Rais wa zamani, Donald Trump wameendelea kupambana kwenye hotuba zao huku Biden akisema kuhusu utimamu wa akili wa mpinzani wake na Trump anasema kama atashindwa uchaguzi huu itakuwa mwisho wa demokrasia Marekani.

Washington. Wakati Donald Trump akisema kama atashindwa uchaguzi wa urais wa Novemba itakuwa mwisho wa demokrasia Marekani, Rais Joe Biden amemchokoza Trump kwa kuweka utani kwenye hotuba yake kuhusu utimamu wa akili wa mpinzani wake kwenye uchaguzi ujao.

Trump alitoa kauli hizo mwishoni mwa wiki alipohutubia wafuasi wake huko Ohio huku akiendeleza madai yake kwamba ushindi wake ulioporwa kwenye uchaguzi wa 2020 dhidi ya mgombea wa Democratic, Joe Biden ni matokeo ya udanganyifu kwenye uchaguzi.

“Kama hatutashinda uchaguzi huu, sidhani kama kutakuwa na uchaguzi katika nchi hii,” alidai Trump kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Marekani utakaofanyika Novemba 5, mwaka huu.

Wakati Trump akitoa madai hayo, Rais Biden naye alirusha kombora kwenye hotuba yake aliyoitoa wakati wa hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari ya Gridiron jijini Washington.

Klabu hiyo iliyoanzishwa  mwaka 1885 ni maarufu kwa kuandaa chakula cha usiku kwa Rais na viongozi wengine wakiwamo watu maarufu.

Akihutubia kwenye hafla hiyo Biden amesema: “Mmoja wa wagombea ni mzee sana na hayuko timamu kiakili kuwa rais. Mwingine ni mimi.”

 Biden amesema hayo kwenye hafla hiyo iliyofanyika juzi Jumamosi mbele ya waalikwa zaidi ya 650, wakiwamo Waziri Mkuu wa Estonia, Kaja Kallas, Waziri  Mkuu wa Ireland, Leo Varadkar, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, mwanzilishi wa Amazon na gazeti la Washington Post owner Jeff Bezos, na Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok, Shou Zi Chew ambaye mtandao wake unaweza kupigwa marufuku na Biden.

Biden mwenye umri wa miaka 81 anaweza kupambana kwenye uchaguzi ujao na Trump (77) aliyeondolewa madarakani na Biden kwenye uchaguzi wa 2020.

Trump kwenye kampeni zake ndani ya chama chake cha Republican amekuwa akimshutumu Biden kwamba ni mzee sana ambaye nguvu za mwili zimeanza kutoweka.

Wakati Biden akitoa utani huo, Gavana wa Jimbo la Utah kupitia chama cha Republican, Spencer Cox (48) naye alitoa utani kwamba atatangaza kugombea urais mwaka 2052. “Mwaka 2052, wakati nitakuwa kijana kuliko Rais Biden na Rais Trump.”

Mwaka jana kwenye hafla ya chakula cha usiku ya Gridiron, aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa Trump, Mike Pence, alinukuliwa akisema  historia itakuja kumuwajibisha Trump kwa kitendo cha wafuasi wake kuvamia Bunge la Marekani Januari 6, 2021, kuvuruga shughuli za Bunge kwa kuingia ukumbini na mwingine kwenda kukakilia kiti cha Spika.

Katika hotuba yake ya dakika 10, Biden alianza kwa kuchekesha akizungumzia umri wake na Trump kwamba wote ni wazee sana kugombea urais. “Mmoja wa wagombea ni mzee sana na hayuko timamu kiakili kuwa Rais. Mwingine ni  mimi,” amesema Biden.

“Mnajua yeye ni mtu yule yule niliyemshinda mwaka 2020. Lakini sijamwambia. Anadhani anagombea akipambana na Barack Obama. Hivyo ndivyo anavyosema.”