Dunia inavyozungumzia mashambulizi ya makombora ya Iran  dhidi ya Israel

Muktasari:

  • Colombia inaona kama ni kiashiria cha Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, huku Urusi, China, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Papa Francis wametaka utulivu. Marekani, Uingereza, Ujerumani, Canada na Argentina zimetangaza mshikamano na Israel.

Washington. Wakati jumuiya ya kimataifa imeonyesha hofu kuhusu mashambulizi ya makombora ya Iran kwa Israel, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewaita kuwahoji mabalozi wa nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani waliopo Tehran.

“Tumesikia kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewaita mabalozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuwahoji wanadiplomasia hao wa Magharibi juu ya kile Tehran inachokielezea kama msimamo wao ‘wa kutowajibika’ kuhusiana na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.

“Bado hatujasikia kutoka kwa mabalozi wenyewe wanasema nini,” imesema ripoti ya Aljazeera.

Iran imesema mashambulizi yake ya makombora yanayojiendesha na yaliyopo kwenye ndege zisizo na rubani ni kulipa kisasi kwa Israel.

Serikali ya Iran imekuwa ikitishia kuishambulia Israel tangu mashambulizi ya anga yaliyotokea Aprili 1, 2024 kwenye ubalozi wa Iran huko Damascus nchini Syria na kusababisha vifo vya watu 13, wakiwamo majenerali wawili wa jeshi la Iran.

Iran imekuwa ikiituhumu Israel kuhusika na shambulio hilo na kwamba ilichokifanya usiku wa kuamkia leo ni kutuma ujumbe, na imeionya Israel isithubutu kujibu mapigo.

Hata hivyo, jeshi la Israel kwenye taarifa yake limesema wameweza kuyatungua makombora mengi ya Iran nje ya mpaka wa Israel.

Hofu ya mapigano kati ya Israel na Iran imeibuka wakati Israel ikiwa kwenye  vita na wapiganaji wa Hamas  ukanda wa Gaza iliyodumu kwa miezi sita sasa.

Dunia na mashambulizi ya Iran

Rais wa Colombia, Gustavo Petro ameyaita mashambulizi hayo ‘yanayoweza kutabirika’, kwamba ni kama dunia iko kwenye Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, wakati binadamu anatakiwa kuanza kujenga uchumi ulioharibika.

Amesema msaada wa Marekani kwa kile alichokiita mauaji ya halaiki, umeiwasha moto dunia.

 “Kila mtu anajua vita vinavyoanza, lakini hajui vitaishaje. Kama Waisrael wangekuwa juu kama mababu zao wangewalazimisha watawala wa sasa wenye wazimu kuacha mapigano.”

Ameutaka Umoja wa Mataifa kuitisha mkutano wa haraka kuzungumzia amani.

Vatican

Papa Francis amezitaka pande zote kutosababisha kuenea kwa mapigano, huku akionya kutokea vita vya kanda.

"Ninatoa wito wa kukomeshwa kwa hatua yoyote ambayo inaweza kuchochea kuongezeka kwa vurugu ambayo inaweza kuhatarisha Mashariki ya Kati kwenye mzozo mkubwa zaidi."

"Ninaomba kutokana na wasiwasi huu, lakini pia maumivu, habari ambazo zimekuja katika saa za hivi karibuni kuhusu hali mbaya ya Israel kutokana na kuingilia kati kwa Iran," Papa amewaambia waumini kwenye ibada leo asubuhi.

“Hakuna anayepaswa kutishia kuwepo kwa wengine. Nchi zote lazima ziwepo, hata hivyo, ziunge mkono amani na kuwasaidia Waisraeli na Wapalestina kuishi katika mataifa mawili, bega kwa bega na kwa usalama,” amesema.

Argentina

Ofisi ya Rais Javier Milei wa Argentina imesema inaungana na Israel na imelaani shambulio hilo.

“Argentina inaiunga mkono kwa dhati Taifa la Israel katika kutetea mamlaka yake, hasa dhidi ya tawala zinazoendeleza ugaidi."

Pia, amesema hivi karibuni mahakama ya Argentina iliitaja Iran kuhusika na mashambulizi ya bomu kwenye ubalozi wa Israel na kituo cha jumuiya ya Wayahudi, huko Buenos Aires lililotokea kwenye miaka ya 1990.

Brazil

Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil imetoa imesema inafuatia ‘kwa wasiwasi mkubwa’ habari kwamba ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran yalitumwa Israel.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa Brazil imekuwa ikiionya jumuiya ya kimataifa, tangu kuanza kwa vita dhidi ya Gaza kwamba mzozo huo unaweza kuenea katika eneo lote.

Canada

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amewaambia waandishi wa habari mjini Ottawa kwamba nchi yake "inalaani bila shaka mashambulizi ya anga ya Iran", na kuongeza: "Tunasimama na Israel."

Taarifa hiyo imesema baada ya kuunga mkono shambulio la kikatili la Hamas la Oktoba 7, 2023, hatua za hivi punde za utawala wa Iran zitazidi kuyumbisha eneo hilo na kufanya amani ya kudumu kuwa ngumu zaidi.

China

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China amesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake kwamba, China ina wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka mapigano baada ya mashambulizi ya Iran.

"China inatoa wito kwa pande husika kuwa watulivu na kujizuia ili kuepuka kuongezeka kwa mivutano. Mvutano huu ni kutokana na mzozo wa Gaza," imesema taarifa hiyo

Misri

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeonyesha "wasiwasi wake mkubwa" katika kuongezeka kwa uhasama na kutoa wito wa kuzuia uhasama huo wa kiwango cha juu.

Taarifa yake pia ilionya juu ya hatari ya kupanuka kwa mzozo wa kikanda, na kuongeza kuwa Misri itawasiliana moja kwa moja na pande zote kwenye mzozo kujaribu kudhibiti hali hiyo.

Umoja wa Ulaya

"EU inalaani vikali shambulio lisilokubalika la Irani dhidi ya Israeli," mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU), Josep Borrell amesema katika chapisho lake kwenye X.

"Hili ni ongezeko lisilo na kifani na tishio kubwa kwa usalama wa kikanda.”

Ufaransa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Stephane Sejourne amesema Iran inachukua hatua mpya ya kudhoofisha na kuongeza hatari ya kijeshi.

Ujerumani

"Tunalaani vikali shambulio linaloendelea, ambalo linaweza kutumbukiza eneo zima katika machafuko. Iran na washirika wake lazima wakomeshe hili mara moja," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock na kuongeza kuwa watashikamana na Israel kwa wakati huu.

Jordan

Waziri Mkuu wa Jordan, Bisher Khasawneh amesema ongezeko lolote la mapigano katika eneo hilo litasababisha hatari zaidi, na kwamba kuna haja ya kupunguza kuongezeka kwa mzozo kwa pande zote.

Katika hotuba yake kwa baraza la mawaziri, Khasawneh amesema vikosi vya jeshi vya nchi hiyo vitakabiliana na jaribio lolote la chama chochote kinachotaka kuhatarisha usalama wa nchi hiyo.

Qatar

Taifa hilo la Ghuba limetoa wito kwa pande zote husika kusitisha ongezeko la mapigano na wamezitaka pande hizo kujizuia kuendeleza mashambulizi.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema;  "ina wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea machafuko katika kanda.

"Tunawaomba wahusika wote kusitisha kuongezeka mapigano, waendeleze utulivu na kujizuia.”

Urusi

Serikali ya Urusi imesema inasikitishwa na mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel na kuzitaka pande zote kujizuia.

"Tunaelezea wasiwasi wetu uliokithiri juu ya kuongezeka kwa hatari nyingine katika eneo hilo," imesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi katika taarifa yake kuhusu mashambulizi ya Iran.

"Tunatoa wito kwa pande zote zinazohusika kujizuia.

"Tumeonya mara kwa mara kwamba migogoro mingi ambayo haijatatuliwa katika Mashariki ya Kati, haswa katika eneo la mzozo wa Palestina na Israel ambayo mara nyingi huchochewa na vitendo vya uchochezi visivyowajibika, itasababisha kuongezeka kwa mvutano zaidi," imesema taarifa hiyo.

Saudi Arabia

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imeeleza wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mapigano ya kijeshi, na kutoa wito kwa wahusika wote kujizuia na kuliepusha eneo hilo na watu wake kuingia kwenye hatari za vita.

Taarifa ya Saudi Arabia imeendelea kuhimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua jukumu lake la kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Hispania

Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez ametoa wito kwa kuzitaka pande zote kujizuia na mapigano zaidi.

Sanchez amesema hayo kwenye akaunti yake ya X kwamba: "Tunafuatilia kwa hofu mabadiliko ya hali ya Mashariki ya Kati. Lazima kwa gharama yoyote iepukwe kuongezeka kwa mapigano kwenye kanda huo.”

Uingereza

Waziri Mkuu wa Ungereza, Rishi Sunak ameita shambulio la Iran kama "uzembe".

"Iran kwa mara nyingine tena imeonyesha kuwa ina nia ya kupandikiza machafuko," amesema Sunak kwenye akaunti yake ya X.

"Uingereza itaendelea kutetea usalama wa Israel na ule wa washirika wetu wote wa kikanda, ikiwa ni pamoja na Jordan na Iraq," amesema.

Umoja wa Mataifa

"Ninalaani vikali ongezeko kubwa linalowakilishwa na shambulio kubwa dhidi ya Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jioni hii," amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa yake.

"Nina wasiwasi sana kuhusu hatari ya kuongezeka kwa uharibifu katika eneo zima. Ninaomba pande zote zijizuie kwa kiwango cha juu zaidi, ili kuepuka hatua yoyote ambayo inaweza kusababisha makabiliano makubwa ya kijeshi katika nyanja nyingi za Mashariki ya Kati,” amesema.

Marekani

Rais Joe Biden wa Marekani amelaani mashambulizi ya Iran na kuahidi jibu lililoratibiwa la kidiplomasia litakalotoka kwenye mkutano wa kundi la G-7.

Amesema Marekani imeisaidia Israel kuangusha makombora na ndege zisizo na rubani karibu zote.

Biden amesema katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House kwamba amesisitiza uungwaji mkono wa Marekani kwa usalama wa Israel katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

"Nilimwambia kuwa Israel ilionyesha uwezo wa ajabu wa kujilinda na kushindwa hata mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa  na kutuma ujumbe wa wazi kwa maadui wake kwamba hawawezi kutishia usalama wa Israel," amesema.

"Kesho (Jumapili), nitawakutanisha viongozi wenzangu wa G-7 ili kuratibu jibu la kidiplomasia kwa mashambulizi ya Iran," amesema.

Imeandaliwa na Noor Shija kwa msaada wa mashirika ya habari.