Iran yaishambulia Israel kwa makombora

Muktasari:

  •  Rais Joe Biden wa Marekani amebainisha vikosi vya Marekani vimeisaidia Israel kudungua ndege zisizo na rubani na makombora yaliyorushwa usiku wa kuamkia leo

Tehran. Makombora zaidi ya 300 yamerushwa Israel usiku wa kuamkia leo Jumapili, Aprili 14, 2024 ikiwa ni hatua ya Iran kulipiza kisasi baada ya kuuawa kwa makamanda wake katika shambulio la ubalozi wake uliopo mjini Damascus lililodaiwa kutekelezwa na Israel mwanzoni mwa mwezi huu.

AFP inasema kulikuwa na utitiri wa ndege zisizo na rubani na makombora usiku kucha shambulio linalotajwa halijawahi kushuhudiwa japokuwa bado haijaelezwa ni madhara gani yaliyotokea hadi sasa. 

Maelfu ya watu  wakipeperusha bendera za Iran na Palestina wakiwa wamekusanyika mjini Tehran alfajiri ya leo Aprili 14, 2024, wakiunga mkono baada ya Iran kushambulia Israel kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora. Picha na AFP

"Jana usiku Iran ilirusha zaidi ya makombora 300 ya balestiki, UAV na makombora ya kusafiri kuja Israel," amesema msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari.

Pia, Jeshi la Iran leo Jumapili limesema mashambulio yake ya ndege zisizo na rubani na makombora yamekuja ili kulipiza kisasi juu ya shambulio katika ubalozi wake mdogo wa Damascus, na hilo limefanikisha malengo yake yote.

"Operesheni Honest Promise imekamilishwa kwa mafanikio kuanzia jana usiku hadi leo asubuhi na kufikia malengo yake yote," Mohammad Bagheri, mkuu wa majeshi ya Iran amebainisha.

 Rais Joe Biden wa Marekani amebainisha vikosi vya Marekani vimeisaidia Israel kudungua ndege zisizo na rubani na makombora yaliyorushwa usiku wa kuamkia leo.

Wakati mashambulizi hayo yakiendelea nchi za jirani za Iraq, Jordan na Lebanon ziliamua kufunga anga zake kutokana na hatari ya kiusalama kabla ya kuzifungua tena mapema leo asubuhi.

Wakati huo huo, kundi la wanamgambo lenye makao yake nchini Lebanon la Hezbollah limesema limerusha safu mpya ya roketi kuelekea eneo la Golan Heights linalokaliwa na Israel, saa chache baada ya kujiunga katika shambulio hilo la Iran.

 Hezbollah inayoungwa mkono na Iran, ambayo mara kwa mara imekuwa ikishambuliana na Israel tangu kuanza kwa vita vinavyoendelea huko Gaza, ilisema katika taarifa yake kwamba imerusha roketi kadhaa katika vituo vitatu vya kijeshi vya Israel huko Golan.

Hata hivyo, Israel na Iran zimekuwa kwenye mapigano kwa miezi sita dhidi ya wapiganaji wa Hamas katika ukanda wa Gaza. Vita hivyo vilizuka baada ya Hamas kutekeleza shambulio la kuvuka mpaka Oktoba 7 mwaka jana na kuua watu zaidi ya 1200 nchini Israel na kuwateka nyara wengine 250.

Hadi sasa mashambulizi ya Israel huko Gaza yamesababisha uharibifu mkubwa na kuua zaidi ya watu 33,000, kwa mujibu wa maofisa wa afya wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, kundi la Hamas kutoka Palestina limesema mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel ya usiku wa kuamkia leo ni haki yake ya asili.

Tovuti ya Times of Israel imeandika kwamba Iran imeionya Israel dhidi ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi hayo.

Imesema pia itashambulia kambi za Marekani ikiwa itaunga mkono kulipizwa kwa kisasi.

"Tutashambulia kwa ukubwa zaidi ya usiku wa kuamkia leo ikiwa Israeli italipiza kisasi dhidi yetu," amesema Mkuu wa Majeshi Meja Jenerali Mohammad Bagheri.

(Imeandikwa na Sute Kamwelwe)