Viongozi 24 washiriki mazishi ya Rais wa Namibia

Gari maalumu la Jeshi la Namibia likiwa limebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob baada ya kuwasili katika uwanja wa michezo wa Uhuru Jijini Windhoek kwa ajili ya mazishi ya kitaifa leo, Februari 24, 2024.

Muktasari:

  • Shughuli ya kitaifa ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob imefanyika leo Jumamosi katika Uwanja wa Uhuru, Windhoek na utazikwa kesho, Jumapili. Alifariki dunia Februari 4, 2024 kwa maradhi ya saratani.

Dar es Salaam. Viongozi 24 wa mataifa mbalimbali wameshiriki shughuli ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob katika mazishi ya kitaifa yanayofanyika leo Jumamosi, Februari 24, 2024 mjini Windhoek huku alitarajiwa kuzikwa kesho Jumapili katika makaburi ya viongozi.

 Wengi wa marais waliohudhuria ibada maalumu ya kumuaga kiongozi huyo ni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye aliwasili nchini humo jana Ijumaa kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.

Baadhi ya marais wengine walioshiriki hafla hiyo ni Hakainde Hichilema (Zambia), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Lazarus Chakwera (Malawi), Felix Tshisekedi (DRC), Evariste Ndayishimiye (Burundi) na William Ruti (Kenya).

Wengine ni Joao Lourenco (Angola), Mokgweetsi Masisi (Botswana), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe),  Frank-Walter Steinmeir (Ujerumani), Sauli Niinisto (Finland), Salhe-Work Zewde (Ethiopia) na Sheikh Tamim Hamad Al Thani (Qatar).

Vilevile, marais wastaafu walioshiriki shughuli hiyo ni Sam Nujoma na Hifikepunye Pohamba (Namibia), Jakaya Kikwete (Tanzania), Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Joachim Chissano (Msumbiji) na Olusegun Obasanjo (Nigeria).


Geingob (82) alifariki dunia Februari 4, 2024 katika hospitali moja nchini humo wakati akipatiwa matibabu kwa maradhi ya saratani yanayotajwa kuwa chanzo cha kifo chake.


Kiongozi huyo aliyeshiriki harakati za kupigania ukombozi wa nchi hiyo kupitia chama cha Swapo, atazikwa kesho Jumapili, Februari 25, 2024 katika makaburi maalumu ya viongozi nchini humo, maarufu kama Heroes Acre."


Mwili wa Geingob uliwekwa katika viwanja vya Bunge la nchi hiyo tangu juzi kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za mwisho na shughuli hiyo ilimalizika jana katika Uwanja wa Uhuru, Windhoek, kabla ya kuanza kwa ibada ya mazishi ya kitaifa na wakuu wa nchi kupata nafasi ya kumuaga.


Rais wa Namibia, Nangolo Mbumba amewaongoza wakuu wa nchi pamoja na wawakilishi wa mataifa mengine katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Namibia na mataifa jirani.


Ibada maalumu ya mazishi ya kitaifa ilifanyika katika uwanja wa uhuru wenye uwezo wa kuchukua watu 25,000. Maelfu ya wananchi, watu mashuhuri na viongozi wa mataifa mbalimbali walihudhuria ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Lutheran nchini humo, Dk Zephania Kameeta.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Rais wa chama cha Swapo ambaye pia ni Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah amesema chama hicho kimempoteza kiongozi wao aliyejitoa maisha yake kuwatumikia wananchi wa Namibia.

Amesema kila Taifa lina shujaa wake aliyejaliwa kuwa kiongozi, kwa Namibia alisema Geingob alikuwa mmoja wa mashujaa wao aliyepigania ukombozi si tu wa Namibia, bali Afrika na dunia kwa ujumla.


"Swapo na nchi yetu imempoteza mwanamapinduzi, kiongozi na mwanamajumui wa Afrika aliyejitoa kwa ajili ya nchi yake. Alisimamia mageuzi ya kiuchumi na kujenga uchumi jumuishi kwa wananchi," alisema Nandi-Ndaitwah.

Wananchi wa Namibia wakiwa kwenye shughuli za mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob katika uwanja wa michezo wa Uhuru Jijini Windhoek, leo Februari 24, 2024.

Kwa upande wake, kiongozi wa upinzani rasmi bungeni, McHenry Venaani amwelezea Geingob kama kiongozi aliyekuwa na uwezo wa kujadiliana na kufikia mwafaka.


Amesema atakumbukwa kwa kuandika Katiba inayoliongoza Taifa hilo katika misingi ya haki na wakati wa uongozi wake alijitahidi kuisimamia kwa viwango vya juu. Amsema maisha ya kiongozi huyo yameandikwa kwenye kurasa za Namibia. 


"Geingob na mimi tumekuwa marafiki wakati nikiwa kijana mdogo, wakati huo nikiwa na miaka 26 nikiwa mnadhibu wa upinzani, yeye akiwa mnadhimu wa serikali bungeni. Alikuwa mtu mnayeweza mkatofautiana, lakini mkabaki marafiki," amesema Venaani.


Geingob ambaye amekuwa Rais wa Namibia tangu mwaka 2014, alitarajiwa kumalizia muda wake Novemba 2024, na tayari chama chake cha Swapo kilikuwa kimemchagua Netumbo Nandi-Ndaitwah kuwa mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.


Kwa mujibu wa Katiba ya Namibia, Rais anapofariki, makamu wake ndiyo anachukua madaraka. Hivyo, Nangolo Mbumba aliapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo muda mfupi baada ya kifo cha Geingob, naye akamteua Nandi-Ndaitwah kuwa makamu wake.


Mbumba ameahidi kulivusha Taifa hilo kwenye kipindi hiki cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi ujao na amesisitiza hatagombea kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024.


Geingob aliyezaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Namibia mwaka 1941, alikuwa Rais wa kwanza wa Namibia kutoka nje ya kabila la Ovambo ambalo ni zaidi ya nusu ya watu katika nchi hiyo.


Alianza harakati dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini ambayo wakati huo ilitawala Namibia, tangu miaka yake ya awali ya shule kabla ya kufukuzwa uhamishoni.


Alikaa karibu miongo mitatu nchini Botswana na Marekani, ukiacha ile ya zamani kwa muongo wa pili mwaka 1964.

Viongozi mbalimbali wa Jeshi la Namibia wakiwasili na jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob katika uwanja wa michezo wa Uhuru Jijini Windhoek, leo Februari 24, 2024.

iongozi huyo mrefu na mwenye sauti nzito, alisoma katika Chuo Kikuu cha Fordham huko New York, Marekani na baadaye alipata shahada ya uzamivu (PhD) nchini Uingereza.


Akiwa Marekani, aliendelea kuwa mtetezi mkubwa wa uhuru wa Namibia, akiwakilisha vuguvugu la ukombozi wa ndani (SWAPO), ambacho sasa ni chama tawala, katika Umoja wa Mataifa na kote Marekani.


Mapema miaka ya 1970, alianza kazi ya kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa juu ya masuala ya utawala.


Akionekana kama kiongozi mkuu, alirejea Namibia mwaka 1989, mwaka mmoja kabla ya uhuru wa nchi hiyo.


“Nilikumbatia ardhi ya Namibia baada ya miaka 27 uhamishoni. Nikikumbuka nyuma, safari ya kujenga Namibia mpya imekuwa ya manufaa,” alisema katika ukurasa wake wa X (Twitter) mwaka 2020 akiweka picha ya mdogo wake akibusu lami baada ya kutua nyumbani. .


Swapo iliposhinda uchaguzi wa kwanza mwaka wa 1990, Geingob aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, nafasi aliyoshikilia kwa miaka 12 kabla ya kurejea tena mwaka 2012.


Mwaka 2014, chama kiliposhinda uchaguzi mwingine, kikizingatia urithi wa jukumu lake katika mapambano ya ukombozi, Geingob akawa Rais.