Waziri Mkuu mstaafu, mkewe jela miaka 14 kwa ufisadi

Muktasari:

  • Hukumu ya kifungo cha miaka 14 kwa Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan imetolewa ndani ya saa 24 baada ya kuhukumiwa kifungo kingine cha miaka 10 kwa uvujaji wa siri za Serikali.

Islamabad, Pakistan. Waziri Mkuu mstaafu wa Pakistan, Imran Khan na mkewe wamehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi kwenye kesi iliyohusisha zawadi alizopokea akiwa madarakani, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti.

Hukumu hiyo iliyotolewa leo Jumatano Januari 31, imekuja siku moja a baada ya Khan kuhukumiwa kifungo kingine cha miaka 10 jela hapo jana, katika kesi inayohusiana na uvujaji wa siri za Serikali.

Haikufahamika mara moja, iwapo vifungo hivyo viwili vya Khan vinakwenda pamoja, kufuatia kesi iliyoendeshwa ndani ya jela hiyo ambapo amekuwa akizuiliwa kwa muda mrefu tangu kukamatwa kwake Agosti mwaka 2023.

"Ni siku nyingine ya kusikitisha katika historia ya mfumo wetu wa mahakama ambao unavunjwa," msemaji wa chama cha Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) aliviambia vyombo vya habari.

Haijabainika mara moja ikiwa hukumu za Khan zingetekelezwa kwa pamoja au kwa wakati mmoja kufuatia kesi iliyokuwa ikishikiliwa ndani ya jela hiyo ambapo amekuwa akizuiliwa kwa muda mrefu tangu kukamatwa kwake Agosti 2023.

Lakini Wakili wa Khan, Salman Safdar aliithibitishia AFP kuwa mteja wake alikuwa amehukumiwa pamoja na mkewe, Bushra Bibi ambaye bado hajakamatwa," Safdar alisema.

Wawili hao walioana mwaka wa 2018, miezi kadhaa kabla ya Khan kuchaguliwa kuwa waziri mkuu.

Bibi, mganga wa imani ambaye alikutana na Khan alipomwendea kupata mwongozo wa kiroho, ni nadra kuonekana hadharani.

Tangu kuondolewa madarakani mwaka wa 2022, Khan amekuwa anazongwa na kesi mahakamani, anazodai zimechochewa kumzuia asirudi madarakani baada ya kampeni ya kukaidi viongozi wa kijeshi wa Pakistan.

Khan alikuwa amelishutumu jeshi, ambalo alitawala nalo kwa ushirikiano kwa muda mrefu wa uongozi wake, kwa kupanga kumwondoa madarakani kwa njama zilizoungwa mkono na Marekani.

Khan alipokamatwa kwa mara ya kwanza Mei mwaka jana, ghasia zilizuka kote nchini.

Lakini mamlaka yake ya mtaani yalizimwa na ukandamizaji wa kijeshi ambao ulishuhudia maelfu ya wafuasi wakikamatwa, 100 kati yao wanakabiliwa na kesi za kijeshi na viongozi kadhaa waandamizi kulazimika kujificha.