Aga Khan Foundation kupanda miti milioni 50

Mkurugenzi wa AKF, David Siso, akishiriki shughuli ya upandaji miti aina ya mikoko wilayani Bagamoyo.

Muktasari:

 Miti milioni 50 inatarajiwa kupandwa maeneo mbalimbali nchini hadi kufikia mwaka 2030. Ni mkakati wa Taasisi ya Aga Khan Foundation (AKF) wa kulinda na kutunza mazingira.

Bagamoyo. Taasisi ya Aga Khan Foundation (AKF) imesema katika dhamira yake ya kulinda na kutunza mazingira inalenga kupanda miti milioni 50 hadi kufikia mwaka 2030.

Akizungumza baada ya kupanda mikoko zaidi ya 60,000 katika fukwe za kata ya Kisutu wilayani Bagamoyo, hivi karibuni, Mkurugenzi wa AKF, David Siso amesema:

‘‘Leo tumepada mikoko zaidi ya 60,000 kwa ujumla mwaka huu tumepanda mikoko zaidi ya 120,000, juhudi hizi ni kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo ni changamoto ya ulimwengu, mpango wetu ulianza mwaka 2022 na mpaka sasa tumeshapanda miti zaidi ya milioni nane,’’ amesema Siso.

Amesema katika mpango huo tayari miti zaidi ya 450,000 ya mikoko imepandwa na lengo la sasa ni kupanda walau mikoko 60,000 kwa mwezi.

"Mbali na kupanda mikoko piat tunatekeleza miradi ya misitu midogo katika shule mbalimbali, tayari shule 75 za manispaa ya Ubungo na Kindondoni zimenufaika na miradi hiyo na lengo ni kufanya zaidi,’’ alisema Siso.

Kwa upande wake, Ofisa Misitu Msaidizi Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Constantine Laswai amesema mpango wa AKF ni muhimu ikizingatiwa uhusiano uliopo kati ya binadamu na mazingira na hali ya uhalibifu inayoshuhudiwa sasa.

"Ni shughuli muhimu kwetu kwa kuwa binadamu yeyote anategemea mazingira. Miti imekuwa ikiharibiwa na ongezeko la watu lakini pia shughuli za kiuchumi, kulinda miti ambayo ni muhimu kwa mazingira kunaanza na kupanda miti hivyo kwetu hii ni hatua muhimu sana kwa kushirikiana na wenzetu wa Aga Khan," amesema.

Makamu Mwenyekiti wa kikundi cha ulinzi wa fukwe kata ya Kisutu, Siyasemi Salumu amesema tatizo katika ulinzi wa mikoko ni kukosekana kwa silaha kwa watu wanaoilindi ikiwa waharibifu wake wanakuwa nazo.

"Tunalinda mikoko lakini hatuna silaha hivyo tulija huku (ufukweni) huwa hatumudu ulinzi hususani tukikutana na watu wenye silaha kubwa," amesema Salumu.