Aga Khan kupanda miti milioni tatu Zanzibar

Wanafunzi wa Sekondari ya Mikindani Dole wakipanda miti shuleni hapo katika mradi wa upandaji miti milioni tatu inayotekelezwa na Taasisi ya Aga Khan leo. Picha na Zuleikha Fatawi
Unguja. Katika kukabiliana na chamgamoto ya mabadiliko ya tabianchi na kutekeleza kaulimbiu ya Zanzibar ya kijani, Taasisi ya Aga Khan (AKF) imeanzisha mradi wa upandaji miti shuleni na mjini kisiwani Zanzibar ambapo humo.
Akizungumza wakati wa kuzindua programu hiyo ya kupanda miti katika sekondari ya Mikindani Dole Unguja leo Oktoba 18, 2023 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk Omar Shajak amesema mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka 10 kwa kupanda miti milioni tatu italeta tija kubwa katika visiwa hivyo.
Mradi huo utatekelzwa kwa awamu mbili, kipindi cha miaka mitano kila awamu.
"Shabaha ya Serikali ni kuwa na Zanzibar ya kijani na yenye utulivu kwa kuwahamasisha wananchi kupanda miti ili kupata mazingira yatakayoweza kukabiliana na tabianchi,” amesema Dk Shajak.
Amesema ndani ya mradi huo kuna miradi miwili inayotekelezwa ambayo ni msingi wa mafunzo na mradi wa shule.
Aga Khan kwa kushirikiana na madrasa ya kuendeleza watoto Zanzibar imepanga programu ya kuanzisha na kusimamia miti shuleni Pemba na Unguja, walianza Pujini Pemba na Mikindani Dole Unguja.
Amesema lengo la mradi huo ni kuwapa elimu wanafunzi ya umuhimu wa kupanda na kuimarisha mazingira na unakwenda sambamba na Dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kidunia.
Mkurugenzi Mkazi AKF Tanzania, Atteeya Sumar alisema mabadiliko ya tabianchi ni changamoto za kidunia hivyo taasisi hiyo inajikita katika kupunguza changamoto hiyo kwa kutumia eneo dogo kupanda miti mingi.
"Naishukuru shule hii kukubali mradi huu kwani wanafunzi wataweza kujifunza masomo yao kwa vitendo, na mabadiliko haya yana athari kwa wanawake,” amesema Sumar
Meneja wa mradi huo Japhet Wange amesema katika mradi huo wanaangalia mambo makuu matatu ikiwemo kupanda misitu midogo maeneo ya mjini na shuleni ili kuimarisha masomo kwa wanafanzi.
Pia, upandaji wa mikoko ambapo anasaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi, mwisho kuweka maji ambapo watafanya kwa jumla ya shule 12.
"Turejeshe mazingira katika uhalisia kwani athari zake zinaongezeka ikiwemo kuongezeka kwa joto hivyo wananchi tujitahidi kupanda miti ili kupunguzaathari hizi,” amesema Wangwe.
Mwalimu Mkuu sekondari ya Mikindani Dole, Mshenga Haji Silima amesema wapo tayari kupokea mradi huo laki shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya maji hivyo kufika kwa mradi huo wanaamini kuwa wataondosha tatizo hilo.
Amesema shule hiyo ya sayansi na kilimo utaudhibiti mradi huo ili wanafunzi wengine wajifunze kupitia shule yao.