Bosi wa zamani arejeshwa Maabara ya Taifa

Dk Nyambura Moremi

Muktasari:

  •  Ni baada ya miaka minne tangu alipoondolewa, Dk Nyambura Moremi ni mtaalamu wa biolojia na mwanasayansi mbobezi wa vipimo vya maabara Tanzania.

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imemrejesha kwenye nafasi yake aliyekuwa Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL), Dk Nyambura Moremi aliyesimamishwa kazi Mei 4, 2020 kupisha uchunguzi.

Dk Moremi amerejeshwa ikiwa ni miaka minne, baada ya kuondolewa katika nafasi hiyo na Waziri wa Afya, baada ya Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli kutia shaka usahihi wa vipimo vya Maabara ya Taifa vilivyothibitisha kuwapo Uviko-19 katika sampuli za wanyama na mimea.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Englibert Kayombo, Dk Moremi ameteuliwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa maabara hiyo, Medard Beyanga.

“Kwa kipindi chote Dk Moremi alikuwa Mkuu wa Idara ya Tafiti katika Maabara Kuu ya Taifa,” amesema Kayombo.

Dk Moremi ni miongoni mwa wabobezi katika fani ya maabara na ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza.


Alivyoondolewa

Akizungumza wakati wa kumuapisha  Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Mei 3, 2020 Rais Magufuli alisema siku za karibuni zilitumwa sampuli zisizo za binadamu katika maabara hiyo kwa sir na kurudisha baadhi ya majibu yakionyesha uwepo wa maradhi ya Uviko-19 kwa wanyama, ndege na matunda.

"Sampuli kwa mfano iliyotoka kwenye gari, tuliipa jina la Jabir Hamza mwenye miaka 30, ile ilileta negative. Tulipopeleka sampuli ya fenesi, ambayo tuliipa jina la Sarah Samweli miaka 45, matokeo yake yalikuwa unconclusive. Tulipopeleka sample (sampuli) ya papai tukaipa jina Elizabeth Anne miaka 26 papai lile lilikuwa positive," alisema Dk Magufuli.

Alihitimisha kuwa matokeo ya vipimo vya uongo vya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa papai, ndege na mbuzi vilivyoandikwa sampuli za binadamu, yalithibitisha Maabara ya Taifa si ya kuaminika.

Akitilia shaka juu ya uaminifu wa vifaa vya maabara na wanasayansi NPHL, Dk Magufuli alikataa takwimu kuhusu janga la Uviko-19 akitaka uchunguzi ufanyike kwa kile alichotaja kuwa ‘mchezo mchafu’ katika Maabara Kuu ya Serikali.

"Vifaa au wafanyakazi wanaweza kutumika kwa hujuma," Dk Magufuli alisema katika hotuba yake, akisisitiza maombi na tiba mbadala pekee ndizo zingeilinda Tanzania dhidi ya janga hilo.

Siku moja baada ya kauli ya Dk Magufuli, Waziri wa Afya, alimwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwasimamisha kazi mara moja Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Jamii, Dk Nyambura Moremi na Meneja Udhibiti wa Ubora, Jacob Lusekelo ili kupisha uchunguzi.

Pia aliunda kamati ya watu 10 kuchunguza mwenendo wa maabara hiyo ya Taifa, iliyotakiwa kuwasilisha taarifa Mei 13, 2020.

Waziri Ummy aliyerudi tena katika Wizara ya Afya miaka miwili iliyopita baada ya kutumikia Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kipindi kifupi, amemrejesha Dk Moremi katika nafasi yake ya awali.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Sakata la Uviko19

Wakati dunia ikipambana na Uviko-19, Dk Magufuli mara kadhaa alitamka hadharani kuwa Serikali yake inapigana vita ya uchumi na majeshi ya kibeberu ya kigeni ambayo yamedhamiria kuhujumu maendeleo ya nchi.

Alikuwa na shaka na misaada ya kigeni zikiwemo barakoa, akidai zinaweza kuchafuliwa makusudi na virusi vya Uviko-19 ili kuingiza janga hilo nchini.

Mbali na kukataa vipimo vya maabara, pia alitupilia mbali chanjo, uvaaji wa barakoa, utolewaji wa takwimu na kuondoa njia zote za kujikinga.