Ileje wajipanga kupambana na udumavu wa watoto

Mkuu wa Wilaya Ileje Farida Mgomi akipata maelekezo kutoka kwa muelimishaji lishe ngazi ya Kijiji cha Kabale aina ya vyakula vinavyotakiwa kwa watoto. Picha na Denis Sinkonde
Muktasari:
Ofisa Lishe wa Wilaya ya Ileje, Ester Mshana amesema hayo leo Aprili 4, 2024 katika Maadhimisho ya Wiki ya Lishe na Afya yaliyokwenda sambamba mafunzo ya kupika aina ya vyakula wanavyotakiwa kula watoto
Songwe. Baada ya kubainika kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto wanaoishi na udumavu wilayani Ileje Mkoa wa Songwe, Serikali imejipanga kutoa elimu kijiji kwa kijiji kuhusu aina ya vyakula wanavyotakiwa kulishwa.
Hatua hiyo imekuja baada yakubainika watoto 7,018 chini ya miaka mitano, wana udumavu unaosababishwa na kutokula mlo kamili.
Ofisa Lishe wa Wilaya ya Ileje, Ester Mshana amesema hayo leo Aprili 4, 2024 katika Maadhimisho ya Wiki ya Lishe na Afya yaliyokwenda sambamba mafunzo ya kupika aina ya vyakula wanavyotakiwa kula watoto.
Mshana amesema wamejipanga kutoa elimu kwa vitendo kwa wanawake na wanaume kuhusu aina za vyakula rafiki kwa watoto na namna ya kupika ili kufanikisha lengo la kupunguza udumavu hadi shuleni.
“Tunatarajia elimu tutakayoitoa kwa wananchi wa Ileje itapunguza tatizo la udumavu kutoka asilimia 31.9 mpaka asilimia 20 kufikia mwaka ujao wa fedha kwa kuwa tumeiweka kama ajenda ya kimkakati,” amesema Mshana.
Mshana amesema mpaka sasa wamezifikia kata zote 18 za Ileje na kuweka mkazo wa elimu waliyoitoa kwa vitendo hivyo.
Amezitaja kata ambazo watoto wa chini ya miaka mitano wana udumavu kwa wingi ni Bupigu, Isongole, Luswisi na Ngulilo.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi amesema licha ya wilaya hiyo kuwa na aina mbalimbali za vyakula, bado udumavu ni tishio, hivyo kampeni hiyo ambayo ipo kisheria atahakikisha anaisimamia kwa kushirikiana na wataalamu wa lishe ili kusaidia watoto kuondokana na udumavu.
“Jitihada za kupambana na udumavu zinakwamishwa na baadhi ya wanawake ambao badala yakuwapa vyakula rafiki wanawanywesha pombe za kienyeji na kwenda nao virabuni, atakayebainika sheria itashughulika nao,” amesema Mgomi.
Mkazi wa Kijiji cha Kalembo wilayani humo, Magidalena Mtambo amesema elimu hiyo iwe endelevu na itungwe sheria kali itakayowabana wazazi watakaobainika kwenda na watoto virabuni na kuwanywesha pombe ikiwamo kufungwa jela miezi sita.
Japheti Simbeye amesema ili kukabiliana na udumavu, wanaume pia wanatakiwa kufuatilia maendeleo ya makuzi ya watoto wao sambamba na utoaji wa fedha za matumizi ya kununulia vyakula ambavyo watoto wanatakiwa kula ili kuimarisha afya zao.