Sababu watumishi wa afya kuzuiwa kutumia simu kazini

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu akizungumza katika mahafali ya kitaaluma ya 10 ya kutunuku vyeti vya usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga.


Muktasari:

 Waganga wafawidhi katika hospitali zote wameagizwa kuhakikisha wanasimamia jambo hilo na kwamba, linawezekana iwapo litasimamiwa vizuri

Dodoma. Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu ametaja sababu mbili za kupiga marufuku matumizi ya simu kwa watumishi wa afya wakati wakifanya kazi.

Amesema katazo hilo linalenga kuzuia maambukizi na kutoa huduma bora.

Bila kueleza sababu, Profesa Nagu alitoa katazo hilo  Januari 26, 2024 alipozungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure mkoani Mwanza akiwa ziarani kukagua mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.

Akizungumza leo Februari 23, 2024 katika mahafali ya kitaaluma ya 10 ya kutunuku vyeti vya usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga waliofaulu mitihani ya usajili na leseni, Profesa Nagu amesema wengi wametoa visingizio kuwa wanatumia simu kutuma taarifa na kufanya rejea.

“Naomba niwakumbushe kuwa mazingira ya hospitali ni ya infection (maambukizi). Namna moja ya kujikinga na kudhibiti magonjwa ni kunawa mikono lakini simu mara umeweka kwenye kitanda cha mgonjwa, mara umeweka mahali fulani unabeba kila aina ya vimelea,” amesema.

Amesema matumizi ya simu wakati wa kutoa huduma ni njia ya kupeleka maambukizi kutoka kwa mgonjwa mmoja kwenda kwa mwingine lakini pia kwa mtumishi.

Profesa Nagu amewaagiza waganga wafawidhi katika hospitali zote kuhakikisha wanasimamia jambo hilo na kwamba, linawezekana iwapo litasimamiwa vizuri.

Amewataka kuweka utaratibu wa kuitana wakati wa dharura na kutumia simu binafsi kuepusha visingizio vya kuwa wanatumia simu kuitana ikitokea dharura.

Profesa Nagu amesema hilo litawezesha pia watumishi walio na dharura za kifamilia kujulikana wanafikiwaje wanapowahudumia wagonjwa.

Amesema malalamiko mengine ni kuhusu lugha zinazotumika kwa wateja kuwa hazijali umri, utu na staha.

Amesema mengine ni muda wa kukaa kwenye vituo vya afya na huduma zisizo na staha kwa baadhi ya watu kuhudumiwa bila ya usiri kama miongozo ya afya inavyotaka.

Profesa Nagu amesema malalamiko mengine ni kelele katika hospitali ambazo husababishwa na baadhi ya watumishi kuongea kwa sauti kubwa, hivyo kuondoa utulivu.

Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga katika Wizara ya Afya, Ziada Sellah amewataka wauguzi na wakunga kuhakikisha wanakuwa na muonekano wa staha kwenye mavazi, viatu, nywele na kucha.

Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Profesa Lilian Mselle ametaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uwepo wa malalamiko ya ukiukwaji wa maadili kwa baadhi yao, uelewa mdogo juu ya sheria inayosimamia kada hiyo, mawasiliano hafifu kati ya wagonjwa na watoa huduma na mabadiliko ya miundo ya kiutumishi.

“Changamoto nyingine ni baadhi ya wahitimu kumaliza vyuo wakiwa hawana weledi wa kutosha na kushindwa kufikia viwango vya utoaji huduma,” amesema.

Amesema ili kuboresha huduma za afya, ofisi yake iliona ni vyema kutengeneza moduli itakayosaidia kuhakikisha wauguzi wanaofanya kazi katika vyumba vya upasuaji wanakuwa na umahiri unaohitajika. Amesema wauguzi 362 wamefikiwa na wamenufaika.

Katika mitihani iliyofanyika Desemba 29, 2023 jumla ya watahiniwa 2,043 sawa na asilimia 49.3 kati ya 4,142 waliofanya mitihani ya usajili na leseni walifeli.

TNMC imewasajili na kuwapa leseni wauguzi na wakunga 2,999 baada ya kufaulu mitihani hiyo, hivyo kufanya jumla wauguzi na wakunga waliosajiliwa kufikia 52,093.