Sababu za Mchungaji Kimaro kupewa likizo KKKT Kijitonyama

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama, Eliona Kimaro.

Dar es Salaam. Wakati waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama wakiendelea kushinikiza kurejeshwa Mchungaji Eliona Kimaro, imebanika mchungaji huyo kutoa lugha zenye utata zinazokinzana na maadili ya dhehebu lake kuwa miongoni mwa sababu za kupewa likizo ya siku 60 inayopingwa.

Januari 16, Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) ilimpa likizo ya siku 60 mchungaji huyo huku ikimtaka kuripoti makao makuu pindi likizo yake itakapomalizika, jambo lililoibua sintofahamu kwa waumini wa usharika huo.

Chanzo kutoka ndani ya dayosisi hiyo kimetueleza kuwa likizo aliyopewa Mchungaji Kimaro si ya kwanza na imekuwa ikitolewa kwa watumishi wengi wa kanisa hilo ambao hubainika kukiuka maadili.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa wapo ambao wamekuwa wakipewa adhabu kubwa zaidi ya aliyopewa mchungaji huyo kutokana na makosa yao kupisha uchunguzi.

“Hii likizo ya siku 60 ni halali na iko kisheria kwa sababu kuna kanuni inayoruhusu hilo, hilo halina shaka,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilifafanua kuwa likizo ya aina hiyo mara nyingi hutolewa kwa wachungaji waliokiuka maadili au kuonyesha utovu wa nidhamu. “Hili huwa linajadiliwa kwenye vikao vya viongozi wa kanisa, hakuna mlei yeyote anayeshiriki na uamuzi ukitolewa huwa wa kikao,” kilisema.

Hata hivyo, taarifa zaidi zinasema watumishi hurudishwa makao makuu kufanyiwa tathmini na wapo ambao baadaye huhamishwa usharika au kusimamishwa kutoa huduma.

“Kwa utaratibu, mchungaji anaajiriwa na dayosisi. Kanisani zipo ajira za aina mbili, moja ni hiyo ya watumishi wa madhabahuni na wapo walei, taratibu za kazi zikikiukwa lazima hatua zichukuliwe, haijalishi ni mchungaji au ni mlei,” kilisema chanzo kingine.

Mchungaji Kimaro alipokabidhiwa barua ya likizo ya siku 60, chanzo hicho kilisema tayari alikuwa amekiuka baadhi ya maadili wakati akihubiri kwenye mikutano yake huko nyuma.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa ngazi za chini wa kanisa hilo waliozungumza na Mwananchi jana walisema hata kama Dk Kimaro amekosea, kumpa likizo ndefu ni kuwanyima haki waumini.

“Tulitarajia dayosisi wangetoa taarifa nini kimekosewa na Mchungaji Kimaro kusudi waumini wajue, haya ndiyo malalamiko makubwa ya waumini wa usharika huu,” alisema mmoja wao.

Mwingine alisema kanisa linahubiri kusamehe “sasa kama huyu wameona amekosea, si wangemsamehe badala ya kuendelea kuleta taharuki huku usharikani?”

Hata kama adhabu ipo kikanuni, walitaka ifike wakati uongozi uitafakari hiyo kanuni kwani “kuna mambo uongozi wa juu hauwezi kuingilia, tunashuhudia migogoro katika dayosisi ikizidi kuongezeka na hii inatukumbusha haja ya kuirekebisha katiba yetu ili askofu mkuu aweze kuingilia mambo na kufanyia uamuzi migogoro hii.”

Juhudi za kumtafuta Mchungaji Kimaro ziligonga mwamba baada ya simu yake kutopokelewa.


Waumini wapungua

Kwenye misa ya asubuhi jana, idadi ya waumini ilikuwa ndogo tofauti na ilivyozoeleka. Mwananchi lilifika kanisani hapo saa 12:25 asubuhi na kukuta ibada ikiendelea, liliwashuhudia baadhi ya viongozi wakiwa lango kuu wakimhoji kila muumini anayeingia.

Viongozi hao walitaka kujua muumini anatoka jumuiya ipi pamoja na namba ya bahasha ya ahadi (inayotumika kutolea sadaka na waumini wa KKKT).

Alipotafutwa Kaimu Mchungaji wa KKKT Kijitonyama, Anna Kuyonga kupata ufafanuzi wa utaratibu huo mpya, alisema unalenga kuimarisha usalama.

“Ni utaratibu tu wa kuhakikisha ibada inafanyika kwa utulivu na kama ninyi ni waandishi wa habari, mlipaswa kujitambulisha kwa kutoa taarifa ili hatua zote zifuatwe na kilichokuwa kinafanyika kwa ibada ya asubuhi hatuhitaji au haikuwa inahitaji kurekodiwa,” alisema.

Mchungaji huyo alisema hakuna muumini aliyezuiwa kuingia kanisani. “Hata jana (juzi) walikuja waandishi wa habari na niliwaeleza mimi si msemaji na leo tulisema hatutaki vyombo vya habari mpaka wapige simu au watoe taarifa wanataka nini,” alisema Anna.

Wakati mchungaji akisema hayo, muumini aliyejitambulisha kwa jina la Hellen Minja alisema ibada ya asubuhi ni ya watu kutoka maeneo tofauti hasa waendao kazini.

“Sasa ukianza kuuliza masuala ya jumuiya na bahasha si sawa, wawaache watu wasali waendelee na shughuli zao,” alisema Hellen.


Imeandikwa na Herieth Makwetta, Fortune Francis na Victor Tullo.