Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau watoa misimamo tofauti shule za bweni

Wanafuzi wa shule ya sekondari ya St Anne Marie Academy wakiwa na mabegi yao  baada ya kufungwa kwa shule wakirudi nyumbani.Picha Maktaba

Muktasari:

  • Wadau wa elimu wamekuwa na mitizamo tofauti na msimamo wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), kuzuia uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za kutwa kwenda za bweni.

Dar es Salaam. Wadau wa elimu wamekuwa na mitizamo tofauti na msimamo wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), kuzuia uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za kutwa kwenda za bweni.

Juzi Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe alisema hakutakuwa na uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa shule za kutwa kwenda kwenye shule za bweni, akisema upangaji wa wanafunzi umefuata vigezo na taratibu zilizowekwa.

Kwa mujibu wa Profesa Shemdoe, tangu Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki atoe taarifa ya kuwapangia shule wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023, kumekuwa na maombi kutoka kwa wazazi au walezi wanaotaka watoto wao kuhamia kwenye shule za bweni.

Profesa Shemdoe alisema miongoni mwa sababu wanazozitaja wazazi hao katika maombi hayo ni ugonjwa au matamanio ya wazazi au watoto.

Akizungumzia msimamo huo, mdau wa elimu, Dk Aviti Mushi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema si sahihi kuweka msimamo huo na sio wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule hizo za bweni watakwenda huko.

Alifafanua kuwa, awali shule za bweni zilitoa fursa kwa wanafunzi kuifahamu Tanzania, lakini uzuiaji huu hautakuwa na tija kwa Taifa na elimu kwa ujumla.

Alisema kufanya hivyo kunakwenda kuzuia uhamilishaji na uboreshaji wa maarifa.

“Uzuiaji huu utapoteza nafasi ya mwanafunzi wa Kitanzania kujua makabila mengine yanayoishi mikoa tofauti na anapoishi na kukosa fursa za kujifunza umoja wetu wa Kitanzania ulivyoundwa kwa kuchangamana makabila mbalimbali huko shuleni,” alisema Dk Mushi.

Alisema Tanzania ni kubwa yenye mazingira mbalimbali tofauti, inahitaji watu wenye uelewa mpana wa mazingira hayo. Alisema wanafunzi wakiandaliwa vyema kwa kujua mazingira mbalimbali ya Tanzania, watakuja kuwa na tija katika siku za usoni kwenye utimizaji wa majukumu yao ya kitaifa.

“Nashauri Tamisemi kubadilisha uamuzi huu na kuwaacha wanafunzi wapelekwe shule ambazo wazazi wamezipenda kwa sababu zao. Mzazi ana nafasi kubwa ya kumuelewa mtoto wake na kujua akisoma wapi atafaidika zaidi,” alisema Dk Mushi.

Mdau mwingine, Emmanuel Mshana alisema kwa haraka uhitaji wa mabweni ni mkubwa kuliko yaliyopo, ndiyo maana hakuna changamoto kwa watu wanaopangwa katika maeneo hayo kuomba kurudishwa katika shule za kutwa.

“Lakini imekuwa changamoto kwa watu shule za kutwa kuhamia bweni, hii ni taswira inayoifanya Serikali kujua kuna changamoto ya watu au walezi kukosa watu wa kukaa nao na kutamani watoto wao kupelekwa shule za bweni.

“Wazazi wanapaswa kukubaliana na hali halisi kwa sababu mabweni yamejaa, lakini Serikali iweke mpango mkakati wa kuongeza shule za bweni maana mahitaji ni makubwa,” alisema Mshana, ambaye ni mmiliki wa shule za Bethel Mission.

Mhadhiri wa UDSM, Dk Faraja Kristomus alisema msimamo huo wa Serikali huenda umetokana na ushauri wa kitaalamu wa maofisa wa wizara.

Hata hivyo, alisema kuna haja ya kueleza vigezo vilivyotumika kupanga wanafunzi kwenye shule za bweni, akisema yapo madai kuwa wapo wanafunzi waliofaulu vizuri wamepangwa shule za kata.

“Sababu kubwa ya kupanga wanafunzi kwenye shule za kata kuliko za bweni ni shule nyingi za bweni kongwe nchini zimegeuzwa kidato cha tano na sita.

“Lakini pia tusisahau sera ya Serikali ni kuifanya elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne kuwa sehemu ya elimu msingi na msisitizo unawekwa kwa kidato cha tano na sita. Hivyo shule za bweni kwa kidato cha kwanza hadi cha nne zimekuwa chache na nafasi inatolewa kwa kidato cha tano na sita,” alisema.