14 mbaroni kufuatia vurugu za wakulima na wafugaji Lindi

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, akilieleza baraza la madiwani Halmashauri ya Lindi, juu ya vurugu za wakulima na wafugaji wilayani humo. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, amesema watu 14 wameshakamatwa, wakiwemo wakulima na wafugaji, kufuatia vurugu zilizotokea siku tatu zilizopita, ambapo inadaiwa mkulima kujeruhiwa sehemu za kichwani na mtu anayedaiwa kuwa ni mfugaji.
Lindi. Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, amesema watu 14 wameshakamatwa, wakiwemo wakulima na wafugaji, kufuatia vurugu zilizotokea siku tatu zilizopita, ambapo inadaiwa mkulima kujeruhiwa sehemu za kichwani na mtu anayedaiwa kuwa ni mfugaji.
Katika vurugu hizo, inadaiwa kuwa Mikidadi Nalinga (40), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mnyangara, Tarafa ya Mipingo, Manispaa ya Lindi, alijeruhiwa na kwamba anaendelea na matibabu hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani robo ya nne, kilichofanyika wilayani hapa, DC Ndemanga amesema Polisi wilayani humo inawashikilia kwa mahojiano watu hao na mara baada ya Upelelezi kukamilika, watafikishwa kwenye mamlaka husika, ili sheria ichukue mkondo wake.
“Kiukweli nimesikitishwa na kitendo kilichotokea, Lindi hatutaki kabisa yatoke mambo kama haya, wakulima na wafugaji, waishi kama ndugu,” amesema na kuongeza;
“Toka mwaka 2020, hatukuwahi kuwa na migogoro baina ya wakulima na wafugaji, makundi haya mawili waliishi vizuri; lakini tatizo hili limeanza hivi karibuni kutokana na mifugo mingi kuingia Lindi bila ya kuwa na utaratibu,” amesema.
Kwa upande mwingine, Ndemanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Wilaya ya Lindi, amewataka wafugaji walioingia wilayani humo bila ya kufuata utaratibu, warudi walipotoka kabla zoezi la kuwaondoa kwa lazima halijaanza.
“Ninawataka watu wa Lindi wasipokee mifugo ya watu wengine, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima...mifugo imejaa na hatuna uwezo wa kupokea mifugo mingine tena kwa Manispaa ya Lindi, na tutafanya zoezi la kuwatambua walioingia kihalali na kutoa vitambulisho kwa wafugaji hao, ambao ni watiifu na walioingia kinyemela waondoke." Amesema na kuongeza;
"Lakini pia, niwaombe wananchi wa Lindi, waache tabia ya kujichukulia sheria mkononi, jeshi lipo linafanya kazi yake.”
Akizungumzia tukio la kupigwa kwa mkulima, Naibu Meya Manispaa ya Lindi, Salumu Ng'ondo, amesema tukio hilo limetokea Jumanne Agosti 15, 2023 ambapo mkulima huyo alipigwa na mfugaji maeneo ya kichwani, baada ya kutokea ugomvi kati yao.
"Mkulima alikuwa shambani kwake, na mfugaji akatokea na mifugo yake nakuiingiza shambani kwa mkulima, jambo hilo lilisababisha kuzuka ugomvi ambapo, mkulima alipigwa sana hasa maeneo ya kichwani, na kumsababishia majeraha makubwa, hadi sasa yupo Hosptali ya Muhimbili," amesema Naibu Meya huyo na kuongeza;
"Baada ya kutokea fujo hizo, wakulima nao wakakatakata mifugo, na kuchoma moto mabanda ya wafugaji," amesema meya huyo.