Acacia yawarejesha kazini walinzi wake 55

Muktasari:
> Ni baada ya Mkuu wa Wilaya kuingilia kati mgogoro huo
Kahama. Uongozi wa Kampuni ya Acacia inayomiliki mgodi wa Buzwagi umeridhia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhil Nkurlu la kuwarejesha kwenye huduma walinzi wake 55 ambao waligoma kusaini mkataba wa ajira mpya kutoka Kampuni ya Pangea Buzwagi kwenda G4S kama walivyotakiwa.
Msemaji wa kampuni hiyo, Nector Foya alisema mpaka sasa watumishi hao vitambulisho vyao vilivyokuwa vimefungwa sasa vimefunguliwa na wamo mgodini wakati wakisubiri kikao cha maridhiano kitakachofanyika Julai 10.
Juzi Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Nkurlu alifanya mazungumzo na pande zote mbili baada ya walinzi 28 kukwama ndani ya mgodi huo na wengine 27 nje baada ya vitambulisho vyao vya kutumia kuingia na kutoka kufutwa kwenye mtandao hali iliyofanya waliokuwa nje kubaki nje na waliokuwa ndani kubaki humo.
Kutokana na hali hiyo walinzi hao kupitia kiongozi wao, Shigela Aloyce walidai waliomo ndani wameshindwa kupata chakula na huduma zingine za kibinadamu kwa siku nne baada ya vitambulisho vyao kuondolewa kwenye mtandao.
Hata hivyo, baada ya Nkurlu kusikiliza malalamiko hayo aliagiza walinzi hao waendelee kutambuliwa kama wafanyakazi halali wa mgodi huo kwa kuwa kikao cha maridhiano bado hakijamaliza mazungumzo hivyo baada ya hapo ndipo maafikiano yatakamilika.
Kutokana na hali hiyo, Foya alisema wafanyakazi hao pamoja na kugoma wanapatiwa huduma zote za kibinadamu kama walivyo wafanyakazi wengine na hali ni shwari kwa sasa hakuna mgogoro wowote.
“Mgodi wa Buzwagi umejitoa kwenye shughuli za ulinzi umebinafsisha Kampuni ya G4S Security ambayo itafanya kazi hiyo na kipaumbele cha kwanza walipewa nafasi ya kuajiriwa walinzi ambao walikuwa kwenye Kampuni ya Pangea Buzwagi na katika hali hiyo wenzao 52 walikubali kusaini mkataba mpya na kuajiriwa G4S Security,” alisema Foya.
Pamoja na madai hayo, Aloyce alisema walinzi hao wamegoma kuajiriwa na Kampuni ya G4S kutokana na malipo kidogo ya mshahara na walipokuwa mshahara ulikuwa mkubwa pia kampuni ya Pangea Buzwagi ilifuta vitambulisho vyao kabla ya kumalizika kwa mazungumzo ya usuluhishi wa mgogoro uliokuwapo.