Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika yaweza kupunguza kukopa na ikapiga hatua

Tangu nchi za Afrika na nyinginezo duniani zilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni miaka ya 1960 na kuendelea, zilijikuta kwenye mzigo wa madeni kutoka kwenye nchi zilezile zilizowatawala.

Kwa sehemu kubwa, mikopo kwa nchi mbalimbali imekuwa ikitolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) na nchi wahisani, madeni ambayo yamegeuka mzigo mzito.

Mwaka 1996 uliandaliwa mpango IMF na WB kwa ajili ya kuzisaidia nchi 39 zilizoonekana kuwa na mzigo wa madeni yasiyolipika (HIPC), mataifa mengi ya Afrika, ikiwemo Tanzania, yalinufaika na mpango huo.

Mipango mingine iliyofanyika kupunguza mizigo ya madeni ni pamoja na ule wa kimataifa wa kupunguza deni (Multilateral Debt Relief Initiative) wa mwaka 2005 na mkakati wa kuondoa madeni kupitia mapambano ya Uviko-19 (DSSI).

Vilevile ulikuwepo mpango wa Special Drawing Rights uliotoa dola 6.6 bilioni ambao uliwezesha Afrika kupata asilimia 5; pamoja na mpango wa mataifa tajiri, G20 uliozinufaisha Zambia, Chad, Ethiopia na Ghana, yote ililenga kupunguza mzigo wa madeni kwa nchi masikini.

Hata hivyo, pamoja na mipango hiyo yote, bado nchi nyingi za Afrika zimeendelea kuelemewa na madeni kama ambavyo takwimu za IMF za mwaka 2022 zinaonyesha kuwa yanaongezeka wakati uwezo wa kuyalipa ukiwa chini.

Takwimu hizo zinaonyesha, madeni ya nchi hizo yamepanda kutoka dola 700 bilioni mwaka 2010 hadi kufikia zaidi ya dola 2,700 bilioni hadi mwaka 2023.

Wakati huohuo, pato la ndani la nchi hizo limeongezeka kutoka dola 250 bilioni mwaka 2010 hadi kufikia dola 1,700 bilioni ambalo halifikii hata madeni yenyewe; huku uwezekano wa kulipa sehemu ya madeni hayo ukiongezeka kutoka dola 200 mwaka 2010 hadi dola 500 bilioni mwaka 2023.


Hali tete

Kwa mujibu wa IMF, nchi za Afrika zilizo na hali mbaya zaidi kwa madeni ni Jamhuri ya Congo, Madagascar, Msumbiji, Malawi, Sao Tome and Principe, Somalia, Sudan, Zambia na Zimbabwe.

Nchi nyingine zenye hali tete ni Burundi, Cape Verde, Cameroun, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Comoro, Djibouti, Ethiopia, Gambia, Ghana, Mauritania, Guinea Bissau, Kenya, Sierra Leone, Sudan Kusini na Togo.

Nchi zilizo na hali ya wastani ni Benin, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ivory Coast, Guinea, Lesotho, Liberia, Madagascar, Mali, Niger, Rwanda, Tanzania na Uganda.

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wa waandishi wa habari kutoka nchi za Afrika ulioandaliwa na taasisi ya AFRODAD jijini Accra, Ghana, Meneja wa Sera, Uchechemuzi na Utafiti, Theophilus Jong anasema ifike wakati nchi za Afrika zigeukie rasilimali zake kujiendeleza kiuchumi.

“Mikopo inachukuliwa ili kufanyia shughuli za maendeleo, ikiwemo mipango ya maendeleo na maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), lakini nchi za Afrika zina njia mbadala badala ya kuendelea kukopa,” anasema.

Anaongeza: “Kuna kodi na mapato ya madini, kudhibiti utoroshwaji wa fedha nje ya nchi, ambapo inakadiriwa zaidi ya dola 88.8 bilioni hutoroshwa nje ya nchi kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD),” anasema.

Mratibu wa mtandao wa kupigania usawa Afrika (FIA), Njoki Njehu yeye anazikosoa taasisi za fedha, IMF na WB, akisema ni taasisi zenye sera za uliberali zilizosababisha kukosekana kwa usawa kati ya mataifa masikini.

“Mabadiliko yanayofanywa na IMF na WB yamegawa mataifa, huku yakipandikiza sera za kiliberali kupitia mifumo ya siasa za madeni.

“Kukua kwa masharti ya mikopo ni tishio kwa haki za kidemokrasia kwa nchi zinazodaiwa na kunyang’anywa uwezo wa kudhibiti rasilimali za nchi hizo,” anasema.

Kwa mujibu wa Njehu, mikopo inapoteza uhuru wa nchi za Afrika kwa kuwa madeni ndiyo yanayoziendesha nchi hizo katika uamuzi wa matumizi, vipaumbele na ufanyaji uamuzi.

“Serikali zinapangiwa jinsi ya kuwatumikia watu wake, kwa mfano, kabla hata ya Uviko-19, nchi zaidi ya 60 zilikuwa zikutumia fedha zake zaidi kulipa madeni kuliko huduma za afya.   

“Tunajua kwamba jamii zikiwa na usawa zitafaidi ubinadamu, lakini madeni yamesababisha kutokuwa na usawa, kuongezeka kwa rushwa, kuondoa uhuru wa habari, kukwaza ukuaji wa uchumi na ukuaji wa jamii, badala yake unakuza uhalifu na migogoro,” anasema.

Mkurugenzi wa taasisi ya Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), Hebron Mwakagenda anasema bado nchi za Afrika hazijawa na uwezo wa kulipa madeni, ndiyo maana zinapata changamoto katika ulipaji.

“Dhana ya madeni ipo duniani kote, hata Marekani inadaiwa na China. Tofauti yao na sisi ni kwamba ukifika muda wa kulipa wao wanalipa, lakini sisi tunaanza kulialia,” anasema.

Mwakagenda anaongeza kuwa nchi nyingi za Afrika hazina mifumo mizuri ya ukusanyaji wa kodi na hivyo fedha zinazotakiwa kulipa madeni zinapotea.