Aliyekuwa na jinsi mbili aondolewa ya kike Hospitali ya Temeke

Daktari bingwa wa upasuaji wa jumla na mfumo wa mkojo, Hussein Msuma (kulia) akiwa sambamba na Dk Hamis Mbarouk wakati wa upasuaji wa kurekebisha maumbile ya kijana mwenye umri wa miaka 22. Upasuaji huo umefanyika leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke. Picha na Mpiga picha wetu
Muktasari:
- Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke leo imefanikisha upasuaji wa kuondoa viungo vya kike kutoka kwenye korodani ya kushoto ya mgonjwa aliyekuwa na mwonekano wa jinsi ya kiume.
Dar es Salaam. Kutokana na kukua kwa teknolojia ya matibabu, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, imefanikiwa kufanya upasuaji wa kutoa viungo vya uzazi vya kike kutoka kwenye korodani ya mgonjwa aliyekuwa na jinsia mbili huku muonekano wake ukiwa wa kiume.
Mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 22 (jina linahifadhiwa), alifika hospitalini hapo akiwa na jinsi zote mbili na baada ya vipimo kukamilisha akafanyiwa upasuaji wa kuondoa jinsi ya kike.
Upasuaji huo uliofanyika leo Oktoba 3, 2023 umefanywa na jopo la madaktari kutoka hospitali hiyo, ambalo limeongozwa na Daktari Bingwa wa upasuaji wa jumla na mfumo wa mkojo, Hussein Msuma na Dk Hamis Mbarouk.
Dk Msuma ameshirikiana na Ofisa Muuguzi Mwandamizi na msimamizi wa upasuaji Curtius Mbalamula, Mtaalamu wa dawa za usingizi, Abraham Mkwati na muuguzi anayesimamia vifaa Shani Maupa.
Upasuaji huo siyo tu ni wa kwanza kufanyika katika hospitali hiyo, lakini pia unafanyika kwa mara ya kwanza katika hospitali za rufaa hapa nchini, ambapo awali upasuaji wa aina hiyo, umekuwa ukifanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pamoja na ile ya Benjamin Mkapa (BMH).
Akizungumza baada ya upasuaji kufanyika na kufanya vipimo vya sampuli zilizo tolewa katika upasuaji huo, Dk Msuma amesema mgonjwa alifika hospitalini akiwa na muonekano wa jinsia ya kiume, japo alikuwa na umbile la kike na kiume.
“Upasuaji tumefanya kwa mgonjwa aliyekuwa na muonekano wa nje wa jinsia ya kiume ila alikua na mifumo ya uzazi ya jinsia mbili, ya kiume kwenye korodani ya kulia na ya kike kwenye korodani ya kushoto,” amesema Dk Msuma na kuongeza;
“Kwa lugha ya kitaalamu huu upasuaji unaitwa ‘scrotal hystero-salpingo-oophorectomy’ na kwa lugha rahisi ni upasuaji wa kutoa viungo vya uzazi vya kike kutoka kwenye korodani ya mgonjwa wa jinsia mbili mwenye muonekano wa jinsia ya kiume...
“Ugonjwa huu unatokana na changamoto wa ukuaji wa kijinsia ‘ovotesticular DSD’ ambao ni ugonjwa nadra na adimu kutokea ambapo binadamu huzaliwa na viungo vya ndani vya uzazi ‘gonadi’ za jinsia zote yaani ovari za kike na korodani za kiume.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Vicent Kimaro amesema kufanyika kwa upasuaji huo katika hospitali ya rufaa ni kuelekea kutimiza malengo ya taifa kwani moja ya jitihada ya ni kuhakikisha hospitali zote zina uwezo wa kutoa matibabu ya kibingwa na bingwa bobezi.
Amesema huo ni mwendelezo wa upasuaji bingwa na bingwa bobezi katika hospitali hiyo, kwani hospitali hiyo pia ilifanikiwa kufanya upasuaji wa kutoa saratani ya figo bila kutoa figo pamoja na kutoa jiwe katika figo.
“Mafanikio haya yanatokana na uwepo wa madaktari bingwa na bingwa bobezi wenye utaalamu katika fani mbalimbali za afya katika hospitali hii,” amesema Dk Kimaro.