VIDEO: Miaka 62 ya mateso kwa wajawazito

Muktasari:

  •  Vuta hisia ya safari ndefu kwa pikipiki katika barabara mbovu ya vumbi, yenye milima, mabonde na mashimo.


Songwe. Vuta hisia ya safari ndefu kwa pikipiki katika barabara mbovu ya vumbi, yenye milima, mabonde na mashimo.

Hisia unayopata ndiyo wanayopitia wajawazito wanaokwenda kujifungua, wakisafiri umbali wa takribani kilomita 20 kufuata huduma kwenye kituo cha afya.

Tangu uhuru miaka 62 iliyopita, Kijiji cha Nsanzya wilayani Momba, mkoani Songwe hakijawahi kuwa na zahanati.

Wajawazito husafiri kwa pikipiki kwenda kujifungua katika Kituo cha Afya cha Kamsamba, kilichopo Kijiji cha Chilulumo, umbali wa takribani kilomita 20. Kwa mwendo wa mguu ni zaidi ya saa tatu kukifikia kituo hicho.

Si hayo tu, Mto Momba, wenye kina kirefu unaotenganisha vijiji vya Nsanzya na Chilulumo, ni changamoto nyingine, hasa wakati wa masika.

Hili ni kutokana na daraja la mbao ‘kiteputepu’ linalotumika kuunganisha vijiji hivyo kutopitika wakati huo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Calvin Mwasha anasema wana vituo vya afya vinne vinavyotoa huduma ya upasuaji, vitatu vikiwa vya Serikali, cha Kamsamba kikiwamo.

Anasema halmashauri hiyo yenye kata nne na vijiji 72, ina zahanati 43 pekee.

Ni kutokana na hayo, baadhi ya wajawazito katika kijiji cha Nsanzya hujifungulia nyumbani, wakisaidiwa na watu wasio wataalamu wa afya au njiani wakipelekwa kituo cha afya.

Licha ya changamoto wanazopitia, bado hutozwa faini ya Sh50,000 kwa kuchelewa kufika kituo cha afya, ambacho hakina uwezo wa kuwapokea wengi na kuwalaza ili kusubiri kujifungua.

Baadhi yao na hasa wenye shida ya uzazi pingamizi, wameishia kupoteza watoto waliofariki dunia ama kabla, wakati au baada ya kujifungua.

Uzazi pingamizi ni hali ya mjamzito kushindwa kuzaa kupitia njia ya kawaida, inayoweza kusababishwa na matatizo kwenye njia ya uzazi au mtoto mwenyewe.


Shuhuda za kina mama

Emelda na Rahel ni miongoni mwa kinamama waliopoteza watoto kutokana na changamoto za ukosefu wa zahanati na ubovu wa barabara kijijini hapo.

Emelda Dominic, aliyepoteza watoto wanne, anasema ubovu wa miundombinu na ukosefu wa zahanati kijijini hapo una mchango katika vifo vya wanawe.

Akibubujikwa machozi, anasema kuanzia ujauzito wa kwanza hadi wa nane, amekuwa akipitia changamoto na hasa anaposhikwa uchungu wa kujifungua.

Anasema watoto wawili walifariki dunia akiwa njiani kwenda kujifungua na wengine wawili kutokana na kuchelewa kuzaliwa.

Mtazamo wa Emelda ni kwamba, juhudi za Serikali kuhamasisha wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya afya, zinaweza zisifanikiwe kutokana na umbali mrefu kutoka yalipo makazi ya wananchi hadi vinapojengwa vituo vya afya.

Kwa upande wake, Rahel Siame, mkazi wa kijiji hicho, anasema watoto wake wawili wa kiume walifariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa kutokana na kufika hospitalini akiwa amechelewa.

Rahel, mama wa watoto wawili wa kike, anasema ndoto yake ya kupata watoto watano imefifia, kwa kuwa ana hofu ya kubeba ujauzito kutokana na changamoto ya miundombinu.

"Huwa nabeba ujauzito bila tatizo lolote, lakini changamoto hujitokeza wakati wa kujifungua. Umbali kutoka kwetu hadi Chilulumo tunatembea kwa miguu na wakati mwingine tunashindwa kupita kwenye daraja la mbao," anasema.

Anasema Oktoba 2018, alipoteza mtoto kwa kuwa ilimchukua saa zaidi ya mbili kutembea akiwa mjamzito kwenda Chilulumo. Anaeleza alipofika alijifungua na mtoto alikufa muda mfupi baada ya kujifungua.

"Nilipofika wauguzi walinipokea wakanisaidia, nilijifungua mtoto alitoka akalia mara moja tu, akafariki tukarudisha maiti nyumbani. Wauguzi waliniuliza kwa nini nimechelewa nikawaambia ni kwa sababu ya umbali,” anasema.

Kuhusu kifo cha mtoto wa pili, Rahel anasema alipatwa uchungu akashindwa kutembea, mume wake alimbeba kwa pikipiki hadi Kituo cha Afya Chilulumo.

Anaeleza baada ya kufika Chilulumo na kujifungua, mtoto alilia sana kisha akafariki, wauguzi wakamweleza kifo kilitokana na uzazi pingamizi.

Miaka 62 ya mateso kwa wajawazito

Kiongozi wa kijiji

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nsanzya, kilichopo Kata ya Kamsamba wilayani Momba, mkoani Songwe, Stanslaus Simchimba anasema katika miaka minne ya uongozi wake ameshuhudia vifo vya wanawake wawili kutokana na changamoto za uzazi.

Mbali na vifo hivyo, Simchimba anasema ameshuhudia vifo vya watoto zaidi ya 10, akitaja ukosefu wa zahanati kuwa unachangia vifo hivyo.

Anasema wajawazito kijijini hapo hulipa zaidi ya Sh5,000 kukodi pikipiki kwenda Chilulumo kujifungua na wanapojifungulia nyumbani au njiani, wanapofika kituo cha afya hutozwa faini ya Sh50,000.


Alichosema mganga mkuu

Akizungumzia changamoto hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Boniface Kasululu anasema miongoni mwa vyanzo vya vifo vya watoto ni uhaba wa wahudumu wa afya.

Dk Kasululu alisema takwimu zinaonyesha mwenendo wa vifo vya watoto wakati wa kujifungua hupanda na kushuka katika Halmashauri ya Momba.

Anasema mwaka 2021 kulikuwa na vifo vya watoto watano, vifo viwili mwaka 2022 na vitatu hadi Agosti, 2023.

Dk Kasululu alisema watoto waliofariki saa chache baada ya kuzaliwa mkoani Songwe mwaka 2021 walikuwa 49, watoto 16 mwaka 2022 na wanane (Januari hadi Agosti, 2023).

Anasema kwa kutambua ukubwa wa changamoto hiyo, ofisi yake iliwatambua madereva wa pikipiki 14 wilayani Momba wanaotumika kuwabeba wajawazito kuwapeleka zahanati na vituo vya afya inapotokea dharura ya kujifungua.

Dk Kasululu anasema pikipiki hizo huwa na mafuta wakati wote na kwamba, namba za simu za madereva huwekwa kwenye zahanati ili kurahisisha upatikanaji wao pindi huduma yao inapohitajika. Madereva hao wanapatikana kwenye kila kata.

Anataja sababu nyingine inayochangia vifo hivyo kuwa ni umbali mrefu kutoka makazi ya watu hadi vituo vilipojengwa na jamii kutokuwa na mwamko wa kujifungulia hospitalini, baadhi wakiamini kufanya hivyo ni kutengeneza mazingira ya kufanyiwa upasuaji.

Dk Kasululu anasema Halmashauri ya Wilaya ya Momba ina vituo 45 vya huduma ya uzazi salama.

Anasema kuna vituo vitatu vinavyotoa huduma ya upasuaji, ikiwamo hospitali ya wilaya ambayo inakamilisha ujenzi wa jengo la upasuaji.

Mganga mkuu anasema kwa kutambua jiografia ya Momba kutoka makao makuu ya halmashauri kwenda kituo kimoja cha afya ni zaidi ya kilomita 120, Serikali ilitoa Sh900 milioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na ujenzi wa jengo la afya ya mama na mtoto litakalokuwa na chumba cha upasuaji.

"Tunatarajia mwaka 2025 Halmashauri ya Momba itakuwa na vituo vitano vinavyotoa huduma ya upasuaji; halmashauri iko katika mazingira ya vijijini, maeneo mengine kutoka kijiji kilipo hadi huduma zinakopatikana ni zaidi ya kilomita tano," anasema.

Anasema kwa wastani wanawake 12 wilayani Momba hujifungulia nyumbani kila mwaka; wakisaidiwa na ndugu na wakunga, jambo linalochangia baadhi yao kufariki dunia kutokana na kuchelewa kufika hospitalini.

"Wanaojifungulia nyumbani, wengine huzalishwa na mama mkwe. Kuchukua uamuzi wa kujifungulia kituo cha afya ni mpaka wanapoona hali ya dharura," anasema.

"Tuna kundi sogozi la WhatsApp la watumishi wa afya. Tunawasihi ukipokea mjamzito aliye katika hatua mbaya toa taarifa kwa mganga mkuu wa halmashauri au mratibu wa huduma ya mama na mtoto ili afikishwe kituo cha afya haraka iwezekanavyo," anasema.


Matumizi ya pikipiki

Madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi waliohojiwa na Mwananchi wamezungumzia suala la wajawazito kupanda pikipiki.

Dk Godfrey Kaizilege wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, anasema matumizi ya pikipiki wakati wa ujauzito hayawezi kuchangia moja kwa moja kwenye changamoto za uzazi.

Alisema mjamzito anaweza kupatwa na changamoto ikiwa atachelewa kufika au kutojifungulia hospitalini.

Dk Kaizilege alisema wanawake wengi wanaopoteza watoto huonyesha dalili za uzazi pingamizi wakati wa ujauzito, hivyo kuchelewa kufika hospitalini ni jambo linaloweza kusababisha madhara kwake, mtoto au wote wawili.

"Changamoto za umbali zipo na zinajulikana, lakini mtu anapokuwa mjamzito kila anapohudhuria kliniki anaelezwa kuwa anatakiwa kufika sehemu ambayo atajifungulia kwa wakati. Wengine wanajifungulia njiani au kupata madhara wakati wa kujifungua kutokana na kuchelewa kwenda hospitalini," anasema Dk Kaizilege.

Yapo mapungufu ya miundombinu, ikiwamo watu kuishi mbali na vituo vya afya, ndiyo maana wanashauriwa kufanya maandalizi kabla ya kujifungua. Nashauri kama mahali anapoishi mjamzito miundombinu ni mibovu ni vyema akahamia karibu na kituo cha afya anapotarajia kujifungulia ili kupata msaada wa haraka ikitokea akapata uzazi pingamizi," anasema.

Kwa upande wake, Dk Joseph Mberesero anasema iwapo hana shida yoyote ya kiafya, mjamzito anaweza asipate madhara makubwa.

“Ujauzito una mambo mengi, kuna wengine unakuta mtoto ni mkubwa hadi anashindwa kupumua vizuri, hivyo ukimweka kwenye pikipiki si sawa. Kuna mwingine kondo la nyuma linakuwa limetangulia, hivyo anaweza akaanza kutokwa damu na wakati mwingine anatakiwa apate usafiri wa gari alale ili sehemu ya shingo ya uzazi isikandamizwe,” anasema.

Anashauri mjamzito apande pikipiki iwapo kuna dharura, lakini si kila siku kwa sababu hawezi kujua iwapo ana shida hadi afike hospitali ndipo aambiwe.

Kwa upande wake, Dk Abdul Mkeyenge wa Hospitali ya Salaaman, anasema madhara kwa matumizi ya pikipiki yanategemea ujauzito ni wa muda gani.

“Kwa aliye hatua za uchungu anaweza akazalia njiani kwa wenye uwezo wa kujifungua wenyewe, lakini kwa asiyeweza upo uwezekano akapoteza maisha yeye na mtoto kutokana na damu kutoka nyingi,” anasema.

Anasema wapo ambao mimba hazitaki purukushani, hasa zikiwa changa, hivyo upo uwezekano ikaharibika kutokana na mtikisiko au akajifungua kabla ya wakati.

Miaka 62 ya mateso kwa wajawazito

Iwapo atatumia usafiri wa pikipiki mara kwa mara kwa safari ndefu na hasa barabara ikiwa mbovu.

Dk Naomi Sanga wa Hospitali za Apollo na Aga Khan anasema hakuna madhara makubwa kwa safari moja, isipokuwa za mara kwa mara kwa mimba changa huongeza hatari ya kuharibika.

“Mjamzito akipanda pikipiki huhisi kichefuchefu anaweza kutapika kutokana na mtikisiko. Upo uwezekano pia wa kutokwa damu na kupata maumivu ya nyonga kwa mimba kubwa. Ubongo wa mtoto na mapigo ya moyo yanaweza kubadilika,” anasema.

Dk Naomi anasema inaweza kusabababisha maumivu ya tumbo na kuachia kwa kondo la nyuma, ijapokuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha usafiri wa pikipiki katika barabara mbovu unaweza ukachangia uchungu kuanza.

Diwani wa Kata ya Kamsamba, Frola Sichalwe anasema, "Tumeamua kufyatua matofali na kujenga jengo lenye vyumba sita ambalo litatumika kama zahanati; ujenzi umefikia eneo la linta. Hata hivyo, tumeshindwa kuendelea kutokana na gharama za ujenzi."

Amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.

Diwani wa Kata ya Kamsamba, Frola Sichalwe anasema, “Tumeamua kufyatua matofali na kujenga jengo lenye vyumba sita ambalo litatumika kama zahanati; ujenzi umefikia eneo la linta. Hata hivyo, tumeshindwa kuendelea kutokana na gharama za ujenzi.”

Amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.

"Tumechoka kuzika wajawazito na watoto. Mjamzito anatembea umbali mrefu akifika hospitalini ameshachoka kiasi kwamba anashindwa hata kusukuma mtoto,” anasema.

Imeandikwa kwa ushirikiano na Bill & Melinda Gates Foundations