ATCL yaongeza safari za ndani, nje ya Tanzania

ATCL yaongeza safari za ndani, nje ya Tanzania

Muktasari:

  • Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeongeza safari zake za ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni kipindi kifupi baada ya ujio wa ndege mbili aina ya Airbus.

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeongeza safari zake za ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni kipindi kifupi baada ya ujio wa ndege mbili aina ya Airbus.

Msemaji wa ATCL, Josephat Kagirwa amesema hayo leo Jumatano Oktoba 13, 2021 wakati akitambulisha safari hizo mpya zinazotarajiwa kuanza Novemba, 2021.

Safari zilizoongezwa ni pamoja na Dodoma-Mwanza, Dar-Mtwara, Dar-Bujumbura, Dar-Lubumbashi pamoja na Dar -Nairobi.

Amesema safari za Dar-Mwanza zitaanza Novemba 5 na Dar kwenda Mtwara Novemba 8 na Novemba 18 ni Dar Lubumbashi-Bujumbura na safari za Nairobi zitaanza Novemba 26.

Kagirwa amesema uwepo wa ongezeko la safari hizo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa mwaka 2017 hadi 2022 ambapo shirika lilijipanga pia kupanua safari zake kwa kuongeza ndege.

“Ujio wa ndege zilizowasili wiki jana Zanzibar umesaidia kuongeza safari nyingine ndani na nje ya nchi, tutafungua safari za Zambia, Burundi Bujumbura, Lubumbashi” amesema.

“Kutakuwa na safari za moja kwa moja kutoka Dodoma kwenda Mwanza lakini pia kupitia Dodoma tumewarahisishia kwamba wanaweza kwenda moja kwa moja. Tulisimama safari za Mtwara sasa tunarudi Novemba 8,” amesema Kagirwa.

Akizungumzia ndege hizo mpya amesema zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 132, na kati ya hao 12 wa daraja la biashara na 120 daraja la uchumi.

Amesema ndege hizo zina mfumo wa kisasa na zimeongezewa uzito hasa wakati wa kuruka kutoka Tani 67 hadi kufikia tani 69.9 lakini pia ina viti vya kisasa ambavyo vitawafanya abiria kustarehe zaidi.

Ujio wa ndege hizo utaifanya Tanzania sasa kuwa na ndege 11.