Bado tunao wahenga leo?

Muktasari:
- Ingawa hakuweka ufafanuzi zaidi juu ya andiko lake, lakini kauli hiyo inatokea kipindi ambacho watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili wanalitumia neno wahenga kwa kasi, hasa katika mitandao ya kijamii.
‘‘Asiye na simu ya kisasa ni mhenga’’ Hii ni kauli ya mmoja wa wanakundi la WhatsApp aliyewaandikia wenzake, akionyesha fasili yake kuhusu neno mhenga.
Ingawa hakuweka ufafanuzi zaidi juu ya andiko lake, lakini kauli hiyo inatokea kipindi ambacho watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili wanalitumia neno wahenga kwa kasi, hasa katika mitandao ya kijamii.
Ni neno lililoteka makundi mengi ya mtandao wa Whatsapp, huku mara nyingi likitumika kuashiria vitu au mambo yaliyofanywa na watu wa zamani.
Ingawa ni neno sahihi la lugha ya Kiswahili, lakini unapoliona na kulitafakari kwa kina hasa linapoambatana na picha zinazotumwa pamoja mitandaoni, linaweza kukufikirisha.
Fikra hii ndiyo iliyosukuma uandishi wa makala hii, huku ikilenga kuweka bayana maana halisi ya neno hilo.
Maana ya wahenga
Mwalimu wa Kiswahili, David Mahenge anaeleza kuwa wahenga ni watu wa kale waliotoa misemo ambayo inatumika kama funzo kwa vizazi vinavyofuatia baada yao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ernesta Mosha ana fasili ifuatayo kuhusu neno wahenga.
“Wahenga ni wingi wa neno mhenga lenye maana ya mtu wa kale mwenye hekima na busara. Ukiangalia namna linavyotumika, ili aweze kuwa mtu mwenye busara, lazima awe ametenda mambo fulani. Na tunavyosema wahenga wetu walisema; inamaanisha ni wale waliotangulia lakini wenye hekima na busara.’’
Kwa mujibu wa kamusi kuu ya Kiswahili, mhenga ni mtu mwenye hekima na busara na mara nyingi huwa na umri mkubwa.
Wahenga wapo hai au wamekufa?
Huu ni utata ambao unajitokeza katika mijadala ya matumizi ya neno wahenga. Mathalani, kwenye mitandao ya kijamii wapo wanaoamini kuwa wahenga ni watu wa kale, wakiamini kuwa wameshakufa hivyo wanakumbukwa kwa kupitia matendo yao.
Inaendelea uk 16
Inatoka uk 15
Hata hivyo, wapo wanaoamini kuwa wahenga wanaweza wakawa bado wanaishi na wanatenda mambo yenye manufaa katika jamii.
Mwalimu Mahenge anashikilia msimamo kuwa wahenga ni wafu waliosema maneno yanayotumika kama misemo yenye kuleta funzo kwa kizazi cha sasa
“Ni watu waliosema maneno ya busara ambayo leo hii tunajifunza kupitia maneno hayo, na pia ujue kuwa wameshakufa,” anasema.
Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Mchungaji Isaya Mbazicha, anasema wahenga ni watu waliopitia mambo mengi katika uhai wao na taarifa zao zinaweza kuwa zimehifadhiwa kwenye vitabu au kuzipata kwenye hadithi.
“Mimi ninavyojua mhenga ni mtu mwenye historia ambaye kumbukumbu zake unaweza kuzipata kwenye vitabu vya historia au hadidhi zinazotoa funzo fulani ila wameshakufa kabisa,” anabainisha.
Mbazicha anaongeza kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuwa inapotosha kwa kuwataja watu wanaoishi kuwa ni wahenga.
Tofauti na mwalimu Mahenge na Mchungaji Mbazicha, mtaalamu wa isimu ya lugha, Sefania Motelwa anaeleza kuwa mhenga anaweza akawa amekufa au yuko hai bado, lakini ni yule ambaye amezungumza kitu fulani chenye funzo.
Motelwa anasema kilicho muhimu, huyu lazima awe na maarifa yanayomwezesha kutafakari kwa kina jambo fulani na kutoa uamuzi unaokubalika.
Kwa upande wake, Dk Mosha anamuelezea mhenga kama mtu wa kale aliyefariki dunia, lakini anakwenda mbali akielezea kuwa mhenga pia anaweza kuwa hai.
“Kwa kuwa maana inatuambia ni mtu wa zamani, swali la kujiuliza je, ni wa zamani tu au hata wa sasa anaweza kuwa mhenga? anahoji na kuongeza:
“Kwa muktadha wa linavyotumika, maana zote zinaweza kuwa sawa. Ni vema kuangalia kamusi tofauti katika kupata maana ya neno hilo, kwa sababu kamusi nyingine zinatoa maana zaidi ya moja.”
Mhenga ni mzee wa baraza
Pamoja na maana ya kwanza iliyobainishwa na kamusi ya Kiwahili sanifu kuwa ni mtu wa kale, lakini kamusi hiyohiyo inatoa maana ya pili kuwa ni mzee wa baraza mwenye maarifa anayetegemewa katika mashauri.
Kwa dhana hiyo, ni dhahiri kuwa wapo wahenga ambao tayari wameshakufa lakini wengine bado wanapatikana katika jamii, wakiendelea kutoa miongozo mbalimbali yenye hekima na busara.
Wahenga na mitandao ya kijamii
Vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii vina nafasi kubwa ya kuathiri matumizi ya lugha na watumiaji wake. Athari hizi zinaweza kuwa hasi ama chanya, hasa kutokana na ukweli kuwa idadi kubwa ya watu wanatumia vyombo hivyo katika mawasiliano.
Vyombo hivi vinapotumia maneno yenye ukakasi, vinaweza kuharibu lugha lakini pale vinapotumia maneno sahihi kulingana na maana sahihi, ni dhahiri vinasaidia kukuza lugha kwa kuwa huwafikia watumiaji wengi.
Neno wahenga limepata umaarufu wa haraka kwa sababu linatumika kwenye mitandao ya kijamii, bila kujali dhana halisi ya maana ya neno hilo.
Mwalimu Mahenge anasema, dhima ya lugha ni pamoja na kuburudisha, hivyo mitandao ya kijamii inaweza kutumia istilahi fulani ikiwa na lengo la utani kwa ajili ya kuwafurahisha wanajamii wenye utamaduni mmoja.
“Kuibuka kwa matumizi ya neno hilo kwa sasa kunaweza kuwafurahisha wengi kwa kuwa mitandao ya kijamii haitumiki tu katika kupashana habari, bali ni pamoja na kuburudishana,” anasema.
Anaongeza: “Picha zinazotumika kwenye mitandao ya kijamii ambazo nyingi zinaambatana na maelezo ya wahenga, sio zote zinazotoa maana halisi bali zaidi ni katika kuburudishana.’’
Hata yeye anasema anafurahishwa na baadhi ya picha zinazotumwa kwenye makundi ya WhatsApp zikiwaonyesha watu wanaodaiwa kuwa ndio wahenga.
Inawezekana matumizi ya neno wahenga kwenye mitandao ya kijamii, ni kudhihirisha ile nadharia ya lugha ya ukuaji.
Inawezekana pia wapo wengi ambao walikuwa hawajui hata hilo neno, lakini kupitia mitandao ya kijamii, wamefunguka kimaarifa.
Hata hivyo, kwa kuwa tabia ya binadamu ni kuwa na shauku ya kujua kile kigeni anachokutana nacho, ikiwa ni pamoja na maneno yanayomtatiza, hatuna budi kujihangaisha kutafuta dhana na maana sahihi ya maneno mbalimbali ya Kiswahili.
Ni wakati mwafaka kwa taasisi zinazohusika katika taaluma za lugha hasa ya Kiswahili, kunusa matakwa ya watumiaji wa lugha na pale inapobidi, zije na istilahi mpya au kuziongezea maana za ziada zilizopo.
Huku ndiko kukuza na kuitunza lugha yetu. Chambilecho wahenga: Kitunze kidumu.
0753590823