Bosi wa zamani NIC kortini kwa uhujumu uchumi

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Samuel Kamanga na wenzake sita, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 365 yakiwemo ya kughushi na kutakatisha fedha kiasi cha Sh 1.8bilioni mali ya NIC.

Washtakiwa hao wamefikisha mahakamani hapo jana, Juni 2, 2023 na kusomewa mashataka ya uhujumu uchumi namba 18/2023 na wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Mwanga akishirikiana na Ipyana Mwakatobe.

Hata hivyo, washtakiwa hao wamesomewa mashtaka 101 tu, huku mashtaka mengine wakitarajia kusomewa Jumatatu, Juni 5, 2023 kutokana na muda wa Mahakama kuisha.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu, Evodia Kyaruzi.

Katika mashtaka hayo 365, yapo ya kughushi nyaraka mbalimbali, kutakatisha fedha, kuongoza genge la uhalifu, kuchepusha fedha, kuwasilisha nyaraka za uongo na kulisababishia hasara shirika hilo.

Mbali na Kamanga, washtakiwa wengine ni Tabu Kingu, Victor Mleleu, Peter Nzunda, Kenan Mpalanguro, Lusubilo Sambo na Mafworo Ngereji.